CCM: Anayetaka kutushinda akaribie uwanjani Oktoba

Muktasari:
- Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumanne Aprili 29, 2025 Mwananyamala wilayani Kinondoni, Amos Makalla amesema CCM haijiweki yenyewe madarakani bali kwa matakwa ya wananchi hivyo vyama vinavyotaka iondoke madarakani basi vijipange Oktoba.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema vyama vya siasa vinavyotangaza nia ya kuiondoa CCM madarakani vijiandae kukutana nayo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya vyama mbalimbali vya upinzani vikiwamo vya Chadema, ACT Wazalendo na CUF vimekuwa vikitamba kwamba vimedhamiria kuiondoa CCM madarakani hivyo wanawaomba Watanzania kuwaunga mkono katika harakati hizo.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumanne Aprili 29, 2025 Mwananyamala wilayani Kinondoni, Dar es Salaam Makalla amesema CCM haijiweki yenyewe madarakani bali kwa matakwa ya wananchi hivyo vyama vinavyotaka iondoke madarakani basi vijipange Oktoba.
"Kila uchaguzi CCM inachaguliwa kutokana na ushawishi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotatua kero za Watanzania, ndio maana wananchi bado wanaendelea kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi," amesema.
"Kwa hiyo watakaotaka (vyama vya siasa) waje sisi (CCM) tupo tayari, ndio maana nimesimama hapa kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi kuwashukuru kwa namna mnavyokiunga mkono," amesema Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.
Ametumia nafasi hiyo, kuwashukuru wananchi wa Kinondoni kwa kukipigia kura kwa wingi chama hicho na kukihakikishia ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27,2024.
Makalla ambaye ni mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es Salaam, amewataka WanaCCM kuendelea kujivunia na kulinda mafanikio yaliyopo katika Serikali na CCM, badala ya kubeza kila juhudi mbalimbali zinazofanyika.
Katika hatua nyingine, Makalla amewataka Watanzania kuwa makini na kuwakataa baadhi ya watu aliodai wanaeneza siasa za chuki kwa lengo la kusababisha uvunjifu wa amani.
Hata hivyo, Makalla aliyewahi kuwa mbunge wa Mvomero mkoani Morogoro, amewahakikishia Watanzania muda ukifika mchakato wa uchaguzi mkuu utakafanyika kwa amani na utulivu na wananchi wasiwe na wasiwasi badala yake wajitokeze kushiriki.
"Kuanzia sasa na baada ya uchaguzi mkuu, Serikali itahakikisha inaimarisha amani na utulivu, hii ndio dhamana ya CCM iliyoiweka Serikali madakarani. Niwaombe Watanzania tusimame na Rais Samia Suluhu Hassan, nchi imetulia, Tanzania ni mahali salama," amesema Makalla.
Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas amemwambia Makalla katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mbalimbali ya afya, masoko, barabara katika kata 10 za jimbo hilo ili kurahisisha huduma za wananchi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Juma Simba 'Gaddafi' tujiandaae kwa uchaguzi wa Oktoba na kura zote za udiwani hadi urais ziende wagombea wa chama hicho tawala.