Kesi ya 'Bwana harusi' yakwama kwa mara ya pili, sababu zatolewa

Mshtakiwa Vicent Masawe (aliyevaa kofia) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi ya wizi wa gari inayomkabili kuahirishwa leo Jumanne Januari 7, 2025. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Masawe katika kesi hiyo anakabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la wizi wa gari aliloazimwa kwa matumizi siku ya harusi yake.
Dar es Salaam. Serikali imeshindwa kumsomea maelezo ya awali (PH) "Bwana Harusi" Vicent Masawe (36) anayekabiliwa na kesi ya wizi wa gari aina ya Ractis, kutokana na mawakili wanaoendesha kesi hiyo kuwa kwenye kikao cha mawakili mkoani Dodoma.
Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kuahirishwa ikiwa katika hatua ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH) kwani Machi 24, 2025 kesi hiyo iliahirishwa kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo mahakamani hapo siku hiyo.
Masawe anakabiliwa na mashitaka mawili ambayo ni wizi wa gari aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni ambalo aliazimwa kwa ajili ya kulitumia katika sherehe ya harusi yake, na kujipatia fedha taslimu Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Hata hivyo, leo Jumatatu Aprili 14, 2025 kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya Serikali kumsomea hoja za awali mshtakiwa, lakini wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama ya Hakimu Kisutu, kuwa mawakili wanaoendesha kesi hiyo wapo mkoani Dodoma kwenye kikao cha mawakili wa Serikali.
Kamala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki anayesikiliza kesi hiyo.
Wakili Kamala amedai kutokana na mawakili hao kuwa kwenye kikao, upande wa mashitaka unaomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomewa hoja za awali.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29, 2025 kwa ajili ya kumsomea hoja za awali na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.
Katika kesi hiyo ya jinai, Massawe anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 15, 2025 kinyume na vifungu namba 258 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kwa mara ya kwanza Massawe alipandishwa mahakamani Desemba 24, 2024 na kusomewa mashitaka yanayomkabili.
Katika shitaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa akiwa wakala, Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari lenye namba aina ya Toyota Ractis.
Gari hilo lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashitaka ni mali ya Silvester Masawe.
Anadaiwa kuwa aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake lakini baada ya hapo, hakurudisha kama ambavyo walikubaliana.
Katika shitaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kuwa tarehe hiyohiyo ya tukio katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh3 milioni kutoka kwa Silvester.
Anadaiwa kuwa alijipatia fedha hizo kwa kuahidi kuwa atamrudisha baadaye, wakati akijua kuwa ni uongo na hakuzirudisha hadi alipokamatwa.
Kabla ya kukamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka hayo, Massawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es salaam alidaiwa kupotea.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Novemba 18, 2024 Massawe ambaye alikuwa fungate baada ya kufungua ndoa, alitoa taarifa kwa marafiki zake kuwa alikuwa Mbezi na alikuwa anafuatiliwa na gari ambalo alikuwa halijui.
Tangu siku hiyo, hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.
Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.
Kamanda Muliro alisema kuwa Massawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba na alikuwa na tuhuma za wizi wa kuamiwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.
Alieleza kuwa kutoka na tuhuma hizo ndio maana alitengeneza mazingira ya uwongo kwamba amepotea kisha akaenda kujificha kwa mganga huyo wa kienyeji.
Hata hivyo alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka hayo, Massawe alikana na aliachiwa kwa dhamana.