Makalla awajibu wapinzani mafanikio Bandari ya Dar es Salaam

Masasi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kampuni ya DP World umeongeza mapato, idadi ya makasha yanayoingia na kupungua kwa siku ya meli kukaa bandarini
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ameeleza hayo leo Aprili 17, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ikiwa ziara yake ya siku kumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makalla ameeleza hayo akijibu hoja ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche aliyedai kuwa nchi yetu imeshindwa kuendesha bandari na kuwapa watu binafsi.
Makalla amesema mtoa hoja hajui mambo ya uchumi na biashara anahitaji aelimishwe faida za uwekezaji na uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa moja ya bandari yenye ufanisi Afrika Mashariki na Kati.
Pia, amesema kuwa makaa ya mawe kuuzwa nje ya nchi ni fursa nzuri inayosaidia Serikali na taifa kwa ujumla kuongeza mapato na fedha za kigeni zinazosaidia kufanya maendeleo ya nchi kutokana na masoko yanayopatikana nje ya nchi.
“Kuwa na makaa ya mawe ni fursa kwa sababu yanatumika katika kazi mbalimbali na hapa ndani ya nchi, uhitaji wa makaa ya mawe ni mkubwa katika kwenye viwanda vyetu,” amesema Makalla.
Ameongeza: “Kwa hiyo namwambia John Heche mbali ya kupata fursa ya masoko nje ya nchi na kutuingizia fedha za kigeni ambazo tunazipata na tunapata kodi yetu na Rais (Samia Suluhu Hassan) anapata uwezo wa kujenga shule, kuweka miradi ya maji na kujenga barabara.
Pia, Makalla amesema kuwa Tanzania makaa ya mawe yanatoka kusini na kuna viwanda vya saruji nchini ambavyo vinahitaji uwepo wa makaa ya mawe kikiwemo Kiwanda cha Saruji cha Wazo, Tanga Cement na Dangote vyote vinauhitaji wa malighafi hiyo.