Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia kuhudhuria Dk Ruto akiapishwa Kenya

Muktasari:

Dk William Samoei Ruto aliyeibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9,2022, leo Jumanne anaapishwa kuwa Rais wa Kenya, kuchukua nafasi ya Uhuru Kenyatta ambaye anamaliza muda wake wa uongozi wa miaka kumi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi na wageni mbalimbali watakaoshuhudia Dk William Samoei Ruto akiapishwa kuwa Rais wa Kenya.

 Ruto ataapishwa kuwa Rais wa tano leo Jumanne, Septemba 13, 2022 katika Uwanja wa Kasarani.

Anachukua nafasi ya Uhuru Kenyatta, ambaye anamaliza muda wake wa utawala wa miaka kumi aliyoianza Aprili 9, 2013, akivaa viatu vya Mwai Kibaki.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa jana Jumatatu imesema, Rais Samia ataambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri wa Tanzania na Zanzibar, akiwemo Balozi Libarata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje.

Ruto ambaye ni Naibu wa Rais, ataanza safari ya kuwaongoza Wakenya, baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 kwa kumshindi hasimu wake wa karibu, Raila Odinga mwenye miaka 77.

Mbali na Ruto mwenye miaka 55 ambaye alizaliwa Desemba 21, 1966, mwingine atakayeapishwa  ni Naibu wake wa Rais, Rigathi Gachagua.

Rais huyo mteule wa Muungano wa Kenya Kwanza, alipata kura milioni 7.1 sawa na asilimia 50.49 huku Raila wa Muungano wa Azimio akiambulia kura milioni 6.9 sawa na asilimia 48.8

Baada ya matokeo hayo, Raila aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta alipinga matokeo hayo katika Mahakama ya Juu nchini humo ambayo ilisikiliza kesi hiyo na kuyatupilia mbali mapingamizi aliyokuwa ameyaweka dhidi ya Ruto.

Katika uamuzi wake, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Raila na waleta maombi wenzake walishindwa kuthibitisha kulikuwa na udanganyifu na uchakachuaji wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi, siku na baada ya kupiga kura.

Baada ya kiapo hicho, Kenyatta atakuwa ni Rais mstaafu. Marais wengine waliowahi kuongoza taifa hilo ni, Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki ambao wote wamekwisha fariki kwa nyakati tofauti.