Veta yaagizwa kuandaa kozi zinazokidhi mahitaji ya jamii

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk Prosper Mgaya (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa chuo cha VETA Dodoma alipotembelea karakana ya Fani ya Elektroniki chuoni hapo Jijini Dodoma.
Muktasari:
- Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) imetakiwa kuongeza ubunifu kwenye kuandaa kozi na kuboresha vifaa vya utoaji mafunzo vinavyokidhi ukuaji wa teknolojia duniani.
Dodoma. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dk Prosper Mgaya ameitaka mamlaka hiyo kuongeza ubunifu kwenye kuandaa kozi za muda mfupi zinazojibu mahitaji halisi ya jamii ya Watanzania.
Dk Mgaya ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 14, 2023 alipofanya ziara katika ofisi za Veta Kanda ya Kati na Chuo cha Veta Dodoma ambapo ametembelea karakana kujionea shughuli za mafunzo zinazotolewa na chuo hicho.
Dk Mgaya ameainisha mikakati mbalimbali ya kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kuendesha shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
“Ni lazima tuongeze ubunifu katika kuandaa kozi za muda mfupi kujibu changamoto zinazowakabili wananchi kwenye shughuli zao za kiuchumi, tunafanya vizuri kwenye eneo la ubunifu lakini changamoto ni namna ya kuhakikisha ubunifu huo unaingia sokoni hivyo tunahitaji kuweka nguvu katika suala hili,”amesema Dk Mgaya.
Dk Mgaya ameeleza pia umuhimu wa kupata ithibati za kimataifa kwenye mafunzo yanayotolewa ili kuwezesha wahitimu wa Veta kutambulika kwenye soko la ajira kimataifa na kusisitiza nia yake ya kuwezesha walimu kupata mafunzo na ujuzi ndani na nje ya nchi.
Amekielekeza Chuo cha Veta Dodoma kuandaa kozi za aina mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya jamii na kuzitangaza ili wananchi wazifahamu na kujitokeza kujiunga na kozi hizo ili waweze kujipatia ujuzi wa kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Dkt Mgaya amesema mikakati hiyo itachangia kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwapatia Watanzania ujuzi utakaokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwamba Veta inategemewa kufanikisha malengo hayo.
Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara, John Mwanja amesema Kanda yake imejipanga vyema katika kuhakikisha vyuo vilivyopo kwenye kanda yake vinatoa mafunzo bora na kufikia wananchi wengi zaidi.
Mkuu wa Chuo cha Veta Dodoma, Stanslaus Ntibara amesema hadi sasa chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 4,350 ambapo 650 ni wa kozi za muda mrefu na 3,700 ni wa kozi za muda mfupi ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka 2022.