Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyakazi wa nyumbani wakanywa vitendo viovu

Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla, akizungumza katika mafunzo ya afya na usalama kazini kwa wafanyakazi wa majumbani kutoka mikoa mbalimbali nchini, yaliyofanyika leo Aprili 29, 2025 mkoani Singida, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yatakayofanyika Kitaifa mkoani hapa, Mei Mosi, 2025. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Singida, wafanyakazi wa nyumbani nchini wametakiwa kuwa waaminifu wasitende vitendo viovu ili wajijengee uaminifu.

Singida. Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, Serikali imewataka wafanyakazi wa nyumbani nchini kutokutenda vitendo viovu vinavyosababisha kundi zima kuchukuliwa na jamii kuwa ni kundi la hatari au kuwadharau na kusababisha kuathiri hadhi ya kazi zao.

Aidha imeahidi kuendelea kulinda kundi hilo la wafanyakazi wa nyumbani wapate haki sawa na wafanyakazi wengine.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 29, 2025 na Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla akifungua mafunzo ya afya na usalama kazini kwa wafanyakazi wa majumbani kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na Chodawu.

Mkurugenzi huyo amesema ni muhimu wafanyakazi hao wa majumbani kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi ikiwemo kutokutenda vitendo viovu vinavyosababisha waonekane ni kundi baya au sehemu ya jamii kuwadharau.

“Tunasikia matukio ya baadhi ya wafanyakazi wa majumbani wasio waaminifu, msisahau kuwa mwajiri anayo haki ya kukushtaki, usifanye vitendo vitakavyokufanya ukashtakiwa na kuja kuifanya jamii kuwachukuliwa nyie ni watu hatari au kuwadharau.

“Muwe mfano wa kuigwa kwa kuheshimu wajibu wenu msifanye matukio yatakayopelekea kundi zima kuonekana ni watu hatari, tekelezeni wajibu wenu vizuri.Msifanye matukio yanayoathiri hadhi ya kazi zenu,mfanye kazi kwa kuzingatia maadili,”amesema.

Kuhusu ubaguzi amesema Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini inalinda wafanyakazi wote na kuwa kifungu cha 7 cha sheria hiyo kinakataza ubaguzi wa aina yoyote mahala pa kazi hivyo waajiri wakiwemo walioajiri wafanyakazi wa majumbani.

“Ndani ya Sheria hakuna ubaguzi unaotenga kundi fulani, nitoe agizo kwa waajiri wote nchini wanaoajiri wafanyakazi wa majumbani, hawapaswi kuwabagua na wajue wana haki sawa na wafanyakazi wengine ikiwemo wa maofisini,” amesema.

Mmoja wa wafanyakazi wa majumbani kutoka Dar es Salaam, Sedi Michael, amesema ni muhimu kundi hilo kufanya kazi zao kwa kuzingatia uaminifu ili waweze kutendewa haki na kupata stahiki zao.

“Sisi tukiwa waaminifu tutafanya kazi katika mazingira rafiki, natoa rai kwa wenzangu wanaoachwa na waajiri wao majumbani, wasitoroke, kuiba watoto wa waajiri wao au kuwafanyia vitendo vya kikatili.

“Tuheshimu kazi zetu kwani ndiyo zinatupatia kipato, uaminifu ni silaha ambayo inaweza kukulinda mwenyewe sehemu ya kazi. Mimi nimefanya kazi zaidi ya miaka 10, mwajiri wangu wa sasa amenipa nyumba ya kuishi, silipi kodi na ananilipa mshahara kama kawaida.

“Kupitia kazi hii ambayo watu wanaidharau mimi kwanza nimeweza kupewa mafunzo ya Veta, nimepata mafunzo mbalimbali ya kutengeenza keki kwa sasa nafanya kazi mbalimbali ikiwemo kutengeneza keki na vitafunwa ni biashara inaniendeleza kiuchumi,” amesema.

Naye Desderia Simon kutoka Morogoro, amesema kupitia mafunzo mbalimbali ya vyama vya wafanyakazi wametambua haki zao pamoja na wajibu wao ikiwemo kutambua ni makosa kupelekwa sehemu moja kwa ajili ya kazi na kutoroshwa kwenda kufanya kazi sehemu nyingine.

“Mafunzo kama haya yametusaidia kutimiza majukumu yetu bila kukiuka kanuni, sheria wala katiba. Nikitolea mfano suala la kutolewa mkoa mmoja kupelekwa mkoa mwingine kwa ajili ya kufanya kazi, najua ni makosa kutoroka kwa mwajiri wangu na kupelekwa kufanya kazi sehemu nyingine, wengi wana hiyo tabia kwa sababu hawajui athari zake,” amesema.

Mkurugenzi wa ILO, Ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline Mugala, amesema nchi za Jumuiya hiyo ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ziko kwenye hatua za mwisho kuridhia na kusaini mkataba namba 189 wa Kazi zenye Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani.

Amesema wamekuwa wakisaidia baadhi ya nchi hizo kuingia mikataba na nchi za nje zinazopokea wafanyakazi wa majumbani ili kuhakikisha wanaenda kwenye nchi hizo kwa njia halali na kufuata taratibu pamoja na kulinda haki zao.

“Ni lazima tutambue mchango wa wafanyakazi wa majumbani kwa ukuaji wa uchumi na ukuaji wa wanaowafanyia kazi, mimi binafsi hii kazi ninayofanya siwezi kuifanya bila msaada wa mfanyakazi wangu wa nyumbani.

“Ninasafiri sana naweza kumaliza mwezi siko nyumbani ila nyumba naiacha na uangalizi wa mfanyakazi wangu wa nyumbani ni muhimu tuwalinde, tuheshimu utu wao, mazingira ya kufanyia kazi yawe salama,” amesema.

Mkurugenzi huyo amewataka wafanyakazi hao wa majumbani kuhakikisha wanapokuwa na changamoto katika maeneo yao ya kazi, wanawasiliana na vyama vyao ili waweze kupata msaada.

Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Rehema Ludanga, amesema wanashirikiana na wadau wengine kuhakikisha mkataba huo namba 189 unaridhiwa na kuwa wataendelea kushirikiana nao kuhakikisha kila mfanyakazi hata ambaye siyo wa majumbani anapata haki yake.

“Sisi hatubagui tunawathamini na kuwatambua wafanyakazi wa majumbani ndiyo maana wamewekewa vipengele vyao vya mishahara kwa saa, siku na mwezi kila mmoja amekadiriwa kulingana na hali halisi ya eneo la kazi analofanya,” amesema.

“Niwasihi mnaopata mafunzo haya muwe mabalozi wazuri na elimu hii iwasaidie kufanya shughuli zenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Dunia pia inabadilika lazima na sisi tubadilike, tusije kubaki nyuma,”amesema naibu katibu mkuu huyo.