Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makalla: Chadema kubaki jukwaa la harakati, Golugwa ajibu mapigo


Muktasari:

  • Makalla amesema lengo la chama cha siasa ni kushika dola na katiba ya Chadema ibara ya nne inaeleza kitashiriki uchaguzi na kushika dola, sasa kwa miaka mitano hakitashiriki uchaguzi, kitabakia kuhamasisha watu kuandamana.

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amedai baada ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2025, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitabakia jukwaa la harakati sio chama cha siasa.

Amesema lengo la chama cha siasa ni kushika dola na katiba ya Chadema ibara ya nne inaeleza kitashiriki uchaguzi na kushika dola, sasa kwa miaka mitano hakitashiriki uchaguzi, kitabakia kuhamasisha watu kuandamana.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa amesema chama hicho sio tawala.

“Kuitwa chama cha harakati siyo tusi na lazima kifanye kazi za harakati,”amesema Golugwa.

Msingi wa hoja ya Makalla, umetokana hatua ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutangaza Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu baada ya kugomea kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima alitangaza Chadema kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni. 

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala aliwataka watendaji wa INEC wajitathimini kama wanaweza kutekeleza majukumu yao baada ya kueleza kuwa, Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kutokana na kugomea kusaini kanuni za maadili. 

Akijibu madai hayo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama. 

Makalla ameeleza hayo leo Jumatatu Aprili 28, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kimara wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam. Mwenezi huyo ameanza ziara ya siku tatu ya kuimarisha chama mkoani Dar es Salaam.

Katika hotuba yake Makalla amesema lengo la chama cha siasa ni kushika dola, hivyo kati ya vyama 19, Chadema pekee ndiyo hakijasaini kanuni hizo na kukosa sifa za kushiriki uchaguzi huo ambao kwa mara kwanza utasimamiwa na INEC.

"Hawa (Chadema) watakuwa kama Jukwaa la Katiba (Jukata), unajua jukwaa la harakati kazi yake ni harakati. Sasa hivi ukiwauliza Chadema wanataka nini hawana majibu, kwa sababu limekuwa jukwaa la harakati.

"Hivi mtani wangu Heche (John) unaposema Ukonga, Kigamboni, Ilala, Ubungo na Kinondoni waje mahakamani kwa akili ya kawaida inawezekana? Maana yake ndio jukwaa la harakati yaani lazima uwe mtu wa mishemishe na vuruguvurugu," amesema Makalla.

Amedai wanachokifanya Chadema kwa sasa ni harakati, akiwataka Watanzania kutambua kuwa chama hicho kikuu cha upinzani hakina nia njema na Tanzania kwa kuifanya isitawalike.

Akijibu hoja hiyo, Golugwa amesema:"Ni kweli chama cha siasa lazima kifanye siasa, kwa sababu Chadema si chama tawala, tukiitwa chama cha harakati sio tusi ni sahihi, lazima tufanye harakati zetu."

"Tunazipata ajenda kutokana na watu wenyewe na mazingira, kwa hiyo kuitwa chama cha harakati sio tusi, ni kweli tunafanya harakati kwa sababu sio chama tawala na tutaendelea kufanya harakati, hayo maneno yake tunayaapuzia tu," amesema Golugwa alipozungumza Mwananchi.

Adai Chadema kutumiwa

na watu wa nje

Katika mkutano huo, Makalla amedai Chadema ipo katika biashara ya kuwafurahisha watu wanaowatuma aliodai wapo nje ya nchi.

"Fanyeni hiki na kile tutumieni na picha, hamasisheni watu tunajua nawaomba Watanzania tulinde amani...Nawaomba wafuasia wa Chadema, akili za kuambiwa changanya na za kwako, msikubali kutumika," amesema.

"WanaChadema amkeni msikubali kutumika, kuna watu wapo nje ya nchi wanawatuma viongozi wenu tunajua, hatuendi hivyo, yote haya ni... ili watu wanaowatuma wasema Tanzania kuna tatizo, niwaambie chini ya Tanzania hakuna mgogoro wa siasa na mtu yeyote na tunabishana kwa itikadi," amesema Makalla.

Akizungumzia hatua hiyo, Golugwa amesema Makalla amekuwa akitoa kauli zinazozua utata na si mara kwanza akifanya hivyo, lakini mwenezi bado hajajifunza na matamshi yake.

"Sisi tunafanya hivyo kwa sababu mwenyekiti wetu (Tundu Lissu) yupo mahakamani, yaani mwenyekiti wetu yupo mahakamani tututumiwe na mtu wa nje kwenda? Kwani hatuwezi kuona hili?

"Hii si mara kwanza Makalla kuongea maneno kama haya, Chadema hatutumiwi na mtu tunakwenda kwa sababu ni mwenyekiti wetu, kama ambavyo CCM wanamsifia mwenyekiti wao ( Rais Samia Suluhu Hassan).

Makalla ambaye ni mlezi wa CCM wa Dar es Salaam, amesisitiza uchaguzi utafanyika kwa mujibu wa Katiba si takwa la CCM, hivyo kwa mazingira yaliyopo Chadema wasahau kushiriki baada ya viongozi wao kutosaini kanuni hizo.

Katika hatua nyingine amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuendelea kukiamini chama hicho, kwa kuhakikisha wanakiunga mkono tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye.