Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi Simanjiro wanufaika na chakula cha msaada

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Merika Makeseni (wapili kulia) na baadhi ya viongozi wa shule ya msingi Naisinyai, baada ya kupokea msaada wa magunia 120 ya mahindi, magunia 20 ya maharage na mafuta ya kupikia ndoo 20 za lita 400, uliotolewa na kampuni ya Franone Mining and Gems LTD. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Jamii ya wafugaji wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imekumbwa na ukame hivyo kushindwa kuchangia chakula hadi kusababisha Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kuchangia mahindi magunia 120, maharage gunia 20 na mafuta ya kupikia ndoo 20 za lita 400.

Simanjiro. Wanafunzi wa shule mbili za msingi Naisinyai na Oloshonyokie za Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula kutokana na ukame uliozikumba familia zao, wamenufaika na msaada wa vyakula na mafuta vilivyotolewa na kampuni ya Franone Mining and Gems LTD.

Msaada huo wa magunia 120 ya mahindi, magunia 20 ya maharage na ndoo 20 za lita 400 za mafuta ya kupikia umetolewa na kampuni hiyo ya uchimbaji madini ya Franone Mining and Gems LTD inayochimba madini ya Tanzanite kitalu D na wamiliki wa kitalu C.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Septemba 12, 2023 amesema msaada huo umekuja kwa wakati mwafaka hivyo wanaishukuru Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD.

Amesema kwa moyo wa dhati na kwa niaba ya jamii nzima ya wana Naisinyai, anawashukuru wakurugenzi na uongozi wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kwa msaada mkubwa waliotoa kwa shule zetu za msingi Naisinyai na Oloshonyokie.

"Kimsingi maeneo yetu kama yalivyo maeneo mengi ya nchi yetu kwa miaka mitatu yamekumbana na changamoto ya ukosefu wa chakula hali iloyotokana na mvua kuwa chache kutokana na nchi kukabiliana na mabadiliko makubwa ya tabia nchi," amesema Merika.

Amesema hali hiyo pia imesababisha mifugo mingi ambayo ni tegemeo kubwa kwa jamii ya wafugaji kufa na michache iliyobaki kudhoofu kiasi cha kutouzika kirahisi na kwa bei rafiki.

Amesema kutokana na hali hiyo wakaamua kuwashirikisha wadau wa maendeleo kwa mwaka huu walau waweze kusadia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi ambao kwa kawaida huchangiwa na wazazi.

"Niwashukuru viongozi wenzangu waliotupa ushirikiano katika hili ambao ni mheshimiwa mkuu wa wilaya Suleiman Serera, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri Gracian Makota, Ofisa tarafa Moipo Dhulfa Laizer  na mheshimiwa Diwani wa kata Taiko Laizer kwa namna walivyojitoa kuhakikisha tunafanikisha hili," amesema.

Amesema ni ahadi yake na kamati za shule kuwa chakula hicho watakisimamia kukihifadhi na kuhakikisha kuwa kitatumika kwa lengo lililokusudiwa.

"Ni maombi yetu kwa Mungu wetu kuwabariki Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD na kuwajazilizia wale waliokitoa ili wasijutie wao kwa kutoa sadaka hii kubwa kwa watoto wetu," amesema Merika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Naisinyai, Agnes Chanindo ameishukuru Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kwa msaada huo wa chakula cha wanafunzi hao.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Tauta Siria amesema watahakikisha chakula hicho kinatumika ipasavyo kwa lengo husika lililokusudiwa.