Prime
Tulenge kuondoa ubaguzi huu kwenye elimu

Muktasari:
- Unapotazama mwenendo wa elimu kati ya wanafunzi wa shule za umma na zile binafsi, unaona tofauti kubwa iliyopo ya kitabaka.
Arusha. Nimepata fursa ya kuishi katika mazingira ya elimu kwa maisha yangu yote kuanzia chekechea miaka mingi iliyopita hadi sasa nikiwa kama mwalimu au profesa wa chuo kikuu.
Nimepata pia fursa ya kusoma nje ya nchi yetu na kufundisha katika nchi kadhaa duniani.
Hivyo elimu ni hoja iliyo karibu sana na maisha yangu na uzoefu wangu wa maisha.
Si ajabu kwamba kila niendako na kila nchi nyingine niliyotembelea au niliyosoma au niliyofundisha, mawazo yangu mara nyingi yamejikita katika elimu, wanafunzi, ufundishaji na ujifunzaji.
Ukirejea makala zangu zaidi ya 200 katika gazeti la Mwananchi, utaona jinsi elimu ilivyo sehemu ya maisha yangu na ilivyo na nafasi kubwa katika tafakuri zangu za siku zote.
Katika tafakuri hizi endelevu kuhusu elimu, najikuta mara nyingi nikiwaangalia watoto na wajukuu zetu wasomao shule za msingi na sekondari na jambo moja haliishi kunifikirisha sana ni hili la kuwa na shule za Serikali au za kata kwa upande mmoja na shule za binafsi upande wa pili.
Takwimu nyingine zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya watoto wetu husoma shule za Serikali na asilimia 10 husoma shule za binafsi.
Maisha ya kishule ya tabaka hizi mbili za watoto wetu yanatofautiana kama vile mbingu na nchi.
Wote ni wanafunzi lakini baada ya hapo tofauti zao ni kubwa. Kwangu mimi kama mdau wa elimu tofauti hizi zinatisha.
Ubaguzi
Tofauti hizi zinawabagua watoto wetu na kuwaweka katika makundi mawili: wanaopata elimu bora na wanaopata elimu hafifu.
Nauona huu kama ni ubaguzi ambao kama Taifa hatuna budi kuutokomeza, walau tupige hatua kidogo kidogo kila mwaka hadi tufanikiwe. Si haki kuendelea na mfumo huu wa elimu.
Tujadili kwa kinaganaga tofauti zilizopo kati ya makundi haya mawili ya elimu. Kwanza kabisa uwepo wa matabaka haya mawili ya elimu unaonyesha jinsi wazazi wengi walivyo na uwezo mdogo wa uchumi. Hawawezi kuwapeleka watoto wao shule za binafsi. Wanatamani wafanye hivyo lakini hali halisi inawanyima. Ni wazazi maskini. Ni wazazi karibu asilimia 90 ya wazazi wote. Tutaendelea na umaskini huu hadi lini?
Pili, watoto wa shule za binafsi asubuhi wana usafiri mzuri wa kwenda shule, ilihali wenzao wa familia maskini wanatembea kwenda shuleni, wengine kwa zaidi ya kilomita mbili au tatu. Nawaona watoto hawa mtaani katika kata ninayoishi. Ukiwa wewe ni binadamu unajitambua vizuri, unayethamini utu, utaumia kama vile mimi ninavyoumia rohoni nikiwaona hawa watoto wetu na wajukuu zetu wakitembea mwendo mrefu kwenda shule.
Hatari kwa mtoto mdogo kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni ni lukuki. Hawa watoto ikinyesha mvua ni yao, ikiwa baridi ni yao, kuna matope na vumbi watajijua wenyewe. Mwezi huu hapa ninapoishi ni baridi.
Unawaona watoto hawa wana kasweta kadogo na wengine hata sweta hawana. Wachache wana mabuti ya mpira katika matope, wengi wamevaa viatu vya kawaida vinavyobeba matope.
Mtoto huyu aliyelowa mvua, au aliyekaangwa katika baridi ya asubuhi, au aliyetembea mwendo mrefu, anategemewa afike shuleni kwa wakati. Akichelewa anapata adhabu, mahali pengine adhabu ya viboko.
Ninapinga na nitaendelea kupinga adhabu ya viboko shuleni kwa maisha yangu yote.
Mtoto hana mwavuli, amelowa mvua, anatetemeka baridi, huyu anachapwa viboko ati amechelewa shule. Kama huu si uendawazimu basi sielewi vizuri maana ya neno hilo.
Wendawazimu mkubwa zaidi ni kutegemea mtoto huyu asome vizuri, aelewe masomo na afanye vizuri katika mitihani yake.
Ni miujiza ya Mungu kwamba wengine katika watoto hawa hufaulu na kuendelea na masomo.
Lakini si ajabu kwamba ufaulu wa watoto hawa na ule wa shule za binafsi huwa ni tofauti sana.
Huyu mtoto aliyechapwa kwa kuchelewa shuleni, asiye na sweta nzito wakati wa baridi, hapati vitabu vya kusoma, hapati fursa nzuri ya maktaba ya shule, hana fursa ya kutumia maabara kwa sababu haipo shuleni, au kama ipo, haina vifaa tarajiwa, huyu tunategemea ashinde mitihani vizuri.
Mwenzake wa shule za binafsi ana usafiri kwenda shule, amevaa sare nzuri na sweta nzuri na nzito, amebeba begi lililojaa vitabu na madaftari ya kazi za shule alizofanyia nyumbani (homework), na kadhalika.
Tofauti ya kitaaluma kati ya watoto hawa wawili ni kubwa mno. Tutaendelea na ubaguzi huu hadi lini?
Twende kwenye chakula. Watoto wa shule za binafsi wanapata mlo wa mchana, wale wenzao wa shule za umma wanashinda kwa njaa.
Katika shule mojawapo ninayoifahamu hapa kwenye kata yetu ni wanafunzi asili mia 10 tu wanaopata mlo wa mchana. Unategemea mwanafunzi wa umri wa miaka minane afanye vizuri katika mitihani akiwa na njaa, hakupata vitabu vinavyotakiwa, anatembea umbali mrefu kila siku, anakaangwa na baridi, au jua au matope au mavumbi, unategemeaje mtoto ashindane kimasomo na yule wa shule ya binafsi?
Katika makala kama hii hakuna nafasi ya kueleza shida zote wanazopata hawa watoto wetu katika shule za umma. Tukiangalia uwiano wa wanafunzi na mwalimu darasani, hapa ni mbingu na nchi pia.
Mjukuu wangu yuko darasa la tatu katika shule ya binafsi na darasani wapo 31. Hebu ingia darasani katika shule ya umma. Huenda ukakuta wanafunzi 50 au zaidi darasani. Mahali pengine ni wanafunzi 90 au zaidi!
Ina ajabu
Sasa jambo la ajabu zaidi ni kwamba hawa watoto wa matabaka mawili haya wanapata mitihani iliyo sawa.
Mmoja ametayarishwa vizuri, mwingine amepata ellmu duni. Ni lazima taifa hili liachane na ubaguzi huu ambao unawaathiri watoto wetu kwa maisha yao yote.
Mhitimu wa kidato cha nne wa shule za binafsi anajiamini, anamudu vizuri masomo yote, anaongea lugha za Kiswahili na Kiingereza vizuri, na amepata divisheni ya ya kwanza au ya pili katika mitihani ya taifa.
Yule wa shule za umma kwa wastani amepata divisheni tatu au nne au amefeli kabisa. Hapana, tuliangalie hili na tuwe na mikakati ya kuondoa ubaguzi huu katika elimu.
Hauna tija kwa Taifa letu. Unagawanya Taifa kati ya wachache walioelimika vizuri na wengi waliopata elimu rasharasha.
Prof. Raymond S. Mosha
(255) 769 417 886; [email protected]