Benki ya Dunia: Wanaotumia chini ya Sh7,834 kwa siku ni maskini kupindukia

Muktasari:
- Kiwango kipya kinatokana na PPP mpya zilizotolewa mwaka 2024 zikitokana na ukusanyaji wa data za mwaka 2021, ambapo bei za bidhaa za msingi kama chakula, mavazi na makazi zilionyesha kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imetangaza marekebisho ya kiwango cha kimataifa cha umaskini, ikipandisha kiwango cha chini kutoka Dola 2.15 za Marekani kwa siku (sawa na Sh5,614) hadi Dola 3.00 (Sh7,834) kwa siku.
Kwa muktadha huo, mtu yeyote anayeishi kwa kutumia kiasi cha chini ya Sh7,834 kwa siku sasa atahesabika kuwa anaishi katika umasikini uliokithiri, kulingana na viwango vipya vya kimataifa vilivyotangazwa Juni 2025.
Marekebisho haya yamefuatia kutolewa kwa takwimu mpya za uwezo wa kununua (PPP) Mei 2024, kupitia Mpango wa Ulinganifu wa Kimataifa (ICP), ambao hulinganisha bei za bidhaa na huduma kati ya nchi tofauti ili kuweka kipimo cha bei kinachowiana kwa nchi zote duniani.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mabadiliko haya yamelenga kuendana na mabadiliko ya viwango vya bei duniani na kutoa picha halisi zaidi ya kiwango cha chini cha maisha, hasa katika nchi za kipato cha chini.
PPP mpya zilizotolewa mwaka 2024 zilitokana na ukusanyaji wa data za mwaka 2021, bei za bidhaa za msingi kama chakula, mavazi na makazi zilionesha kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Viwango vipya vya PPP hutumiwa kubadili sarafu mbalimbali kuwa katika kipimo kimoja cha kulinganisha, hivyo kurahisisha tathmini ya hali ya umaskini duniani. Tangu kutambulishwa kwa kipimo cha ‘dola moja kwa siku’ mwaka 1990, Benki ya Dunia imekuwa ikihuisha kiwango hiki mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya hali ya kiuchumi na kijamii duniani.
Licha ya kuongezeka kwa thamani ya mstari wa umaskini, Benki ya Dunia imesisitiza kuwa, mbinu ya kupima umaskini uliokithiri haijabadilika. Kinachobadilika ni data na tafiti bora zaidi kutoka nchi maskini, ambazo sasa zinatoa picha sahihi zaidi kuhusu hali ya maisha ya watu na uwezo wao wa kumudu bidhaa na huduma za msingi.
Kiwango hiki kipya cha Dola 3 za Marekani kwa siku kinajumuisha maboresho ya upimaji wa hali ya ustawi wa watu katika nchi za kipato cha chini, kikilenga kupima ukosefu wa kipato kwa viwango vinavyokubalika kimataifa. Kiwango cha Dola 2.15 kiliwekwa miaka 8 iliyopita.
Aidha, licha ya mabadiliko haya, lengo la WB la muda mrefu la kupunguza umaskini uliokithiri duniani hadi chini ya asilimia tatu ifikapo mwaka 2030 bado halijabadilika.
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Thobias Swai amesema kuongeza kwa kiwango hicho hakuna athari ya moja kwa moja kwa wananchi isipokuwa kitaathiri utungaji na utekelezaji wa sera za nchi katika kupambana na umasikini.
“Huu ni wastani tu, wala haumaanishi kuwa gharama za maisha zitapanda kuanzia leo maana yake ni kuwa zimekuwa zikipanda tangu walipotoa tathimini ya mwisho. Kinachokwenda kuguswa hapo ni utungaji wa sera kwani idadi ya masikini wa kupitiliza sasa itaongezeka,” amesema Swai.
Amesema ni wajibu wa watunga sera sasa kuhuisha sera zilizopo ili kufanikisha mipango ya kupunguza kiwango cha umaskini miongoni mwa watu kama ilivyolengwa akisema kwa mabadiliko ya kiwango hicho tu kutaleta mabadiliko ya takwimu nyingi za kitaifa zihusuzo umasikini na hali ya kipato.
“Sera zitaguswa zaidi hata utekelezaji wake itabidi ubadilike maana kama kulikuwa na masikini milioni 15 sasa huenda wakaongezeka wakafika hadi milioni 20 hivyo unahitaji uwekezaji zaidi katika miradi ya kuwatoa watu katika umasikini kwakuwa idadi yao sasa inaongezeka,” amesema Dk Swai.
Mhadhiri wa Masuala ya Uchumi wa Fedha katika Chuo Kikuu Ardhi, Aziz Rashid amesema viwango hivyo vipya ni kiashiria na uhalisia wa maisha ya watu wengi, akisema Sh7,800 inayotajwa kwa hapa nchini inatosha kula lakini haiwezi kugharamia mahitaji wengine ya muhimu.
“Ongezeko la kiwango hicho ni ishara ya kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu, kwani hata hicho kiwango cha Dola 3 (Sh7,834) kinaweza kutosha kula tu lakini kuna mahitaji zaidi kama malazi, kuvaa na hata kutibia hivyo mahitaji ni makubwa kuliko hata hicho kiwango,” amesema Rashid.
Rashid amesema ili kubadili hali ya umaskini anashauri nguvu kubwa iwekezwe katika kuongeza uzalishaji wa chakula na ujuzi kwa wananchi ili kupata kipato zaidi kinachowawezesha kuishi juu ya viwango hivyo,” amesema Rashid.
Mhadhiri mwingine wa uchumi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano amesema muhimu ni kuzingatia kiwango cha kitaifa kwani mara nyingi hicho kiwango cha kimataifa mara nyingi kinakuwa juu kuliko kile cha ndani.
Dk Mwinuka amesema, “kutokana na hali ya uchumi wa dunia hata viwango vya kitaifa vya umaskini bila shaka vitaongezeka tukifanya kuendana na vipya vilivyowekwa.”
"Kwa hivyo, tunapaswa kuendelea kujiimarisha kiuchumi kupitia jitihada endelevu. Hii ni pamoja na uwekezaji wa kimkakati na kuongeza mapato ya Taifa. Mwishowe, lengo letu ni ukuaji imara wa uchumi na kuhakikisha kuwa, ukuaji huu unawanufaisha wananchi wote,” amesisitiza.