Vipeperushi vyatangaza mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo, viongozi watua Dodoma

Muktasari:

  • Mei 15, 2023 kuliibuka mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo wakilalamikia kero, walizosema zinatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Dar es Salaam. Wakati vipeperushi vikisambaa kwenye mitandao ya kijamii vikieleza kuhusu mgomo wa wafanyabiasha Kariakoo kuanzia Jumatatu, Juni 24 2024, uongozi wao umewataka kuwa watulivu, ukisema tamko litatolewa siku hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Karikaoo, Martin Mbwana akizungumza na Mwananchi leo Juni 22, 2024 amekiri kuona vipeperushi hivyo, akieleza hiyo ni hasira za kuchoshwa na wanayofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, amewataka watulie akisema wapo jijini Dodoma kushughulikia suala hilo na kwamba, wamepanga kukutana na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba Jumatatu Juni 24.

Amesema wataungana Bodi ya Wafanyabiashara Karikoo na bodi ya uongozi wa wafanyabiashara ya Taifa.

“Yote yanayoendelea Karikaoo nimepata taarifa, nayajua na nimeyasikia, lakini kikubwa kwa sababu  viongozi tumewahi serikalini na tumepeleka taarifa, ningeomba wafanyabiashara wawe watulivu, mpaka Jumatatu saa 10.00 jioni tutakuwa tumeshatoka kwenye vikao tutawajulisha  nini kinaendelea,” amesema Mbwana.

Amesema anatambua wafanyabiashara wamechoka, wameumizwa lakini kila kitu ni mazungumzo na maridhiano.

Akieleza sababu ya kutaka kufanya mgomo, Mbwana amesema kumekuwa na mwendelezo wa kamatakamata licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzuia.

Akizungumza na wafanyabishara wa Kariakoo Mei 15, 2023 kutokana na mgomo walioutisha kutokana na kero mbalimbali wanazodai zinatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Majaliwa alisema hakuna mtumishi yeyote wa umma mwenye mamlaka ya kudharau maagizo yanayotolewa na viongozi wake.

Baadhi ya kero walizotaja wafanyabiashara hao ni kamatakamata ya TRA dhidi ya wafanyabiashara na wateja kutoka nchi jirani wanaofanya ununuzi katika soko hilo na ulazima wa kusajili maghala yanayohifadhi bidhaa kitu ambacho kimekuwa kero na kukosa majibu kwa viongozi waliofika sokoni hapo.

Mbwana amedai hivi sasa hali ya kamatakamata imerudi tena kwa kasi kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Sababu nyingine amesema ni baadhi ya wafanyabiashara kufutiwa madeni ambayo wamekuwa wakiidai Serikali ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), pia kufungiwa akaunti zao.

“Kwa hiyo kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimewatia hasira wafanyabiashara, ila yote kwa yote kwa usikivu wa Waziri wa Fedha na Kamati ya Bunge ya Bajeti, tunaamini mpaka Jumatatu tutakuwa tumeshapata majibu ya haya,” amesema.


Kauli ya TRA

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano kwa Mlipakodi wa TRA, Hudson Kamoga amesema: “Hatujapokea taarifa kuhusu malalamiko hayo yanahusu nini ili kuyashughulikia.”

Kamoga amesema kuna utaratibu wa kuwasilisha malalamiko ili kutatuliwa ambao haujafuatwa.

"Lakini kama kuna mtumishi wa TRA amekwenda kinyume cha maadili, kuna taratibu za kushughulikia hilo pia," amesema akisisitiza TRA inatimiza wajibu wake wa kodi kwa mujibu wa sheria, hivyo kila kilichofanyika kilisimamiwa na sheria iliyotungwa na Bunge.

Amesema tayari waziri alishawasilisha mapendekezo bungeni kuhusu mabadiliko ya kodi na tozo na hiki ndicho kipindi wawakilishi wa wafanyabiashara na wananchi (wabunge) watajadili iwapo kuna sheria ambazo haziendani na utaratibu, kufanyiwa marekebisho.


Mkuu wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogo, amekiri kuona kipeperushi na kueleza wanafuatilia.

“Tumejaribu kuulizia kwa  kwa baadhi ya wafanyabishara wakiwemo viongozi wao, hawana wanalojua kuhusu hilo,” amesema.

Mpogolo amewasihi   kuendelea kufanya biashara kama kawaida, amesema Serikali ni sikivu ndiyo maana Mei, 2023 Waziri Mkuu alikutana nao pamoja na mawaziri zaidi ya saba.

Mei 15, mwaka jana mgomo mkubwa ulifanyika Kariakoo uliodumu kwa siku tatu mfululizo hadi pale Majaliwa alipoingilia kati kwa kukutana na wafanyabiashara hao kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliambatana na mawaziri saba wa kisekta, wakiwamo Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba; Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji; Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na Kamishna wa TRA.

Waziri Mkuu Majaliwa alisikiliza kero za wafanyabiashara hao ambazo zingine alizitolea majibu.

Pia aliunda kamati ya kutatua mgogoro baina ya wafanyabiashara hao na Serikali iliyojumuisha wajumbe 14.