Wanahabari waeleza changamoto za tasnia, mradi wa kuwajengea uwezo ukizinduliwa

Wanahabari nguli, Edda Sanga (wa tatu kulia) na Wenceslaus Mushi (kulia) wakishiriki kuzindua mradi wa kuwajengea uwezo wana habari unaotekelezwa na Taasisi ya Kimataifa ya masuala ya kusaidia Vyombo vya Habari ( IMS) kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na JamiiAfrica chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), mradi huo utafanyika nchini kwa miaka mitatu.
Muktasari:
- Wataja ukuaji wa teknolojia umesababisha uwepo wa habari nyingi feki, jambo ambalo linahitaji sapoti ili kukabiliana nalo.
Dar es Salaam. Wanahabari wameeleza changamoto zinazoikabili tasnia hiyo katikati ya ulimwengu wa teknolojia na akili mnemba.
Wamesema ukuaji wa teknolojia umesababisha uwepo wa habari nyingi feki, jambo ambalo linahitaji sapoti ili kukabiliana na changamoto hiyo ili kutoiweka jamii njia panda.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa programu maalumu ya kuwajengea uwezo wanahabari ili kuepuka kuingia kwenye mtego wa habari feki sambamba na kujikita kuandika habari zinazohusu watu na maendeleo, baadhi ya wanahabari wamesema katikati ya ukuaji wa teknolojia kumekuwa na changamoto ya uwepo wa habari feki pia.
Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya amesema katika ulimwengu wa teknolojia na akili mnemba (AI) wanahabari wanapaswa kupata taarifa, kutoka kwenye vyanzo na kwa wakati sahihi.
Amesema jambo la kupata taarifa sahihi kutoka kwa watu sahihi ni miongoni mwa mambo ambayo klabu hiyo kwa kushirikiana na JamiiAfrica na IMS imeyazingatia katika kuwajengea uwezo wanahabari kukabiliana nayo kwenye ulimwengu wa teknolojia, kipindi ambacho habari feki zinasambazwa kwa wananchi.
"Tunakwenda kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili jamii iweze kupata taarifa sahihi, kwa wakati sahihi na muda sahihi.
"Wanahabari wanapaswa kuangalia masilahi ya wananchi, kuandika habari ambazo zinahusu watu na maendeleo," amesema Simbaya akisisitiza kwamba uandishi unaogusa jamii unaanza kukosekana.
Mwanahabari nguli, Edda Sanga amesema miaka ya nyuma vyombo vya habari havikuwa vingi.
"Uchache huu ulisababisha habari zilizotoka kuwa zilizothibitishwa na zenye uhakika, tofauti na sasa ukuaji wa teknolojia umesababisha habari nyingine kuwa feki," amesema.
Mwanahabari mwingine, Imani Luvanga amesema kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia maendeleo ya kidijitali ni wakati sahihi wa wanahabari kujengewa uwezo wa namna ya kutumia teknolojia ipasavyo.
"Lakini waandishi profesheno wakijengewa uwezo, itasaidia kupunguza hizi habari feki, na wao kutoingia kwenye mkumbo wa habari za kughushi ambazo hazijafanyiwa utafiti kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya habari," amesema.
Kuhusu mradi
Akizungumzia mradi wa kuwajengea uwezo wanahabari unaotekelezwa na Taasisi ya Kimataifa ya masuala ya kusaidia Vyombo vya Habari ( IMS) kwa kushirikiana na UTPC na JamiiAfrica chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiAfrica, Maxence Melo, amesema mradi huo ni wa miaka mitatu.
Amesema mradi huo uliobuniwa mwaka 2022 utafanyika kote nchini kuanzia mwaka huu.
"Lengo kuu la mradi ni kuwajengea uwezo wanahabari, kuandika habari ya uhakika ambazo zitagusa zaidi masilahi ya wananchi," amesema.
Amesema pia utawajengea uwezo wanahabari juu ya kutumia teknolojia ya akili mnemba (IA) na namna ya kukabiliana na taarifa za upotoshaji ili kuepusha kutowaweka wananchi njia panda wanapokutana na habari feki.