Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa alilia somo la maadili shuleni

Muktasari:

  • Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Arusha hivi karibuni, anasema bila kuwa na msingi wa maadili, masomo yote mengine yanakosa mwelekeo.

Mtaalamu bobezi wa falsafa na maadili nchini, Profesa Raymond Mosha, ametoa wito kwa Serikali, wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kulitambua somo la maadili kuwa somo  mama, lililo huru na la lazima kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, akieleza kuwa somo hilo ni msingi wa mafanikio ya elimu na maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwananchi jijini Arusha hivi karibuni, anasema bila kuwa na msingi wa maadili, masomo yote mengine yanakosa mwelekeo,  kwani maadili ndio yanamjenga binadamu kuwa na utu, uwajibikaji na uaminifu, mambo anayosema  ni muhimu katika jamii yoyote inayotaka kupiga hatua.

“Somo la maadili lisimame peke yake kwa sababu ni somo mama. Masomo mengine yote yanategemea uadilifu wa mtu. Bila maadili, nchi haisongi mbele, kwani ni somo linalojenga utu wa binadamu tangu akiwa mdogo,” anasema Profesa Mosha.

Mbali na kuhimiza maadili kuwa somo linalojitegemea, Profesa Mosha anasema hata masomo mengine ya kawaida kama hisabati, sayansi, au lugha yanapaswa kufundishwa kwa mtazamo wa kimaadili kwa kuwa kila somo lina maadili yake ya ndani ambayo humjenga mwanafunzi kuwa raia mwema.

Anasema moja ya sababu za matatizo ya kijamii na kisiasa nchini ni kushuka kwa maadili katika jamii.

“Tunapitia wakati mgumu. Kuna matatizo ya kisiasa, kijamii, hata kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na ukosefu wa maadili. Wahitimu wengi wanamaliza shule bila kujengewa msingi wa maadili, hali inayochangia matatizo kazini na kwenye jamii kwa ujumla,” anasema.

Anatolea mfano wa lugha za matusi kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni ishara ya jamii inayokosa heshima na maadili, jambo ambalo linaweza kuzorotesha mshikamano wa kitaifa.

Haya na mengineyo yanayoendelea nchini, anasema yanaweza kupatiwa dawa ikiwa somo la maadili litapewa msukumo wa kutosha katika ngazi zote za elimu.

Hata hivyo, kwa sasa, kufuatia mabadiliko ya mtalaa wa elimu ya msingi, Serikali imeanzisha somo la Historia ya Tanzania na maadili ambalo hata hivyo, Profesa Mosha anasema maadili hayakupaswa kuchanganywa ni kitu kingine kutokana na umuhimu wake.

Anaeleza kuwa kuwa vyuo vingi duniani tayari vimetambua umuhimu wa maadili na kulifanya somo hilo kuwa la lazima kwa wanafunzi wote, huku akishauri Tanzania ichukue hatua hiyo mapema ili kujenga kizazi cha waadilifu na viongozi bora wa baadaye.

Kuhusu mabadiliko hayo ya mitalaa, anasema kuwa mafanikio yake sambamba na ya sera za elimu,  haviwezi kufikiwa iwapo walimu wanaofundisha hawajaandaliwa kwa namna ya kuhimiza na kuingiza maadili katika ufundishaji wao.

“Ningekuwa na uwezo, ningependekeza kila somo lifundishwe pamoja na maadili. Lakini pia lazima tufanye mageuzi ya kweli katika vyuo vya ualimu. Walimu watakaowezesha Serikali kufikia malengo hayo lazima watayarishwe vizuri,” anasema.


Lugha ya kufundishia

Kuhusu mjadala wa lugha ya kufundishia, Profesa Mosha anapendekeza Kiswahili kitumike kama lugha ya msingi kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu. Anasema wanafunzi wengi wa Tanzania wanaongea Kiswahili na hivyo kuelewa vizuri zaidi wanapofundishwa kwa lugha hiyo.

“Sisi tunang’ang’ania Kiingereza kwa sababu ambazo hazina msingi. Tufundishe kwa Kiswahili, lugha ya Taifa inayotumiwa na wengi. Watoto wakifundishwa vizuri, wataelewa kwa kina. Kiingereza na lugha nyingine zifundishwe kwa ufasaha kama lugha za kigeni, lakini si lugha ya kufundishia,” anaeleza.

Anaonya kuwa kubadilika kwa lugha ya kufundishia kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza katikati ya safari ya elimu,  kunachangia wanafunzi kufeli na kupoteza mwelekeo wa kitaaluma.

Kwa sasa mfumo wa elimu unazitambua lugha zote mbili katika mfumo wa elimu. Wakati Kiswahili kikitumika katika ngazi ya msingi, Kiingereza kinatumika kuanzia sekondari hadi elimu ya juu.

Mfumo wa elimu na vipaji vya watoto

Akizungumzia mfumo wa elimu nchini, Profesa Mosha anasema ingawa kuna juhudi za mabadiliko, bado utekelezaji wake ni hafifu na hautoshelezi mahitaji halisi ya jamii.

Anatolea mfano wa nchi kama Finland ambapo elimu hujikita katika kugundua na kukuza vipaji vya watoto tangu hatua ya awali ya maisha yao ya elimu.

“Finland mwanafunzi anapoanza chekechea anasoma katika mazingira ya utulivu, walimu wanafuatilia vipaji vya kila mtoto na kuwasaidia kuvikuza. Hapa kwetu bado tupo kwenye mfumo wa kukariri. Hatujengi uwezo wa kufikiri wala kubuni,” anasema.

Anasema kuwa katika nchi hiyo, wanafunzi wa elimu ya awali hawazidi 25  darasani, hali inayomwezesha mwalimu kushughulika na kubaini vipaji vya watoto wake na kisha kuwajulisha wazazi.

 “Taifa lile limeendelea tunapaswa kuwa na mfumo wa elimu unaojali vipaji hata kama idadi siyo ndogo darasani lakini walimu watayarishwe kuona mtoto anaelekea wapi ili wanapofundishwa wafundishwe kwa namna inayojali vipaji vyao,”anaeleza.

Anapendekeza Taifa kuwa na  mfumo wa elimu itakayomsaidia mtoto wa Kitanzania kuwa na uwezo wa kujitambua kama mtu anayeweza kuchangia maendeleo kwa njia ya kipekee, bila kumsukuma kufuata njia moja tu ya ajira kama ilivyozoeleka.

Aina ya elimu anayoitamani

Akijibu kuhusu aina ya elimu anayoiona inafaa kwa Tanzania, Profesa Mosha anasema ni elimu inayotambua somo la maadili kama msingi na inayoongozwa na walimu waliopikwa kufundisha maadili.

“Elimu itakayomsaidia mtoto wa Kitanzania ni ile inayomwandaa kuwa mzalendo, mwadilifu, mchapakazi na mtoa huduma kwa jamii. Lazima ijikite pia katika kukuza vipaji vya wanafunzi na si kuwapa tu maarifa ya kukariri mitihani,” anafafanua na kuongeza:

“Maadili ni msingi. Elimu bila maadili si elimu kamili. Tuwekeze katika kuandaa walimu wa maadili, kuboresha vyuo vya ualimu, na kuijenga jamii ya watu wanaojali wenzao. Tukifanya hivyo, tutarudisha heshima ya Taifa letu.”

Anaongeza: “Nikiangalia elimu hapa nchini mimi nataka kulia, nikilinganisha na mataifa mengine jinsi watoto wanavyopata bahati. Hapa kwetu bado sana.Bajeti kwa ajili ya sekta ya elimu ni ndogo iongezwe.

“Mfumo wenyewe wa kufundisha ni ule wa kukariri, mtoto anakariri anakosa uwezo wa kufikiri, kujadili au kujenga hoja tofauti na enzi zetu.Tulivyokuwa tunasoma zamani tulikuwa na mijadala shule ilitujenga na kuwa na uwezo wa kujenga hoja,”

‘’Nimeona nchi zilizoendelea  watoto wanahitimu ila hawafikirii kuajiriwa mwanafunzi anamaliza chuo kikuu hapa kwetu anawaza kuajiriwa haipaswi kuwa hivyo hayo ni mawazo ya zamani sana.

Natamani kuona utayari wa kisisasa ili kuboresha sekta ya elimu na tuwekeze zaidi kwenye vyuo vya ualimu ili watoto wetu wafundishwe na walimu wenye vigezo.’’


Akumbukia elimu ya mababu

Akiangazia falsafa za wazee wa zamani, Profesa Mosha anasema bado kuna hazina kubwa ya maarifa kutoka kwa mababu zetu, ambayo bado inaweza kutumika katika dunia ya leo kwa mtazamo wa sasa.

“Mababu walifundisha kwa matendo. Tulijifunza shambani, porini na majumbani. Hatufundishi kama wao lakini tunaweza kutumia falsafa zao kama mshikamano, kuheshimu mazingira, na kuishi kwa kutegemeana,” anasema.

Anasema matukio kama mabadiliko ya tabianchi na ukame unaosababishwa na ukataji miti, yanaonyesha namna ambavyo jamii imeshindwa kuona uhusiano kati ya mazingira na maisha yake, jambo ambalo zamani lilizingatiwa sana na wazee.


Wasifu wake

Profesa Mosha, ni msomi bobezi wa masuala ya falsafa na maadili, aliyefundisha  vyuo mbalimbali hapa nchini, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Alirejea nchini mwaka 2011 na kwa sasa anaendelea kufundisha kwa njia ya mtandao katika chuo kikuu kilichopo Marekani.