Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanuni za maadili uchaguzi Rais, Wabunge, Madiwani kuanza rasmi

Muktasari:

  • Tayari kanuni hizo zimechapishwa kwenye gazeti la Serikali hivyo, kuashiria kuwa ni rasmi kuanza kutumika na hatua zingine za uchaguzi kuendelea.

Dar es Salaam. Sasa rasmi, Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, zitaanza kutumika baada ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.

Kuanza kutumika kwa kanuni hizo kwa mujibu wa wataalamu wa sheria, kunakwenda sambamba na sharti la kutohojiwa au kupingwa na yeyote hadi mahakama itakapobatilisha.

Hatua hiyo ya kuchapishwa kwa kanuni hizo, inafungua milango kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuendelea na michakato mingine ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, tayari INEC imeshatangaza kuanza kwa ratiba ya awamu ya pili ya uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la mpigakura.

Kanuni hizo zilizochapishwa, ndiyo zile ambazo vyama 18 vya siasa vimezisaini, isipokuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku INEC ikiweka bayana kwamba, hatua ya chama hicho kutozisaini, kimejiengua na kukosa sifa ya kushiriki uchaguzi kwa miaka mitano.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima alitoa kauli hiyo Aprili 11, 2025 na kuirudia tena Aprili 12, 2025, akirejea kifungu cha 1.5 cha kanuni hizo.

Kifungu hicho kinasema, “kila chama cha siasa, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi watawajibika kusaini kanuni hizi za Maadili. Chama cha siasa ambacho hakitasaini kanuni hizi za maadili kitazuiliwa kushiriki katika uchaguzi.”

Kifungu hicho na kauli ya INEC, kumeibua mjadala kwa baadhi ya wanasheria na wadau wa uchaguzi kuwa kanuni hiyo haijaweka wazi ukomo wa kusaini.

Kwa kutoweka ukomo, wadau hao wanasema chama cha siasa kinaweza kusaini siku yoyote, tofauti na Aprili 12, 2025 iliyopangwa na INEC.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema kilichozungumwa na tume hiyo ni tafsiri yao huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama.

“Mahakama ni mtafsiri wa mwisho inaweza kusema kipi sahihi, ni suala la kutafsiri tu Katiba imesema hivi na sheria zinasema hivi na Kanuni zinasema hivi kwahiyo msimamo ni upi. Tume huru ya Uchaguzi tulitoa tafsiri yetu maana yake wewe usipo saini hutashiriki kwenye uchaguzi,” amesema.


Marufuku kuhoji

Akizungumzia hilo, Wakili August Mramba amesema kuchapishwa kwa kanuni hizo, ndio kunaruhusu kuanza kutumika kwake.

“Kanuni yoyote au marekebisho yoytote ya sheria haiwezi kutumika kama haijachapishwa kwenye Gazeti la Serikali,” amesema.

Amesema katika hatua hii, kanuni hizo hazipaswi kuhojiwa na yeyote hadi utakapofika wakati mahakama ikabatilisha kwa kusema kifungu kinachozuia kuhojiwa kipo kinyume na katiba.

“Kama mahakama haijatamka kwamba hicho kifungu ni uncosistitutional hautaruhusiwa kusema chochote, hadi mahakama itamke kuwa kifungu hicho ni kinyume cha katiba,” amesema.

Amesisitiza kifungu cha kuzuia ukaguzi wa mahakama katika sheria ya utawala ni kipengele ndani ya sheria kinacholenga kuzuia au kupunguza uwezo wa mahakama kupitia mchakato wa kuangalia upya uamuzi uliofanywa na taasisi za umma.

“Kifungu hiki huwa na nia ya kuondoa mamlaka ya usimamizi wa mahakama juu ya hatua fulani, kwa hoja kwamba jambo hilo linafaa kushughulikiwa zaidi kwa uwajibikaji wa kisiasa badala ya ule wa kisheria,” amefafanua.

Wakili Michael Mushi amesema kuchapishwa kwa kanuni hizo kunamaanisha kwamba, zimeshakuwa rasmi kutumiwa na wahusika.

“Zikichapishwa zinapaswa kufanyiwa kazi, kwa sababu kuwa katika Gazeti la Serikali ndio unakuwa msimamo,” amesema.

Kwa upande wa Wakili Dominic Ndunguru amesema ni takwa la kisheria kwa kanuni na sheria baada ya kujadiliwa, zinapaswa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

Hatua hiyo, amesema inamaanisha rasmi kanuni au sheria husika inastahili kutumika na umma.

“Kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali kunamaanisha umma unaarifiwa kuwa, sheria au kanuni husika, sasa iko tayari kutumika,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza pamoja na kuchapishwa, wananchi wana haki ya kuhoji kwa mujibu wa sheria, hasa iwapo wataona kipengele kinachokiuka haki zao.