Washauri Lugalo kujengwe kituo cha Utalii, Chuo cha Diplomasia badala ya kubaki pori

Baadhi ya wadau wa utalii wakiwa katika kaburi la nyundo ambalo inadawa kiongozi wa Wajerumani, Von Zelewsk na askari wake walizikwa baada ya kuchapwa wakati wa vita baina yao na Mkwawa katika eneo la Lugalo, Wilayani Kilolo.
Muktasari:
- Wadau wa Utalii kutoka mikoa 10 ya kusini mwa Tanzania wameshauri eneo la Lugalo ambalo lilikuwa uwanja wa vita baina ya Chifu Mkwawa na wajerumani kijengwe kituo cha Utalii na chuo cha Diplomasia.
Iringa. Wadau wa Utalii kutoka katika mikoa 10 ya kusini mwa Tanzania wametembelea eneo la Lugalo ambalo lilitumika kama uwanja wa vita baina ya Chifu Mkwawa na wajerumani na kushauri kijengwe kituo cha utalii na chuo cha Diplomasia.
Mkwawa na Wajerumani walipigana vita mwaka 1891 katika eneo la Lugalo, Wilayani Kilolo ambalo lilipata umaarufu baada ya kiongozi huyo wa wahehe na jeshi lake kushinda licha ya kuwa na silaha duni.
Kiongozi wa Wajerumani, Von Zelewsk na askari wake walizikwa kwenye eneo la Lugalo ambalo limejengwa kaburi linaloitwa Nyundo huku likizungukwa na pori.
Kutoka na umuhimu wa historia hiyo ya ushindi wa Mkwawa, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Boma Iringa Jimson Sanga amesema upo umuhimu wa kujengwa kituo cha utalii na chuo cha Diplomasia.
"Bonde hili limebeba historia yenye ushindi ndani yake, ilikuwa vita iliyompatia Mkwawa ushindi, hapa pasibaki pori,bonde hili liwe kituo cha utalii," amesema Sanga na kuongeza;
"Wataalamu na wanazuoni pia wafanye tafiti tujue familia za kiafrika ambazo zilipoteza askari hapa, ushindi alipata Mkwawa lakini wapo Askari wake waliouawa,"
Mdau wa Utalii kutoka Morogoro, John Joseph ameshauri ka sasa kiwekwe kibao au alama itakayokuwa ikiwajulusha watu juu ya eneo hilo la Lugalo.
"Ukipita barabarani huoni chochote, naijua historia ya Mkwawa, nalijua jina la Lugalo lakini sikuwa najua kama ni hapa kwa sababu hakuna kinachoonyesha zaidi ya kaburi la nyundo," amesema Joseph.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Laili Kamendo amesema mkakati wao ni kujenga shule na kuweka alama ili wanaopita eneo hilo lililo Barabara Kuu ya Tanzam, waijue historia ya Lugalo.
"Shule itajengwa kilometa chache kutoka hapa na tayari fedha zimeshatolewa," amesema Kamendo.