Vijana Siha waomba kulima hifadhini

Kiongozi wa Bodaboda Wilaya ya Siha, akieleza changamoto zinazowakabili kwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi.Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Eneo la West Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo nchini ambayo yanalima kwa wingi kilimo cha Viazi, Karoti, Njegere na Mbogamboga
Siha. Vijana wa bodaboda wa Ngarenairobi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameomba kupatiwa maeneo ya kulima katika msitu wa hifadhi wa West Kilimanjaro, hatua ambayo itawawezesha kujiongezea kipato na kuondokana na hali ngumu za kimaisha.
Eneo la West Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo nchini ambayo yanalima kwa wingi kilimo cha Viazi, Karoti, Njegere na Mbogamboga.
Vijana hao wametoa ombi hilo leo Mei 16, 2023 wakati wakiwasilisha changamoto zao kwa kamati ya utekekezaji ya umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, ikiongozwa na mwenyekiti, Ivan Moshi.
Akizungumza kiongozi wa kundi la bodaboda Ngarenairobi, Thobias Pius amesema changamoto kubwa inayowakabili ni hali ngumu ya kimaisha na kwamba endapo watapewa maeneo ya kilimo, wataweza kulima mazao mbalimbali kibiashara na kujikwamua kiuchumi.
"Vijana wa Bodaboda tunakabiliwa changamoto mbalimbali ikiwemo kipato duni, na ili kukabiliana na changamoto hii, tunaomba kupatiwa maeneo ya kilimo kwenye Msitu wa West Kilimanjaro, ili vijana tuweze kujiimarisha kiuchumi".
"Maeneo yale yanatolewa kwa watu kwa ajili ya kilimo, tunaomba na sisi vijana tuangaliwe ili kujikita kwenye kilimo na kuweza kujikwamua kiuchumi, kwani kwa sasa maisha ni magumu".
Aidha kiongozi huyo ameomba pia vijana kupatiwa maeneo ya maegesho pamoja na mikopo ya pikipiki ili kuondokana na zile wanazokodisha ambazo nyingi wanazopewa ni chakavu.
"Tunaomba serikali itusaidie kupata mikopo ya pikipiki ili kila mtu aweze kumiliki ya kwake na kuondokana na changamoto ya kukodisha pikipiki za watu, hii itatusaidia kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi".
Akijibu changamoto hizo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi ameahidi kufuatilia suala hilo la maeneo ya kilimo, ili kuona uwezekano wa vijana kujiingiza kwenye kilimo na kujikwamua kiuchumi.
"Tumesikia changamoto ya maegesho kwa bodaboda, niwahakikishie ndani ya mwezi juni, tutakuwa tumetengeneza eneo la maegesho hapa, lakini pia tumesikia changamoto ya eneo la kilimo West Kilimanjaro, niwaahidi kulifuatilia hili na kulifanyia kazi".
Moshi ambaye ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji UVCCM Taifa, pia amewaonya vijana hao wa bodaboda, kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiyagharimu maisha ya wengi.
"Naomba vijana wenzangu muwe makini muwapo barabarani na vyombo hivi vya moto, na hakikisheni mnafuata sheria za usalama barabarani, kwani hatuhitaji kuona tunapoteza vijana wetu kwenye ajali za bodaboda na bajaji"
Katika Wilaya ya Siha, kamati ya utekelezaji ya UVCCM Mkoa, imetembelea vijiwe vya bodaboda,bajaji na kuzungumza na vijana kusikiliza changamoto zinazowakabili pamoja na kukagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi.