Wanachama 50 wa ACT Wazalendo watimkia ADC

Muktasari:
Viongozi waliohamia ADC wakiwa na wanachama wao ni aliyekuwa Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Nyamagana, James Dioniz, Katibu wa Kata ya Mkuyuni jijini Mwanza, Mayala Dai na Katibu wa Vijana Kata ya Kishiri, Boaz Moi.
Mwanza. Zaidi ya wanachama 50 wakiwemo viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo mkoani Mwanza wamehamia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Viongozi waliohamia ADC wakiwa na wanachama wao ni aliyekuwa Katibu wa ACT Wazalendo Jimbo la Nyamagana, James Dioniz, Katibu wa Kata ya Mkuyuni jijini Mwanza, Mayala Dai na Katibu wa Vijana Kata ya Kishiri, Boaz Moi.
Akizungumza leo Jumapili Septemba 24, 2023 baada ya kukabidhiwa kadi ya ADC, Dioniz amesema uamuzi huo haujashinikizwa na mtu yeyote badala yake amevutiwa na Sera za ADC ambazo amedai zinaenda kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
"Nimefanya maamuzi baada ya kusoma Sera ya ADC kina malengo ya kumkomboa mtanzania. Niwaombe watanzania wengine kutoka vyama vingine kujiunga na chama hiki tuendeleze gurudumu la mapambano ya kuikomboa nchi kutoka kwenye mikono ya CCM,"
"Nimeshuhudia harakati zao kwenye chaguzi mbalimbali nchini hasa chaguzi za marudio kimeonyesha nia na ushupavu wa juu na ndicho kimekuwa chama kiongozi katika nchi hii. Hivyo niwaombe wanachama wengine kujiunga na chama hiki," amesema Dioniz
Kauli ya Dioniz, haitofautiani na Mayala Dai ambeye amesema amechukua uamuzi wa kuikacha ACT Wazalendo baada ya kuvutiwa na namna ADC inavyojiendesha nchini.
"Tumeshuhudia katika uchaguzi wa marudio ambapo chama hiki kimepambana kushindana na CCM, tunaamini ndicho chama kitakacholeta upinzani dhidi ya chama tawala (CCM) katika uchaguzi ujao," amesema
Mwanachama mwingine mpya kutoka Kata ya Mkuyuni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Mariam Bakari ameahidi kujituma kutafuta wanachama wapya kwa ajili ya kuwaunganisha na ADC.
Makamu Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaaban Itutu akizungumza baada ya kuwakabidhi wanachama wapya kadi zao za uanachama amewataka kukitumikia kwa nidhamu na weledi wa hali ya juu huku akiwakaribisha wanachama wengine ambao hawaoni uelekeo mzuri katika vyama vyao.
"Sisi tunawakaribisha wanachama kutoka vyama vyote iwe ACT Wazalendo, CCM, Chadema na vingine, kama mnaona mlipo hamtendewi haki njooni ADC hamtatawaliwa bali mtaongozwa. Niwaombe wanachama wapya kupambana kuvuta wanachama wengine wapya," amesema
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mashiku amesema James Dioniz alikuwa amesimamishwa uongozi ndani ya chama hicho kutokana na utovu wa nidhamu aliyouonesha kwenye maadhimisho ya Siku ya ACT Wazalendo yaliyofanyika jijini Mwanza.
Kuhusu wanachama wengine, Mashiku amesema anaamini ACT Wazalendo ni chama chenye ukomavu hivyo kuondoka kwa wanachama hao hakutoteteresha chama hicho badala yake kitaendelea kuvuna wanachama kutoka vyama vingine.
"Aliondoka kama yeye (Dioniz) na kikao halali cha Kamati ya Uongozi ya Jimbo kiliazimia kwamba kutokana na utovu wa nidhamu ambao alionesha kwenye maadhimisho ya siku ACT Day ndiyo yaliyopelekea asimamishwe uongozi,
"Kwa hiyo hasira za kusimamishwa uongozi ndiyo zilizopelekea ahame na wanachama. Tunatambua kila binadamu huwa ana mchango katika sehemu yake lakini nafasi yake imeshajazwa, haijaathiri na wanachama wapo na kazi inaendelea," amesema Mashiku