‘Jitokezeni mafunzo ufundi stadi’

Mgeni rasmi Kasongo Kisafa, akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu fani ya bomba, waliopata ufadhili wa E4D
Muktasari:
- Vijana mkoani Lindi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujiajiri.
Lindi. Licha ya kuwa na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi mkoani hapa, imeelezwa kuwa bado kuna mwamko mdogo wa vijana kujiunga na vyuo hivyo.
Hayo yameelezwa jana Novemba 12 na mkuu wa chuo cha Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Mkoa waLindi, Harry Mmari kwenye mahafali ya awamu ya tano ya vijana 218 waliohitimu mafunzo ya ufundi bomba nyumbani.
Mafunzo hayo yatokanayo na mradi wa kukuza ujuzi na ajira E4D yamefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA) na Shirika la misaada la Ujerumani (GIZ).
Amesema kuwa vijana wa Mkoa wa Lindi hasa vijana wa kike wanashindwa kuchangamkia fursa za masomo ya ufundi bomba majumbani na viwandani pamoja na uungaji vyuma,
"Wafadhili wamejitokeza kuwasaidia vijana wetu wa Manispaa ya Lindi, lakini hawataki kabisa kuja kusoma. Masomo yenyewe hutolewa kwa muda mfupi, lakini wanakuja vijana kutoka wilayani,” amesema Mmari.
Awali akisoma risala ya wahitimu, mhitimu Hadija Issa amesema kuwa changamoto iliyokuwepo ni vijana wa kike kutokuwa na mwamko, lakini sasa watatumia mafunzo hayo kujiajiri.
"Niwashukuru wafadhili kwa kutusaidia kupata masomo haya bila kulipia, ila niwaombe vijana wenzangu hasa wakike kujitokeza kuja kusoma kwani ujuzi utakao upata hapa ni wako na utakusaidia hata kujiajiri mwenyewe,” amesema Hadija.
Kwa upande wake mratibu wa mradi Mawazo Mataje amesema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwaingiza vijana katika mnyororo wa thamani ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
"Tulilenga kuwafikia vijana 700 lakini hadi sasa tunamaliza mradi huu leo kwa hii awamu ya tano tumeshawafikia vijana 887 ambapo sawa na asilimia 126.7ni zaidi ya lengo ambalo tuliliweka," amesema Mwazo
Naye Ofisa Elimu ya Mlipa kodi na Uhusiano, aliyemwakilishi Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa waLindi, Kasongo Kisafa amezitaka taasisi za fedha na Shirika la Viwanda vidogo (Sido) kuwasaidia vijana hao kuweza kuwapa mitaji na vifaa ilikiweza kujiajiri wenyewe.
"Niwaombe vijana wangu kujitahidi kuwa na nidhamu huko mnapo kwenda,uwe umeajiriwa au kujiajiri mjitahidi nidhamu," amesema Kasongo.
Kwa upande wa wazazi akiwemo Monica Mchena, ameishukuru Serikali pamoja na wafadhili kuwasaidia watoto ambao hawakuweza kuendelea na masomo.