UVCCM Ulanga yawataka vijana kuacha kulalamika

Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM Wilaya ya Ulanga, Thomas Machupa (katikati)
Morogoro. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Ulanga mkoani hapa umewataka vijana nchini kuacha kuilalamikia Serikali kila wakati juu ya ajira na badala yake wajikite kuanzisha miradi ya kujiajiri kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo kilimo, burudani na biashara.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM wilaya hiyo, Thomas Machupa amesema hayo Juni 6, 2023 mjini Morogoro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya Tamasha la kumpongeza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Ulanga, Salim Alaudin Hasham kwa namna alivyowezesha vijana kujiajiri.
Machupa amesema katika kuhakikisha wanatekeleza ilani ya CCM viongozi hao wameweza kuwafikia vijana wengi kwa kuwagusa moja kwa moja kwenye suala la Mikopo ya Halmashauri kupitia vikundi vyao.
“Huu ni wasaa sasa wa vijana wa CCM kuacha kulalamika kwani kila sehemu tunaonekana ni watu wa kulalamika tu lakini tunatakiwa kushukuru kwa hata tunachokipata ili upate vingi inabidi ushukuru kwanza kwa ulichokipata,” amesema.
“Hatuna budi kwenye tamasha letu kumpongeza Rais, Mbunge wetu na Serikali kwa ujumla kutugusa kwa namna moja ama nyingine katika mambo makubwa yanayoendelea ya kimaendeleo hasa mkoa wetu wa Morogoro hususani wilaya ya Ulanga, vijana sasa wanajitambua na kujituma kwa bidii,”amesema
Juni 10, 2023 UVCCM inaratajiwa kufanya tamasha hilo litakaloshirikisha vijana 2,500 kutoka tarafa nne za Lupilo, Ruaha, Mwaya na Vigoi na kutakuwa na matukio mbalimbali yakiambatana na maandamano ya amani, kufanya usafi hospitali ya wilaya, Gereza la Mahenge kuonana na vijana ambao wako katika kupata elimu ya kutofanya makosa uraiani kwa kuwapatia mahitaji kadhaa, pamoja na kutoa msaada wa watoto yatima Ukwama.
Katibu wa UVCCM wilaya Rukia Makoja alisema umoja huo unakila sababu ya kujivunia miradi ya maendeleo inayofanyika nchini kam ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, pamoja na shule za msingi na sekondari.
Mwenyekti wa UVCCM Ulanga, Shaista Kuyela amesema kwenye tamasha hiyo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi.