Waajiri wakumbushwa kujiweka tayari mabadiliko ya teknolojia

Muktasari:
- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvukazi mahali pa kazi ili kukuza uchumi.
Dar es Salaam. Serikali imewakumbusha waajiri nchini kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari zake hasi zinazoweza kutokea ikiwemo upotevu wa baadhi ya fursa za ajira.
Wito huo umetolewa Aprili 28, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete wakati akiwaongoza mamia ya Watanzania kwenye maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani, iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Singida katika viwanja vya Mandewa.
Akihutubia katika kilele cha maadhimisho hayo, Ridhiwani amesema Serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi yake, hivyo imeendelea kuuwezesha Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan, anatambua na kujali afya na usalama wa wafanyakazi nchini na amethibitisha hilo kwa vitendo kupitia uwezeshaji ambao amekuwa akiufanya kwa OSHA, ikiwamo kuipatia vitendea kazi na kuwaongezea watumishi ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia Watanzania,” amesema.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu isemayo: “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi”, Ridhiwani amesema teknolojia ina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa utendaji.
"Ninawashauri waajiri nchini kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari hasi za teknolojia ikiwemo kupotea kwa baadhi ya fursa za ajira," amesema Ridhiwani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akiwaeleza wafanyakazi manufaa ya matumizi ya akili mnemba katika maeneo ya kazi katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mandewa, Mkoani Singida.
Waziri huyo amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa sera zinazowajumuisha wajasiriamali wadogo katika fursa mbalimbali za kiuchumi yakiwemo masuala ya usalama na afya kazini.
Hatua hiyo inatekelezwa na OSHA ambayo imeanzisha programu maalumu ijulikanayo ‘Afya Yangu, Mtaji Wangu’ ili kuyatambua makundi ya wajasiriamali wadogo na kuyawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi nchini.
Ameanisha shughuli ambazo ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na maonyesho ya usalama na afya mahali pa kazi, kliniki ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, shindano la tuzo za usalama na afya mahali pa kazi, bonanza la michezo pamoja na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO) Kanda ya Afrika Masharika, Caroline Khamati Mgalla ameipongeza Serikali ya Tanzania na wadau wa usalama na afya nchini, kwa maandalizi mazuri ambayo yamehusisha shughuli zenye tija kwa jamii zikiwemo huduma ya upimaji afya na matibabu kwa wananchi na mafunzo kwa wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba amewapongeza waajiri kwa mwitikio mzuri katika maadhimisho ya mwaka huu huku akiwashauri kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo akili unde ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya ametoa tahadhari kwa waajiri nchini kuhakikisha teknolojia mpya zinazotumika katika uzalishaji haziathiri ajira za Watanzania.
Aprili 28, 2025 kila mwaka hutambulika kimataifa kama Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo.
Lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi, pamoja na kuwakumbuka walioumia au kupoteza maisha wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa Maonesho hayo, Meneja wa Usalama wa GGML, Isack Senya amesema wamewekeza katika teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kutoa tahadhari ya maeneo hatarishi na kutumia vifaa vya kisasa kufanya ulipuaji salama.
Amesema pia mgodi huo umekuwa ukitumia mitambo mikubwa ya uchorongaji na kubeba mizigo isiyokuwa na msimamizi (operator) na vifaa vingine mbalimbali zikiwemo kamera na ndege zisitumia rubani (drone) zenye uwezo mkubwa wa kujiendesha wenyewe na kutoa tahadhari ya vitu vyote hatarishi.
Uwekezaji huu, kwa mujibu wake ni miongoni mwa vitu vinavyoufanya mgodi huu kuendelea kuwa kinara katika usalama mahala pa kazi ndani na nje ya nchi.
"Tunaangalia mustakabali wa usalama kwa mitazamo miwili, mifumo ya teknolojia ya kisasa na jumuiya salama, hivyo, ushiriki wetu katika maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya maeneo ya kazi (OSHA 2025) unaonyesha dhamira yetu ya kuongoza katika mambo haya yote mawili,” amesema Senya.
Amesema dijitali na akili Mnemba (AI) ni zana, lakini ni watu wanaoleta mabadiliko, hivyo ni lazima tuwe na mtazamo wa kuangazia usalama wa watu tunapotumia teknolojia hii.
“Na ndio maan GGML tunawekeza katika rasilimali watu pia kuhakikisha usalama unaendelea kuwa ajenda namba moja kuliko kitu chochote katika maeneo yetu ya kazi,” amesema.
Amesema kuwa malengo ya mgodi huo ni kufanya kazi ya uchimbaji dhahabu kwa usalama zaidi bila kuhatarisha maisha ya mtu.
Amesema GGML inajivunia kushikilia rekodi ya kuwa namba moja kwa usalama duniani katika kipindi cha miaka minne mfulululizo toka mwaka 2019 kwa sababu ya uwekezaji mkubwa wa teknolojia ya kisasa, ikiwemo matumizi ya mtambo wa kuzima moto ardhini kwa kutumia povu linalotokana na mbolea ili kulinda mazingira.
Neema Matindiko kutoka kitengo cha utafiti katika mgodi huo amesema katika maonesho ya mwaka huu wamekuja na vifaa mbalimbali vya teknolojia ya hali ya juu vinavyojiendesha vyenyewe vikiwa na uwezo wa kutambua hatari maeneo mbalimbali ikiwemo chini ya ardhi kunakochimbwa dhahabu na kutoa taarifa zote za maeneo hatarishi.
John Kishaluli, ambaye ni Mwalimu mstaafu anayependa kufuatilia mambo ya utafiti amesema amefurahi kuona teknolojia ya hali ya juu inayotumiwa na GGML katika kulinda usalama mahali pa kazi akisema uwekezaji huo unatija katika uzalishaji wa dhahabu kwa maendeleo ya taifa.
“Wenzetu katika mataifa mengine wanatumia teknolojia na kupata matokeo ya kisasa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utafiti,” amesema.
“Uwekezaji huu uliofanywa na GGML unainesha ni namna gani sekta ya madini inaweza kuwa mfano kwa sekta nyingine kutumia teknolojia kwa ajili ya maendeleo,” amesema Kishaluli.