Vyama tisa vya siasa nchini vyabainika kuwa na dosari

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesebu za serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma. Wanaomsikiliza ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Halima Mdee (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka. Picha na Merciful Munuo
Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini dosari katika uendeshaji wa vyama vya siasa nchini huku vyama tisa vikibainika kushindwa kukusanya mapato yake na kuishia kukusanya asilimia 67 tu.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimebainika kununua vitu ambavyo havitumiki na vimepitwa na wakati vya Jumla ya Sh58.60 milioni.
Katika ripoti yake, CAG pia ameigusa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini kwa kushindwa kukiwajibisha chama hata kimoja cha siasa kilichobainika kutowasilisha rejista ya wanachama kama sheria inavyotaka.
Dosari hizo zimo ndani ya ripoti ya CAG, Charles Kichere aliyoiwasilisha bungeni jana ikiwa ni siku chache baada ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
CAG ameeleza kuwa alipitia bajeti ya vyama vya siasa mbalimbali pamoja na taratibu zilizotumika katika kuandaa na kujumuisha bajeti hizo katika kusaidia utekelezaji wa shughuli za kisiasa za vyama.
Hata hivyo, katika ukaguzi wake alibaini kuwa vyama tisa ambavyo ni CCM, CUF, ADC, Chaumma, Demokrasia Makini, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP na Chadema vilishindwa kukusanya mapato ya Sh25.85 bilioni katika mwaka 2021/2022.
Vyama hivyo vilikuwa vimejiwekea malengo ya kukusanya mapato ya Sh78.75 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/22 lakini hata hivyo, vilikusanya Sh52.90 bilioni tu ambayo ni sawa na asilimia 67 ya mapato yaliyobajetiwa.
CAG katika ukaguzi huo alibaini kuwa vyama vinne vya siasa vya ADC, NCCR-Mageuzi, SAU na TLP vilikusanya chini ya asilimia 10 ya mapato yaliyobajetiwa, akisema hali hii inaonyesha tatizo kubwa linalohitaji kushughulikiwa.
CAG alisema sababu za kushindwa kulipa ada zao za uanachama za kila mwezi kutokana na rejista za uanachama kutokuwa na taarifa sahihi za wanachama na kulikuwa hakuna utaratibu wowote wa ufuatiliaji.
Kulingana na CAG, kushindwa kukusanya mapato yaliyobajetiwa kuna athari kubwa kwa vyama, kwani kunazuia vyama vingi vya siasa kutotekeleza shughuli zao zilizopangwa na kufikia malengo yao ya kisiasa.
“Napendekeza Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa kuhuisha kanzidata zao za wanachama na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia ada ambazo hazijalipwa,” alisema CAG katika taarifa yake na kuongeza kuwa:-
“Hii itawezesha ufuatiliaji madhubuti wa ada ambazo hazijalipwa na kuboresha ukusanyaji wa mapato, hivyo kuongeza utekelezaji wa shughuli na mipango mbalimbali ya vyama,” anasisitiza CAG.
CCM na vitu havitumiki
Katika ripoti hiyo, CAG amebaini kuwa CCM kilinunua vitu ambavyo havitumiki na vimepitwa na wakati vya Sh58.60 milioni.
Katika ukaguzi wa vitabu vya ghala la CCM, ilibainika kati ya mwaka wa fedha 2019/20 na 2021/22, chama hicho kilinunua vitu mbalimbali vyenye gharama ya Sh58.60 milioni ambavyo havitumiki kwa sababu ya kupitwa na wakati.
“Kutokana na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia, vitu hivyo havitumiki na vimepitwa na muda. Menejimenti ya CCM ilieleza kuwa vitu hivyo ni nyeti hivyo inasubiri kibali kutoka katika bodi ili iviharibu,” anasema.
Kwa mujibu wa CAG, inasubiri kibali hicho kutoka kwa bodi ya wadhamini ili kuviharibu badala ya kuviuza na hivyo CCM ilisema inalenga kuhakikisha vitu hivyo visije kutumiwa vibaya na watu wasiofaa na kusababisha madhara kwa chama.
Kuhusu rejista ya wanachama, CAG alisema kwa mujibu wa kifungu cha 8C (1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 (iliyorejewa 2019), vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa vinatakiwa kutunza daftari (rejista) ya viongozi na wanachama wake katika kila ngazi.
Pamoja na matakwa hayo, katika mapitio yaliyofanywa na CAG alibaini kuwa vyama vya siasa vitano ADA-TADEA, DP, NRA, UMD na UPDP vilishindwa kuhuisha rejista za viongozi na wanachama wao.
Aidha, tathmini yangu ilibaini kuwa vyama vya UMD na UPDP vilishindwa kuhuisha rejista zao kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo yaani mwaka wa fedha 2020/21 na mwaka wa fedha 2021/22.
Hii ilisababisha ongezeko la idadi ya vyama vya siasa visivyofuata sheria kutoka vyama vinne hadi vyama vitano nah ii inaonyesha haja ya vyama vya siasa kuweka kipaumbele katika uzingatiaji wa Sheria na utendaji kazi wenye uwazi.
PIA CAG katika ukaguzi alibaini kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hajawahi kuviwajibisha vyama vya siasa ambavyo havijawasilisha rejista zao au taarifa zozote zinazohusiana na wanachama kulingana na matakwa ya sheria.
Kutokuwepo kwa uwajibishaji huu, pamoja na baadhi ya vyama vya siasa kushindwa kuhuisha rejista zao,kumesababisha kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi kuhusu idadi ya wanachama.
Ili kuboresha usahihi na upatikanaji wa taarifa za wanachama na viongozi wa vyama vya siasa, CAG amependekeza vyama vyote vya siasa vihuishe rejista zao kwa kuandaa kanzidata ya kielektroniki.