Yaliyojiri saa 72 za mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo

New Content Item (1)

Dar es Salaam. Zilikuwa ni saa 72 za hasara, mvutano, vurugu na kuwekana kikaangoni na sasa hali ya soko la Kariakoo imerejea kama zamani, huku watu wengi wakisubiri kuona nini kitafuata kwa yaliyoibuliwa.

Pia, wanasubiri timu ya watu 14 iliyoundwa itakuja na majibu gani.

Baada ya fununu na minong’ono mingi Jumatatu ya Mei 15, wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo lenye msongamano lililopo kilomita chache kutoka Bandari ya Dar es Salaam, walianza mgomo.

Siku hiyo karibu maduka yote yalifungwa, walikusanyika na kuanza kupaza sauti juu ya kero zao, huku wakitaka kuonana na Rais Samia Suluhu Hasssan, huku kukiwa hakuna msongamano.

Siku tatu mfululizo zilikuwa ni maumivu kwa wafanyabiashara wa soko hilo, wakiwamo wadogo wanaotoa huduma katika soko hilo, huku wanunuzi wa ndani na nje wakikosa mzigo na makusanyo ya Serikali ambayo ni wastani wa Sh472 milioni kwa siku yalikosekana.

Kutokana na mgomo uliotokea, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala aliwaelekeza viongozi wa wafanyabiashara hao kuwa wanatakiwa kwenda Dodoma kuonana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lakini waligoma wakisema yeye ndiye anapaswa kuwafuata hapo na kweli jioni alifika na kuwasikiliza.

Baadhi ya wachambuzi walisema kuwa mgomo huo ulitokana na uzembe wa baadhi ya viongozi kutochukua hatua za mapema kuzuia mgomo huo, licha ya kuwa na fununu, vilevile kulikuwa na wasiwasi wa mgomo huo kusambaa maeneo mengine ya nchi.

“Haikupaswa iwe hivi ilivyojitokeza, naweza kusema ni uzembe. Kariakoo ni eneo muhimu katika biashara na miamala ya kiwango kikubwa cha fedha inafanyika kwa siku,” alisema Mchambuzi wa uchumi, Gabriel Mwang’onda.

Kuhusu uwezekano wa mgomo huo kusambaa maeneo mengine, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano alisema kuna uwezekano mdogo wa kilichofanyika Kariakoo kufanyika maeneo mengine kwa kuwa hoja za wafanyabiashara zinaweza kufanana na maeneo mengine ya nchi.

“Mambo kama haya yanategemea viongozi wenyewe wa wafanyabiashara na namna walivyoshughulikia mambo na mrejesho waliokuwa wakiupata, kikubwa ili kuepuka mambo kama haya kuwe na usawa katika kodi,” alisema Dk Lutengano.

Alisema tathimini ya kina inapaswa kufanyika ili kuwa na kodi halisi, hata kama itaongezeka au kupungua kikubwa iwe na utaratibu mzuri wa kuipatia, “suluhu ya migogoro kama hiyo ni kuwa na muafaka wa pande zote.”


Kinacholalamikiwa

Wafanyabiashara hao walikuwa wakilia na kamata kamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), walipinga kuanzishwa kwa utaratibu mpya wa usajili wa stoo ambavyo vyote vilisimamishwa na Majaliwa, huku akiitaka ijipange kukadiria kodi ya forodha.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana alisema jambo hilo sio Kariakoo pekee, “hiki ni kilio cha nchi nzima, si Mbeya, Arusha, siyo Mwanza kila mfanyabiashara anakayeingia hapa lazima ashughulikiwe, halafu bila aibu wanasema wanaongoza kwa kukusanya kodi mkoa wa kikodi Kariakoo, ni kodi ya damu na maumivu.”

Hata hivyo, utaratibu huo ulioanzishwa na Serikali ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato unatokana na baadhi ya wafanyabiashara kutotoa risiti au kutoa risiti zenye thamani pungufu na uhalisia.

Siku ya kwanza ya mgomo wa wafanyabiashara hao, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo aliliambia Gazeti la Mwananchi kuwa Kariakoo ndiyo kitovu cha biashara, hivyo utoaji wa risiti pungufu au kutotoa kabisa ni kosa na hilo wamekuwa wakiwaambukiza wengine kufuata mfumo huo.

“Baadhi yao wamekuwa wakitoa na wengine hawatoi. Wengine wanatoa risiti wengine hawatoi, wengine wanatoa risiti kiasi pungufu tofauti na bei halisi, wengine risiti moja inasindikiza mizigo kutwa,” alisema.

Kayombo alisema jambo hilo limesababisha kuwepo kwa ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau na wateja na hadi kuandikwa katika vyombo vya habari.

“Hiki ndicho chanzo cha ukaguzi, ukaguzi huu si wa Kariakoo peke yake bali nchi nzima, ndiyo maana hata katika vituo vya ukaguzi, ikiwamo vilivyopo njia kuu tumekuwa tukifanya ukaguzi kuhakikisha risiti zimetolewa kikamilifu,” alisema Kayombo.

Aliongeza kuwa risiti za kielektroniki ndiyo njia sahihi ya utunzaji kumbukumbu ambayo inawezesha upatikanaji wa kodi sahihi isiyo ya kumuonea mtu wala kuipunja Serikali.


Sheria inasemaje

Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya 2022 Kifungu 45A chini ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi sura namba 338, wafanyabiashara wanatakiwa kusajili maeneo yao ya kazi kwa Kamishna Mkuu wa TRA na utaratibu huo ulianza kutumika Julai mosi 2022.

Pia, jambo lingine wanalopaswa kutekeleza wafanyabiashara hao, ni kupeleka taarifa za bidhaa zilizopo kwenye maeneo ya kuhifadhia kila mwezi kwa kamishna mkuu wa mamlaka hiyo.

Mbali na hayo, sheria hiyo inawaelekeza wafanyabiashara wote kutoa taarifa ya maeneo yao ya kuhifadhia bidhaa na kujaza taarifa sahihi za ritani ya bidhaa zilizopo kwenye maeneo ya kuhifadhia.


Kilichotokea

Awali, wafanyabiashara wa Kariakoo walikuwa wakilalamikia kamata kamata inayofanywa na TRA, walipinga kuanzishwa kwa utaratibu mpya wa usajili wa stoo ambavyo vyote tayari vilisimamishwa mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.

Hata hivyo, juzi wakati Waziri Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara kama alivyowaahidi siku ya kwanza ya mgomo wao, hoja zaidi ziliibuka na suala sasa likiwa ni la kitaifa kwa kuwa hata viongozi wa wafanyabiashara katika mikoa mingine walihudhuria.

Katika mkutano wa juzi, wafanyabiashara walitumia saa tano kuzungumza na Waziri Mkuu wakimweleza kero wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku.

Unaweza kusema, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Dk Ashatu Kijaji), Waziri wa Mambo ya Ndani (Hamad Masauni) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walikaangwa mbele ya bosi wao.

Rushwa kwa watumishi wa TRA, mfumo wa kodi ya bandarini kuangaliwa, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kupunguzwa na kuondolewa Sheria ya Usajili wa Stoo ni mongoni mwa hoja zilizotawala katika mkutano huo ambao kila mzungumzaji alizungumza kwa hisia.

Majaliwa alisema Serikali imechukua kero na malalamiko yote ya wafanyabiashara na kwenda kuyafanyia kazi, huku vyombo na taasisi, zikiwamo TRA na Jeshi la Polisi akitaka vijitathimini utendaji wake.