TLS: Utekaji, upoteaji watu Serikali iunde chombo kusimamia vyombo vyake

Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi.
Muktasari:
- Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi amesema kwa kuzingatia mazingira ya kiusalama kwa rai ana kukithiri kwa vitendo vya utekaji na kupotea watu huku Jeshi la Polisi likilaumiwa ni wakati wa Serikali kuunda chombo maalumu cha kuangalia namna wananchi wanahudumiwa katika ‘law enforcement agency’
Arusha. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeiomba Serikali kuunda chombo maalumu cha kisheria kusimamia vyombo vya dola, kufuatia ongezeko la matukio ya utekaji na upoteaji wa watu, ambapo Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa.
Kwa mujibu wa Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, kutokana na lawama zinazoendelea kuelekezwa kwa Jeshi la Polisi katika matukio ya utekaji na upoteaji wa watu, amesema umefika wakati mwafaka kwa Serikali kuunda chombo huru cha kisheria chenye mamlaka ya kusimamia na kufuatilia kwa karibu utendaji wa vyombo vya utekelezaji wa sheria na namna vinavyowahudumia wananchi.
Pia, Mwabukusi amesema TLS ni kama ‘shangazi’ ambaye huonya kwa upendo, hata pale onyo lake linapokera, akisisitiza kuwa jukumu lake si kwa maslahi binafsi, bali kwa ajili ya kulinda taifa na kusimamia utawala bora wa sheria.
Kuhusu nafasi ya chama hicho, Wakili Mwabukusi amesema kuwa TLS inatekeleza majukumu yake kwa misingi ya uwajibikaji, uadilifu, upendo na utii kwa mamlaka halali za nchi, hivyo wanapaswa kuvumiliwa na kueleweka kwani hawana maslahi binafsi bali wanatumikia maslahi mapana ya taifa na kulinda misingi ya utawala wa sheria.
“TLS ina role ya ‘shangazi’, kwa hiyo kuna wakati inakusema, ukinuna unune, shangazi atasema tu atakemea atafinya kidogo ila mwisho wa siku shangazi hakuchukii hata wakati unaondoka, atakupa kibuyu cha maziwa, huo ni upendo,” amesema.
Wakati TLS ikitoa msimamo huo, Serikali imesisitiza kuwa mawakili wana nafasi ya kipekee kutumia taaluma yao kulinda haki za wananchi, kupambana na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, na kuhakikisha kuwa haki inapatikana mahakamani.
Kauli hiyo imetolewa Alhamisi, Mei 8, 2025 na Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, wakati akihutubia mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho unaofanyika jijini Arusha na utamalizika kesho Mei 10, 2025.
Mwabukusi amesisitiza kuwa utawala bora ndio msingi imara wa demokrasia, na kwamba kutokana na hali halisi ya utendaji wa vyombo vya utoaji haki, hususan Jeshi la Polisi katika mazingira yanayoathiri usalama wa raia na kuongezeka kwa matukio ya utekaji na upoteaji wa watu, kuna haja ya hatua madhubuti kuchukuliwa.
“Pamoja na kushamiri desturi ya kuwa na vitu vinavyoitwa vikosi kazi (task force) za polisi ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria.
“TLS inatoa rai kuwa ni wakati muafaka kwa Serikali kuona umuhimu wa kuunda chombo maalumu cha kisheria kitakachosimamia na kuangalia namna wananchi wanatendewa haki na vyombo vya utoaji haki,” amesema.
Wakili Mwabukusi amesema kuwa, katika hatua za dharura, Serikali inapaswa kuboresha mamlaka, uwezo, uhuru na ufanisi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili iwe taasisi huru inayojitegemea kikamilifu.
Amesema licha ya tume hiyo kuruhusiwa kisheria kufanya kazi kama tribunal (baraza) katika baadhi ya maeneo, bado inakumbwa na changamoto ya utegemezi kwa Serikali, hasa pale inapohitaji kushtaki kwa niaba ya wananchi.
“Kwa sasa, ili ishtaki mtu anayelalamikiwa, inatakiwa iombe msaada wa wanasheria kutoka serikalini, hii ni sawa na kumpa mtu mpira na jezi, lakini usimpe uwanja wa kuchezea,” amesema Mwabukusi.
Ameongeza kuwa ni muhimu eneo hilo liangaliwe upya ili kuiwezesha tume hiyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, akisisitiza kuwa ikipewa nafasi ya kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazolalamikiwa na kuwa sauti ya wananchi katika kulinda haki zao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais– Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Boniface Simbachawene ameitaka TLS isaidie kulinda demokrasia kwa kuwa yenyenewe ni msingi wa ushauri wa kisheria.
Amesema Serikali iko tayari kuendelea kupokea ushauri wa kitaalamu kutoka kwa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya kisheria kwa lengo la kuimarisha taasisi na mifumo ya utawala bora.
“Ndio maana nilipokuwa nakusikiliza, Mwabukusi, nilifurahi kuona hujasema ‘No reforms, no election’… umetoa mawazo ya kujenga. Umesema kama muda upo, basi sheria zenye ukakasi zinaweza kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi wa Oktoba. Huo ni mtazamo mzuri,” amesema Simbachawene.
Akizungumzia mvutano kuhusu muda wa kufanya marekebisho ya sheria kabla ya uchaguzi, Waziri huyo alibainisha kuwa yapo makundi yenye maoni tofauti, wapo wanaosema muda unatosha na wapo wanaodhani muda hautoshi.
Simbachawene amesisitiza kuwa jambo la msingi ni kuangalia maslahi ya taifa, si ya pande fulani.
“Lazima tuheshimu maoni ya pande zote; tunachokilinda ni maslahi ya Mtanzania. Tusipokuwa makini, tunaweza kurudisha nyuma taifa kwa kushinikiza mchakato ambao muda haukutosha,” amesema.
Akitumia lugha ya picha, Simbachawene aliifananisha TLS na “shangazi wa kweli” anayekaa katikati, akieleza kuwa chama hicho mara nyingine huonekana kukosolewa na pande zote kwa sababu ya msimamo wake wa kuonya na kuelekeza kwa haki.
“TLS muendelee kuwa shangazi wa kweli, msimame katikati, mchape inapobidi, lakini muendelee kuwa walinzi wa haki, watetezi wa demokrasia na sauti ya busara kwa taifa hili,” amesema.
Mkurugenzi wa TLS, Mariam Othman amesema ajenda kuu ya mkutano wa mwaka huu inalenga kutathmini uhusiano kati ya uchaguzi na utawala wa sheria, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amesema mada mbalimbali zitakazowasilishwa zitachambua jinsi sheria, mwenendo wa taasisi za umma na mifumo ya uwajibikaji vinavyoathiri uhalali, uwazi na uaminifu wa uchaguzi.
“Kupitia uwasilishaji wa mada hizo, tunakusudia kubainisha changamoto za kisheria na kitaasisi zinazokwamisha uchaguzi huru na wa haki, pamoja na kutoa mapendekezo ya mageuzi yatakayosaidia kuimarisha misingi ya uchaguzi wa haki, usawa na uwajibikaji,” amesema Mariam.
Amesisitiza kuwa mkutano huo unalenga kuhimiza mshikamano wa kitaifa na kuchochea hatua za makusudi katika kuimarisha utawala wa sheria kama msingi wa demokrasia ya kweli nchini.