Prime
Chadema kuweka kambi Mbeya kushinikiza Mdude atafutwe

Muktasari:
- Ikiwa imetimia siku saba tangu Mdude achukuliwe na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi, wafuasi na viongozi wa Chadema takriban 500 wameamua kuweka kambi katika ofisi za Kanda mkoani Mbeya huku wakihusisha viongozi wa dini na asasi za kiraia, kwa lengo la kushinikiza polisi kuharakisha kumtafuta Mdude.
Mbeya. Ikiwa ni siku ya saba tangu kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mwanaharakati Mdude Nyagali, kuchukuliwa na watu wanaodaiwa kuwa ni polisi, wafuasi na viongozi wa chama hicho takriban 500 wameamua kuweka kambi katika ofisi za Kanda, wakisubiri tamko kutoka kwa viongozi wa kitaifa.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni kutokana na jitihada mbalimbali za kumsaka kada huyo katika mapori mbalimbali, hospitali, vituo vyote vya polisi nchini, na vyumba vya kuhifadhia maiti bila mafanikio.
Ikumbukwe kwamba Mdude Nyagali alitoweka nyumbani kwake eneo la Iwambi, jijini Mbeya, usiku wa kuamkia Mei 2, 2025, saa nane usiku, baada ya watu wasiojulikana kuvunja nyumba aliyokuwa akiishi, kumshambulia kwa kipigo na kisha kumchukua na kutoweka naye.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi, Mei 8, 2025, Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Hamad Mbeyale, amesema kuwa wameamua kuweka kambi katika ofisi za chama kwa lengo la kusubiri kauli ya Jeshi la Polisi, wakidai kuwa wana imani Mdude bado yuko mkoani Mbeya.
“Kambi hii itajumuisha wafuasi wa chama zaidi ya 500, si kutoka Tanzania pekee bali pia kutoka nchi jirani kama Kenya na Zambia.
“Pia, tunatarajia Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, Amani Golugwa, kuwasili wakati wowote kuanzia sasa kuungana nasi,” amesema Mbeyale.
Aidha, amesema ujio wa Golugwa unalenga kuungana na wafuasi wa Chadema pamoja na kutoa tamko rasmi kuhusiana na sakata la kutoweka kwa Mdude Nyagali.
Kuhusu ujio wa Golugwa, Mbeyale alisema: “Tuliwasiliana naye jana, na kama tayari ameanza safari, basi huenda akawasili mkoani hapa leo, Mei 8, 2025.
“Iwapo hatawasili leo, tunatarajia afike kesho, Mei 9, 2025, akiwa ameambatana na viongozi wengine wa chama kwa ajili ya kutoa tamko na kueleza msimamo wa Chadema kuhusu kutoweka kwa Mdude Nyagali.”

Mbeyale ameongeza kuwa kwa sasa, viongozi kutoka kanda mbalimbali pamoja na baadhi ya wafuasi kutoka mikoa tofauti tayari wameanza kuweka kambi rasmi katika ofisi za Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, huku wengine wakiendelea kuwasili.
“Bado tunaendelea kupokea wanachama na viongozi kutoka majimbo yote. Tutalala, kula, kuoga na kufanya shughuli nyingine hapa hapa hadi pale Jeshi la Polisi litakapotoa ushirikiano na kueleza rasmi Mdude Nyagali alipo,” amesema.
Akizungumzia kuhusu ufinyu wa ofisi za Kanda ikilinganishwa na idadi kubwa ya wafuasi wa Chadema wanaokusanyika, Mbeyale amejibu: “Kama ofisi itajaa, basi hata nje wafuasi na viongozi wa chama watalala. Lengo letu ni kujua hatma ya mwenzetu, awepo hai au amekufa,” amesema.
Kuhusu maeneo waliyomtafuta
Amesema kuwa wamefanya juhudi za kumsaka katika mapori yote hatarishi, hususan katika eneo la Inyala, Mlima Nyoka, Imezu, Mbalizi, na Songwe mpakani, na pia sehemu za maporomoko, kwa kushirikiana na wageni kutoka maeneo ya Kenya na Zambia.
"Baada ya kumsaka bila mafanikio, tumeona ni vyema kuweka kituo cha muda katika ofisi za Kanda hadi tutakapojua hatima ya mwenzetu, kama yupo hai au laa," amesema.
Viongozi wa dini, asasi za kiraia wahusishwa
Mei 5, 2025 viongozi wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Frank Mwakajoka walikutana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera kikao ambacho kiliisha kwa amani.
Hata hivyo, Dk Homera ametangaza kutoa Sh5 milioni kwa mwananchi yeyote atakayefanikisha kumpata kada huyo, huku akieleza kuwa tayari amemuelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Benjamini Kuzaga kuongeza juhudi kumsaka alipo.

Pia, amesema kwa kuwa mamlaka za juu tayari wametoa maelekezo, yeye kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo, anaungana nao kuhakikisha Mtanzania huyo anapatikana.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale amesema leo kuwa bado hawajatulia kwa kuwa matarajio yao ni kukutana na asasi za kiraia na viongozi wa dini juu ya tukio hilo.
Amesema suala hilo si la Chadema pekee bali jamii nzima ndio maana wameamua kupita makanisani kutangaza na kupata maombi na baraka za watumishi wa Mungu kupatikana kwa kada huyo.
“Matumaini yetu ni kwamba Mdude yupo hai, alishikiliwa na Polisi na tunahisi bado wanaye akiwa hai, tutakutana na viongozi wa dini, asasi za kiraia ili kuliweka wazi jamii ijue.
“Tumeomba kukutana na mchungaji Mbarikiwe, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Gervas Nyaisango na viongozi wengine ambao tumeomba kufika kanisani kwao,” amesema Mbeyale.
Katibu huyo ameongeza kuwa tayari viongozi wa chama hicho mkoani humo wamejigawa makundi mbalimbali kwa lengo la kuwafikia walengwa wote kuhakikisha wanapata haki ya mwenzao.

“Kupitia hili wataweza kuliombea hata Taifa kuondokana na janga hili, tumegawana maeneo lengo ni kuona mwanaharakati huyu anapatikana,” amesema Mbeyale.