Uwanja atakapoapishwa Dk Ruto wafurika, wananchi wazuiwa

Muktasari:
Wananchi wamezuiwa kuingia katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo zinafanyika sherehe za kuapishwa Dk William Ruto kuwa Rais wa Kenya kutokana na uwanja huo kujaa.
Nairobi. Wananchi wamezuiwa kuingia katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi ambapo zinafanyika sherehe za kuapishwa Dk William Ruto kuwa Rais wa Kenya kutokana na uwanja huo kujaa.
Kutokana na hatua hiyo, Polisi wamewataka wananchi kuangalia uapisho huo kupitia vyombo vya habari wakiwa nyumbani.
Ruto aliyeibuka mshindi katika uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022, anaapishwa leo Jumanne Septemba 13, 2022 kuchukua nafasi ya Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake wa uongozi wa miaka kumi.
Ruto ambaye ni Naibu wa Rais, aliibuka mshindi katika uchaguzi kwa kumshindi mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga mwenye miaka 77.
Mbali na Ruto, mwingine atakayeapishwa leo ni Naibu wake wa Rais, Rigathi Gachagua.
Rais aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 sawa na asilimia 50.49 huku Raila akiambulia kura milioni 6.9 sawa na asilimia 48.8
Baada ya matokeo hayo, Raila aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta alipinga matokeo hayo katika Mahakama ya Juu nchini humo ambayo ilisikiliza kesi hiyo na kuyatupilia mbali mapingamizi aliyokuwa ameyaweka dhidi ya Ruto.
Katika uamuzi wake, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Raila na waleta maombi wenzake walishindwa kuthibitisha kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.
Baada ya kiapo hicho, Kenyatta atakuwa ni Rais mstaafu. Marais wengine waliowahi kuongoza taifa hilo ni, Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki ambao wote wamekwisha fariki kwa nyakati tofauti.