Mkataba wa wafanyakazi majumbani, mwarobaini haki zao

Mwanasheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhini, Mahotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Wagala Shungu, akizungumza katika mafunzo ya Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004, kwa wafanyakazi wa Majumbani kutoka mikoa nane nchini, leo Alhamisi Machi 6, 2025 jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa yatafanyika Machi 8,2025 jijini Arusha,Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani nchini,kimeiomba Serikali kuridhia na kupitisha Mkataba namba 189 unaohusu staha za wafanyakazi majumbani ili kuwasaidia kupata haki zao za msingi.
Arusha. Kuridhiwa na kupitishwa kwa mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 189 wa Kazi zenye staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani , unaohusu staha za wafanyakazi majumbani,unatajwa kuwa mwarobaini wa upatikanaji haki za msingi za wafanyakazi wa majumbani ikiwemo kutambua haki,stahiki zao pamoja na sheria za haki,kazi na wajibu.
Aidha Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani nchini,kimelaani viteno vya unyanyasaji na ukatili wanavyokumbana navyo wafanyakazi hao wakiwa kazini,wakitolea mfano tukio la mfanyakazi wa majumbani aliyejulikana kwa jina la Hadija,aliyefariki dunia hivi karibuni mkoani Arusha,akidaiwa kubakwa kisha kuuawa.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Machi 6, 2025 kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani Tanzania, Zanini Athumani,akizungumza katika katika mafunzo kwa wanahabari kuhusu umuhimu wa mkataba huo namba 189 pamoja na mafunzo kuhusu Sheria Ajira na Mahusiano kazini yam waka 2004 kwa wafanyakazi wa majumbani.
Amesema kuwa wafanyakazi wa majumbani ni watu wenye mchango mkubwa kwa taifa kwa sababu ni watu wanaoachwa na waajiri wao majumbani ila baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwanyima haki zao za msingi na kuwa mkataba huo ukiendana na Sheria za kazi utasaidia kuweka mazingira salama.
“Kutokana na hali ya uchumi kwa sasa familia nyingi baba ni mfanyakazi,mama ni mfanyakazi hivyo mfanyakazi wa nyumbani ana jukumu kubwa la kulea watoto,tunaomba Serikali iridhie mkataba huo kwani tunauona utakuwa mkombozi wa wafanyakazi wa majumbani,”
“Baadhi ya waajiri wamekuwa wakiwanyanyasa wafanyakazi wa majumbani wamekuwa wakiwapikisha lakini hawala,waajiri ni watumishi wana mikataba ya ajira wanaenda likizo za uzazi ila mfanyakazi wa nyumbani akipata ujauzito imekuwa changamoto inakua ukomo wa ajira,akiumwa anaachishwa kazi ghafla,akiumwa anaachishwa kazi badala ya kupewa likizo,”amesema
Kuhusu vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia wanavyokumbana navyo,ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kutokomeza vitendo hivyo ikiwemo kuwachukulia hatua kali za kisheria wale watakaothibitika kutenda matukio hayo.
“Tunashukuru Chodawu wamekuwa wakitoa elimu kwetu kwa muda mrefu sasa ambapo tumejua masuala mbalimbali kuhusu sheria za haki,kazi na wajibu wetu na imetusaidia walau kwa kiasi fulani kupata haki zetu kwa waajiri ambao wanajua na kuzingatia sheria, “ amesema
Awali Mwanasheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani,Hifadhini,Mahotelini,Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Wagala Shungu amesema mkataba huo kimekuwa kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi wa majumbani na kuwa sekta hiyo imekuwa ikisahaulika hivyo wao kwa kuwa wanajua mchango wao wameamua kuwasaidia ili wapate haki zao.
“Tunaona kuna matukio megi sana wanafanyiwa wafanyakazi wa majumbani yanayoshusha utu wao,hii sekta imekuwa ikionewa kwa muda mrefu wafanyakazi hawa hawachukuliwi kama wafanyakazi wengine,matukio mengi yamekuwa yakitokea kwenye kaya zetu wafanyakazi wa majumbani kufanyiwa vitendo vya utakili,tunaendelea kupambana wafanyakazi watambulike na wapate haki zote,”amesema
Mratibu wa mradi wa kukuza kazi zenye heshima,kazi na utu kwa wafanyakazi wa majumbani kutoka Shirika lisilokuwa la kiserikali la CVM,Ibrahim Tony amesema mradi huo ulioanza mwaka 2018 unatekelezwa katika mikoa nane umelenga kuchangia kuboresha maisha bora kwa wafanyakazi wa majumbanina pia kuhakikisha wanakuwa na mazingira salama.
Ametaja mikoa hiyo ni pamoja na Pwani,Morogoro,Dodoma,Ruvuma, Lindi,Dar Es Salaam na Zanzibarm na kuwa wamekuwa wakishirikiana na Chodawu ambapo wanawajenega uwezo kwa namna ya kufahamu sheria na taratibu za kazi na namna ya kuheshimu sehemu za kazi.
Amesema wameanza mtaala maalum wa mafunzo mbalimbali ambapo hadi sasa wameshawafikia wafanyakazi wa majumbani 600 katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) na wanatarajia hadi mwisho wa mwaka huu kufikia wafanyakazi wa majumbani zaidi ya 1,280 kutoka mikoa hiyo nane.
Naye Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Chodawu,Asteria Gerald,amesema lengo la mafunzo hay oni kuangalia masuala ya wafanyakazi wa majumbani kwani kumekuwa na vitendo vya kikatili wanavyokumbana navyo wafanyakazi hao.
Amesema mkataba huo umeeleza masuala ya haki za wafanyakazi kwa ujumla,mkataba wa ajira wa maandishi,afya na usalama,haki ya kushitaki,wafanyakazi wahamiaji,mawakala wa ajira na vyombo vya malalamiko.
“Sekta hii ni kama imesahaulika ila tunaamini Serikali ikiridhia mkataba ule itakuwa sehemu pekee ya wafanyakazi wa majumbani kupata haki zao,licha ya kuwa kuna sheria ila bado kuna matukio ya ukatili na kukosekana kwa haki nyingi za watumishi ili wawe salama sehemu zao za kazi,”amesema Mkuu huyo