Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliofeli darasa la saba wanaenda wapi?

Sharif Hamad (katikati) mwenye umri wa miaka 14, miongoni mwa wanafunzi waliofeli darasa la saba mwaka 2022 na sasa ni mtoto anayefanya kazi mtaani, eneo la Ubungo mataa. akiwa na rafiki zake katika eneo hilo. Picha na George Helahela

Muktasari:

  • Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa amesema kwa sasa hakuna mfumo rasmi wa kuendelea na wanafunzi waliofeli darasa la saba, zaidi ya masomo ya ufundi stadi.

Dar es Salaam. Zaidi ya wahitimu 600,000 wameshindwa kuendelea na elimu ya sekondari katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hii ni sawa na wastani wa wahitimu 245,888 wanaoshindwa kuendelea na elimu ya sekondari baada ya kuhitimu darasa la saba kila mwaka, kuanzia 2021 hadi 2023.

Wanafunzi hao ambao aghalabu ni watoto chini ya miaka 14, hushindwa kujiunga na elimu ya sekondari kutokana na kutofikisha wastani uliopangwa ambao ni wa angalau daraja A hadi C.

Takwimu za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) zinaonyesha mwaka 2021 wanafunzi 199,658 walishindwa kuendelea na elimu ya sekondari, huku mwaka 2022 wanafunzi 274,671 hawakuendelea na elimu ya sekondari.

Vilevile, Novemba 23, 2023 baraza lilitangaza matokeo ya waliofaulu mtihani wa Taifa darasa la saba, huku wanafunzi 263,336 wakifeli hivyo kushindwa kuchaguliwa kujiunga shule za sekondari za umma.

Loading...

Loading...

Kwa mujibu wa baraza, wanafunzi wa darasa la saba hufanya mitihani sita ambayo ni ya  uraia na maadili, maarifa ya jamii, Kiingereza, Kiswahili, sayansi na teknolojia na hisabati.

Ufaulu wa wastani A hadi C ni kuanzia jumla ya alama 121 hadi 300, huku daraja D na E ambao huhesabiwa wamefeli ni wale walipata jumla ya alama 0 hadi 120 kwenye masomo hayo sita.

Takwimu hizi zinalandana na hali ilivyo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambako baadhi ya watoto waishio mtaani, wanaosema ni wahitimu wa darasa la saba na baada ya kufeli wamejikuta wanatafuta fedha katika mitaa ya jiji hilo la kibiashara.

“Ninakaa na bibi kule Tandale, asubuhi nakuja hapa kuomba ninachopata nakula na kingine nampelekea bibi nyumbani,” amesema Sharif Hamad (si jina halisi) mtoto wa miaka 14 aliyefeli darasa la saba mwaka 2022 aliyekutwa na mwandishi eneo la Ubungo mataa pamoja na watoto wengine.

Simulizi ya Sharif inashabihiana na ya Joseph Zacharia (si jina halisi), mwenye miaka 16 ambaye ni mfanyabiashara wa vifungashio kando mwa soko la Karume jijini hapa, anayesema amesafiri kutoka Kigoma kutafuta maisha baada ya kufeli darasa la saba.

“Kwetu ni Kigoma, hapa nimekuja baada ya matokeo ya darasa la saba mwaka juzi (2021) kutokuwa mazuri. Hapa nauza mifuko, natembea sehemu mbalimbali kuiuza,” amesema na kuongeza:

“Baada ya kufeli darasa la saba kaka yangu alinichukua na kunileta huku (Dar es Salaam) ili nimsaidie kwenye biashara,”amesema.

Licha ya kuwapo kwa wimbi la wahitimu waliofeli darasa la saba, bado hakuna mfumo rasmi wa elimu kwa kundi hili.

Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa amesema kwa sasa hakuna mfumo rasmi wa kuendelea na wanafunzi waliofeli darasa la saba, zaidi ya masomo ya ufundi stadi.

“Kwa sasa hatuna mafunzo labda tutafute njia mbadala, lakini kuna njia nyingi kwa waliopata chini ya alama hizo (A hadi C) ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini,” amesema.

Loading...

Loading...

Wakati Dk Mtahabwa akiitaja elimu ya ufundi stadi kuwa suluhu ya tatizo hilo. Hotuba za  bajeti za Wizara ya Elimu za mwaka wa fedha 2022/23 na 2023/24 zinaonyesha takwimu za udahili katika masomo ya elimu ya ufundi umepungua mara mbili zaidi.

“Jumla ya wanafunzi 123,352 walidahiliwa mwaka 2023/24 ikilinganishwa na wanafunzi 266,236 waliodahiliwa mwaka 2022/23,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.

Katika hotuba ya wizara hiyo ya mwaka 2023/24 iliyosomwa bungeni Mei 2023 na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda imesema Serikali imeongeza vyuo vya masomo ya ufundi stadi ili kuongeza fursa za mafunzo.

“Serikali imesajili vyuo 127 katika kozi za masomo zifuatazo: Afya na sayansi shirikishi (vyuo vitatu), biashara, utalii na mipango (vyuo vinne), Sayansi na teknolojia shirikishi (chuo kimoja) na vyuo vya ufundi stadi -Veta (119).

“Kuongezeka kwa usajili wa vyuo hivyo kumefanya jumla ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuwa 1,329 (Vyuo vya Elimu ya Ufundi -TET (465), vyuo vya ufundi stadi - Veta (809) na vyuo vya maendeleo ya wananchi - FDC (55),” alisema Profesa Mkenda akisoma bajeti hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), sifa za kujiunga na mafunzo hayo ni pamoja na:

“Mwombaji lazima awe amemaliza elimu ya msingi, sekondari na kuendelea pia mwombaji anatakiwa kufanya mtihani wa kujiunga (Aptitude Tests)” imeandika.

Mwalimu na mdau wa elimu, Doris Muchunguzi ameshauri ili kumaliza changamoto ya wanafunzi kubaki nyumbani kwa kigezo cha kufeli, kuwe na mtihani wa upimaji darasa la sita ili wenye ufaulu mdogo wapelekwe mchepuo wa ufundi.

“Kabla ya kuhitimu darasa la saba njia nzuri ni kuwapa mtihani wa kitaifa wa kuwapima ili wale wenye wastani mzuri waendelee na ngazi inayofauta, huku wanaoonekana kuwa na uwezo mdogo zaidi wapelekwe katika mchepuo wa ufundi.

“Kwa waliofeli miaka ya nyuma wasibaki bila kujulikana walipo, Serikali iwe na kanzidata ya kujua walipo na iwapagie vyuo vya ufundi hasa fani wanazozipenda wenyewe,” ameshauri.

Mdau wa elimu, Suzan Lyimo amesema huenda sera mpya ya elimu ikawa mwarobaini wa tatizo hilo miaka ya mbeleni.

“Tatizo hili si la hivi karibuni tu, hadi zamani lilikuwapo ndiyo maana tunashauri sera mpya ya elimu,  iwape wanafunzi nafasi ya kufika hadi kidato cha nne ndiyo iwe elimu msingi,” amesema.

Amesema sera mpya ya Wizara ya Elimu itasaidia kupunguza tatizo hilo. Hata hivyo, ameonyesha wasiwasi wa kukosekana vyuo vya ufundi vya kutosha kwa wanafunzi watakaosoma elimu ya amali.

“Tunatarajia Sera ya Elimu ya mwaka 2023 itatatua tatizo hili hadi kufikia mwaka 2027 kwa sababu hakuna watakaosalia nyumbani kwa kufeli,” amesema.

Loading...

Loading...

Kuhusu suala la muundo wa elimu msingi, Sera ya Elimu ya mwaka 2023 inasema itakuwa miaka 10 badala ya miaka saba iliyo sasa, ambapo mwanafunzi atasoma elimu ya msingi kwa miaka sita na sekondari miaka minne.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maarifa ni Ufunguo, Nicodemus Shauri, ameshauri jamii kuwekeza kwenye vipaji, fani na kazi za mikono ili kuondoa tatizo la wanafunzi wanaofeli kushindwa kuendelea na mfumo wa elimu, kisha kujiunga na makundi rika.

“Hii ni changamoto ya jamii nzima, ili tuiondoe tuwekeze katika vitu vingine pia nje ya elimu kama vile ufugaji, kilimo na fani za watoto wetu ili hata pale inapotokea anafeli darasani bado anakuwa na uwezo wa kuleta tija na kuepuka makundi mabaya,” amesema.

Akilizungumzia hilo, mwanasaikolojia, Naima Omari amesema wanafunzi wanaofeli masomo wengi wanaangukia kuwa watoto wa mtaani kutokana na kukosa usimamizi mzuri na matatizo ya kifamilia.

“Tukijiuliza watoto wanaofeli shule ya msingi na sekondari wapo wapi, katika maeneo ya mjini jibu ni rahisi wengi wanafanya  kazi mtaani kutokana na kukosa usimamizi wa wazazi au walezi, na wakati mwingine migogoro ndani ya familia inachangia,” amesema na kuongeza:

“Kwa upande wa vijijini wachache wanajishughulisha na kilimo lakini pia wapo wanaokimbilia mijini, ambao wengi pia katika kundi hilo wanaishia kuwa watoto wa mtaani,”amesema Naima.


Wadau wa elimu wasemavyo mitandaoni