Dau la atakayemuona Mdude lafikia Sh15 milioni

Muktasari:
- Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, kutangaza dau la Sh5 milioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa kada wa Chadema, Mdude Nyagali, sasa chama hicho nacho kimeongeza msukumo wa jitihada hizo kwa kutangaza dau la Sh10 milioni kwa atakayetoa taarifa sahihi kuhusu mahali alipo mwanaharakati huyo.
Mbeya. Hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza dau la Sh10 milioni kwa atakayetoa taarifa za kupatikana kwa kada wao, Mdude Nyagali, inakuja kufuatia jitihada zinazoendelea tangu Mei 2, 2025, alipovamiwa na kushambuliwa nyumbani kwake na watu waliodaiwa kuwa ni askari polisi.
Dau hilo la Sh10 milioni linaongezea na lile lililotangazwa awali na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, la Sh5 milioni, hatua inayoashiria uzito wa tukio hilo kwa pande zote mbili – Serikali na chama cha upinzani.
Tukio hilo lilitokea usiku katika eneo la Iwambi jijini Mbeya, ambapo Nyagali alichukuliwa kwa nguvu na hadi sasa hajulikani alipo.

Wafuasi wa Chadema wakiwa wamebeba mabango yenye picha ya kada Mdude Nyagali ya kutangaza dau ya Sh10 milioni. Picha na Hawa Mathias.
Sakata hili limeingia katika sura mpya baada ya Chadema kupitia Katibu wake wa Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, kutangaza zawadi hiyo ya Sh10 milioni leo Mei 9, 2025, akiwa katika Ofisi za Chadema Kanda ya Nyasa.
Mbeyale amesema zawadi hiyo ni matokeo ya michango ya wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za haraka za kuhakikisha kupatikana kwa Mdude, akiwa hai au amepoteza maisha.
Mbeyale amedai kuwa Chadema inaamini Mdude anashikiliwa na Jeshi la Polisi, na wametaka jeshi hilo kutoa taarifa rasmi kuhusu alipo au hali yake kwa sasa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga aliwahi kunukuliwa na Mwananchi akisema nao wako kwenye jitihada za kumtafuta Mdude.
Mbeyale leo amesema chama hicho kinaendelea kuchapisha mabango yenye picha ya Mdude pamoja na maelezo ya zawadi na mawasiliano ya viongozi husika ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa.
Mabango ya Chadema yamepachapishwa picha ya Mdude yenye maneno ‘Donge nono la milioni 10.’ Chadema itatoa kiasi cha Shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa ndugu Mdude.” Pia wameweka mawasiliano yao kwenye mabango hayo.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale akionyesha bango lenye picha ya Mdude Nyagali la kutangaza dau la Sh10 milioni. Picha na Hawa Mathias
Katika hatua nyingine, Chadema imeanzisha kambi maalumu ya kufuatilia hatima ya kada huyo, huku wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiendelea kumiminika Mbeya kuonyesha mshikamano.
Mbeyale amesema kambi hiyo haina kikomo cha muda, bali itaendelea hadi Mdude apatikane.
Aidha, misaada ya vyakula na mahitaji muhimu kama mchele, maziwa, nyama na mahindi inaendelea kutolewa na wananchi walioguswa na tukio hilo.
Chama hicho kimelaani kile kilichokiita ukimya wa Jeshi la Polisi na kimeendelea kusisitiza kuwa bado kipo katika kipindi kigumu kutokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa vyombo vya dola, hali inayozidi kuongeza sintofahamu juu ya hatima ya kada wao.