Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye mahitaji maalumu kicheko vyuo vikuu

Muktasari:

  • Vyuo vingi nchini vina miundombinu rafiki kwa wanafuzi wenye ulemavu,  ikiwa ni  matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Moshi. “Nilipochaguliwa kuja chuoni nilifikiri ulemavu wangu ungefanya niwe na maisha magumu chuoni, nilihisi nitakuwa mzigo kwa wenzangu kutokana na hali yangu kutokana na taarifa nilizokuwa nazo kuhusu mazingira ya chuo”.

Hii ni kauli ya Emmanuel Kelvin kijana wa miaka 21 mwenye ulemavu wa miguu  anayesoma mwaka wa kwanza shahada ya Teknolojia ya Habari katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Alipochaguliwa kujiunga na chuo hicho hofu yake kubwa ilikuwa ni namna gani ataishi na hali ya ulemavu aliyonayo kwa kile alichokuwa anafahamu kwamba miundombinu ya taasisi hiyo si rafiki kwa watu wenye ulemavu wa aina yake.

MoCU ni miongoni mwa taasisi kongwe za elimu ya juu ina majengo ya miaka ya 1960 yakiwa na milango yenye wembamba, ngazi za kupandia zisizofikika kwa wote, vyoo visivyokuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu, na njia za changarawe zilizowazuia wengi.

Hata hivyo,  hofu inaondoka kwa kijana huyu baada ya kufika chuoni na kukuta mazingira rafiki yanayoendana na hali yake ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Mradi huo unaotekelezwa chuoni hapo pamoja na mambo mengine unahusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa watu wenye ulemavu ili kuwatengenezea mazingira wezeshi katika safari yao ya kuitafuta elimu ya juu.

Kelvin anakuwa miongoni mwa wanufaika wa malengo ya mradi huu, anatembea chuoni kwa uhuru, anashiriki shughuli za uongozi wa wanafunzi, na pia huwasaidia wanafunzi wapya wenye ulemavu kuzoea maisha ya chuo.

“Nataka kuwa sababu ya mtu kuamini kuwa inawezekana, hata mlemavu anaweza kufikia hatua yoyote ya mafanikio endapo atatengenezewa mazingira wezeshi na chuo changu ni mfano mzuri katika hilo,

“Huenda kuna wenzangu ambao wana hofu kama niliyokwua nayo mimi hapo awali au wazazi wanahofia kuwapeleka watoto wao kwenye taasisi za elimu kwa  kuhofia mazingira, niwajuze kwamba sasa mambo yamebadilika na mahitaji ya watu wenye ulemavu yanapewa kipaumbele ili na wao wapate fursa ya kujifunza na kupiga hatua kwenye elimu, anasema Kelvin.

Sauti hii ya matumaini ya Kelvin inathibitisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi unalingana na Lengo la Maendeleo Endelevu namba 4 (SDG 4) linalosisitiza elimu bora, jumuishi, na fursa ya kujifunza kwa wote.

Kupitia mradi huo MoCU imeweza kutekeleza mkakati huo ambao umetoa matumaini kwa Kelvin na watu wengine wenye ulemavu wanaosoma na kufanya shughuli zao chuoni hapo na kufanya dhana ya elimu jumuishi kutokuwa ya nadharia bali vitendo.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Alfred Sife, anasema kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo, sera kuhusu wanafunzi wenye ulemavu  ziliwekwa chini ya sera za jinsia lakini sasa mambo yamebadilika.

“Tumeanzisha sera na miongozo mahsusi kwa watu wenye mahitaji maalum kwa  fedha hizi, tunajenga majengo mapya ya Tehama na taaluma ambayo yanazingatia upatikanaji wa elimu kwa wote. Pia tumekarabati majengo ya zamani kwa kuongeza miteremko, njia pana na maeneo ya kupumzikia. 

“Majengo yote ya kitaaluma sasa yanafikika kwa watu wote. Idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum imeongezeka kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka miwili. Zaidi ya watumishi 50 wamepatiwa mafunzo kuhusu elimu jumuishi, na maabara ya upatikanaji kidijitali ipo mbioni kukamilika kwa ajili ya wanafunzi wenye changamoto za kuona na kusikia” anasema Profesa Sife.

Mtaalamu wa elimu jumuishi na masuala ya jinsia katika MoCU kupitia HEET, Dk Asteria Gaiza anakiri kuwa hapo awali miundombinu ya chuo hicho hayakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu lakini sasa mahitaji yao yamekidhiwa.

“Miundombinu ya zamani kutoka enzi za ukoloni ilikuwa kikwazo kikubwa. Wanafunzi waliotumia viti mwendo walishindwa kabisa kuhudhuria madarasa ya juu, vyoo vilikosa vifaa maalum, na hata walimu hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.”

Anasema mradi huo haukuishia kwenye majengo pia unafadhili mafunzo kwa wakufunzi na watumishi wa vyuo, kuwawezesha kutambua na kusaidia wanafunzi wenye ulemavu.

“Kabla ya haya mafunzo, walimu wetu wengi hawakujua namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum.Sasa tunaendesha warsha kila mara. Walimu wamebadilika wanajitahidi na wanabadilika kulingana na mazingira ya wanafunzi.

 Zaidi ya kujenga uwezo tumeanzisha huduma za msaada kwa wenye ulemavu pamoja na maeneo salama. Vyoo, kumbi za mihadhara, na maktaba sasa zinafikika kwa urahisi na zinazingatia mahitaji ya watumiaji wa viti mwendo, wanafunzi wasioona, na wengine”    anasema Dk Gaiza.

Mmoja wa wazazi wenye watoto wenye ulemavu, Janeth Shija anasema: “Nilikuwa na wasiwasi mkubwa kumpeleka mwanangu chuo, nilihofia usalama wake na namna ambaye angehudumiwa. Lakini nilipotembelea chuo nilifarijika kuona miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu vitabu vya maandishi ya nukta nundu hii ilinipa amani kubwa ya moyo.