Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyefungwa kwa kujaribu kumbaka bibi wa miaka 76 apunguziwa adhabu

Muktasari:

  • Jaji Martha Mpaze ametumia mamlaka yake kubadili shitaka hilo hadi kuwa shambulio baya la aibu, ambalo linaangukia katika kifungu cha 138A (1) cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo 2022.

Mtwara. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, imembadilishia kifungo, mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kujaribu kumbaka bibi kizee wa miaka 76. Hivyo atatumikia miaka mitano.

Mahakama hiyo imeeleza hapakuwa na ushahidi unaoonyesha mrufani, Juma Hamisi, alijaribu kumvua nguo bibi hiyo, kumgusa au kumfunua na kuziacha wazi sehemu zake za siri.

Hii ni kwa kuwa ushahidi unaonyesha katika wakati ambapo mrufani alivua shati lake, bibi huyo alifanikiwa kutoroka kutoka eneo la tukio na mshtakiwa akakamatwa na shahidi wa pili na wa tatu waliojitokeza kutoa msaada.

Ni kutokana na ushahidi huo, Jaji Martha Mpaze ametutumia mamlaka yake kubadili shitaka hilo hadi kuwa shambulio baya la aibu, ambalo linaangukia katika kifungu cha 138A (1) cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo 2022.

Awali mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa eneo la Mitambo Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, alishtakiwa  na kutiwa hatiani kwa kosa la kujaribu kubaka kinyume na kifungu 132(1) na (2) (a) cha Kanuni hiyo ya adhabu.

Kosa hilo lilidaiwa kutendeka Juni 3,2024 katika eneo la Mitambo lakini mshtakiwa akakana kulitenda akisema siku ya tukio alikuwa amezidiwa na ulevi na kujikuta mtaa ambao siko alikokuwa anakwenda ndipo alipokamatwa.


Tukio lilivyokuwa

Ushahidi wa upande wa mashitaka ulieleza kuwa siku ya tukio saa 8:30 usiku, akiwa amelala ndani ya nyumba yake, mtu asiyemfahamu aliingia bila uhalali wa kisheria na kuzima taa iliyokuwa ikiwaka.

Baadaye mtu huyo alimlalia juu yake, akapumzika katika kifua chake na kwamba bibi huyo alishtuka kutokana na uvamizi huo na alipobaini kuwa mtu yuko juu ya kifua chake, haraka alichukua tochi na kummulika mvamizi huyo usoni.

Ndipo mtu huyo alipotishia kumuua endapo angepiga kelele, ambapo wakati mtu huyo amesimama akianza kuvua shati alilokuwa amevaa, bibi huyo alipata nafasi ya kutoroka na kutoka nje akipiga mayowe ya kuomba msaada.

Shahidi wa pili, Ahamadi Walii na shahidi wa tatu, Abdan Selemani walisikia kelele hizo na kukimbilia eneo la tukio kutoa msaada ambapo Walii ndio alikuwa wa kwanza kufika na kukutana na mtu akitoka kwa bibi kifua wazi akikimbia.

Kulingana na shahidi huyo, alifanikiwa kumkamata na baadaye kidogo alifika shahidi wa tatu katika eneo hilo, na ndipo walipobaini waliyemkamata ni Juma Hamis na kwamba katika purukushani, aliwaumiza kwa kisu wote wawili.

Mashahidi hao walieleza kuwa kwa bahati nzuri, wanakijiji wengine wengi walijitokeza na kusaidia kumdhibiti mrufani na kumkamata na kisha kumkabidhi kwa Polisi na kufunguliwa shitaka la kujaribu kumbaka bibi kizee huyo.


Utetezi wake ulivyokuwa

Katika utetezi wake, mrufani huyo alikanusha kutenda kosa hilo na kudai kuwa siku hiyo ya tukio, alikuwa amekunywa pombe huko eneo la Madimba na kimakosa, alijikuta amepita njia ambayo sio sahihi, ambayo ilikuwa haielekei kwake.

Akiwa katika njia hiyo ambayo haifahamu, alisimamishwa na mtu ambaye alimuuliza anaenda wapi, na baada ya kumjibu, ghafla mtu huyo alianza kupiga kelele, kelele ambazo ziliwavuta wananchi wengi wa eneo hilo.

Baba yake wa kambo alifika eneo hilo na kuagiza apelekwe ofisi ya kijiji lakini hata hivyo wanakijiji waliamua kumrudisha Madimba na njiani walimpiga.

Katika kupishana huko, mrufani huyo alieleza kuwa alichomoa kisu na kuwajeruhi shahidi wa pili na wa tatu na baada ya kuona amewajeruhi wawili hao, walibadilisha uelekeo na kumpeleka kituo cha Polisi Mtwara.

Akiwa kituoni hapo alijulishwa kuwa atashtakiwa kwa kosa la kujaribu kubaka na kusema kesi hiyo ilitengenezwa, lakini Mahakama iliridhishwa na ushahidi wa upande wa mashitaka na kumuhukumu kifungo cha miaka 30 jela.


Hukumu ya Jaji

Mrufani huyo hakuridhishwa na hukumu ya kifungo cha miaka 30 hivyo akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara ambayo ilitoa hukumu yake Mei 2,2025 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa katika mtandao wa Mahakama Mei 6,2025.

Baada ya kupitia sababu za rufaa na hoja za Jamhuri, Jaji Mpaze alisema hoja za rufaa zilikuwa ni pamoja na Jamhuri ilishindwa kuthibitisha shitaka na kuacha mashaka, uchambuzi usio sahihi wa ushahidi na utata katika utambuzi wake.

Hata hivyo, Jaji Mpaze alichambua hoja moja baada ya nyingine na kubaini hazina msingi wowote, lakini akasema mahakama imebaini shitaka la kujaribu kubaka halikuwa limethibitishwa na badala yake, akamtia hatiani kwa shambulio la aibu.

Jaji alirejea maelezo ya bibi huyo akisimulia nini kilitokea akisema siku hiyo saa 8:30 usiku, kijana mmoja aliingia nyumbani kwake wakati taa inawaka na akaizima na kuingia kitandani kwake na kulala juu ya kifua cha bibi huyo.

Kulingana na ushahidi wa bibi huyo, alichukua tochi na kukuta mtu yuko juu ya kifua chake na akatishia angemuua kama angepiga kelele, hapo mtu huyo akavua shati lake akiwa amesimama na yeye kupata upenyo wa kutoroka kwenda nje.

Jaji alisema kwa kusoma neno moja baada ya lingine katika ushahidi huo, bibi huyo alieleza kuwa akiwa amelala, mrufani aliingia na kuzima taa na kulala juu yake na alipoamka alitumia tochi, alimuona mvamizi aliyetishia kumuua.

Baadaye alivua shati na hapo ndipo bibi huyo alifanikiwa kutoroka ambapo shahidi wa pili na wa tatu walifika baadaye na kufanikiwa kumkamata mrufani.

“Ingawa vitisho vya mrufani kuwa “nitakuua kama utapiga kelele” yalikuwa ni matishio mabaya, kinachoonekana lengo lake lilikuwa ni kumnyamazisha mwathirika badala ya kusaidia kumwingilia bibi huyo,”alisema Jaji.

Jaji alisema hakuna ushahidi kuwa mrufani alijaribu kumvua nguo bibi huyo, kumgusa sehemu zake zi siri au kumtaka akubali kufanya naye ngono, na ushahidi uliotolewa hauwezi kusababisha kosa la kujaribu kubaka kama kesi ilivyo.

Kulingana na Jaji, kwa kuutizama ushahidi, mshtakiwa alifanya kosa la shambulio baya la aibu  ambalo linaangukia kifungu cha 138(1) hivyo anapunguza adhabu aliyopewa kutoka kifungo cha miaka 30 hadi miaka mitano.