TRA yatia neno mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo

Dar es Salam. TRA yabainisha sababu za mgomo wa wafanyabiashara soko la Kariakoo kuwa unatokana na na ukaguzi uliofanywa na mamlaka hiyo na kubaini baadhi ya wafanyabiashara hawatoai risiti za kielektroniki kama inavyoelekezwakatika sheria za kodi.

Ufafanuzi huo umetolewa na TRA wakati wafanyabiashara hao wakiendelea na msimamo wa kutofungua maduka yao hadi pale watakapoonana na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye wamemtaja kama mtatuzi  wa changamoto wanayopata dhidi ya TRA.

Baadhi ya changamoto walizotaja wafanyabiashara hao, ni kukamatwa mara kwa mara na TRA kwa madai ya kuandika risiti isiyo na uhalisia kwa wateja pamoja na  kushinikizwa kutekeleza Sheria ya kusajili maghala ambayo itawalazimu kuwasilisha hesabu zao kwa mamlaka hiyo kila mwezi.

Licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Amos Makalla kufika asubuhi Kariakoo na kuzungumza nao kwa kuwaahidi kuwakutanisha na Waziri Mkuu Kassim, Majaliwa jijini Dodoma, wafanyabiashara hao waligoma wakishinikiza kuonana na Rais Samia.

Leo Mei 15, 2023 akizungumza kwa simu na Mwananchi Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi TRA Richard Kayombo ameeleza kiini cha mgomo huo kuwa ni kukosekana kwa uaminifu katika utoaji wa risiti za kielektroniki.

 "Baadhi yao wamekuwa wakitoa na wengine hawatoi. wengine wanatoa risiti kukiwa na kiasi pungufu tofauti na bei halisi, wengine risiti moja inasindikiza mizigo kutwa," amefafanua.

Kayombo amesema jambo hilo limesababisha kuwepo kwa ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau na wateja na hadi kuandikwa katika vyombo vya habari.

"Hiki ndicho chanzo cha ukaguzi, ukaguzi huu si wa Kariakoo peke yake bali nchi nzima, ndiyo maana hata katika vituo vya ukaguzi ikiwemo vilivyopo njia kuu tumekuwa tukifanya ukaguzi kuhakikisha risiti zimetolewa kikamilifu.

Kayombo amesema risiti za kielektroniki ndiyo njia sahihi ya utunzaji kumbukumbu ambayo inawezesha upatikanaji wa kodi sahihi isiyo ya kumuonea mtu wala kuipunja serikali

"Na hii imeanza tangu 2010 kwa walipa kodi wa Ongezeko la Thamani (VAT) na walipa kodi wasiokuwa na VAT ilianza mwaka 2014 na tumekuwa tukiendelea nalo na utaratibu ambao unafanyika wa nchi nzima," amesema.

Amesema Kariakoo ndiyo kitovu cha biashara hivyo utoaji wa risiti pungufu au kutotoa umekuwa ukisababisha wengine wanaokwenda kuuza kuiga mfumo huo.