Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushirikiano wa sekta binafsi, jamii kuboresha mazingira

Muktasari:

  • Wito wa kuimarishwa kwa sera zinazounga mkono jitihada kama hizo za kulinda mazingira

Dar es Salaam. Kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL), kwa kushirikiana na PETPRO, wameandaa warsha ya kitaifa yenye lengo la kuimarisha mbinu endelevu za udhibiti wa taka na kukuza uchumi wa mduara hapa nchini.

Warsha hiyo inayoongozwa na kauli mbiu ya: “Njia endelevu ya udhibiti wa taka,” imewakutanisha wadau wakuu kutoka serikalini, sekta binafsi na mashirika ya kijamii kwa lengo la kurahisisha safari ya Tanzania kuelekea mustakabali usio na taka.

Akizungumza wakati wa mjadala huo leo Jumapili Juni 8, 2025, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na uhusiano wa TBL, Neema Temba amesisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika kulinda mazingira.

“TBL tunaamini kuwa ukuaji wa viwanda unapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji katika suala zima la mazingira. Shughuli zetu zinaongozwa na mfumo madhubuti wa usimamizi wa taka unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa,” amesema.

Hata hivyo, Temba amesema TBL inafuata sheria na imejikita katika kuongoza mabadiliko kupitia uwekezaji katika urejeleaji, elimu ya mazingira, na ushirikiano na wadau mbalimbali wa mazingira nchini.

Mwakilishi wa PETPRO, Nicholaus Jackson ameupongeza uongozi wa TBL huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kuyatunza.

“Warsha hii ni mfano halisi wa jinsi sekta binafsi zinavyoweza kuongoza mjadala kuhusu uendelevu wa mazingira. PETPRO inajivunia kushirikiana na TBL kuunda mifumo ya urejeleaji wa vifungashio inayoweza kuigwa, kuongeza viwango vya urejeleaji na kuchochea mabadiliko ya kimfumo katika sekta mbalimbali.”

Hata hivyo, mwakilishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Bonifas Kyaruzi ametoa wito wa kuimarishwa kwa sera zinazounga mkono jitihada kama hizo za kulinda mazingira.

“Ushiriki wa kampuni kama TBL unaonesha mwelekeo chanya wa sekta binafsi katika kuchukua wajibu wa mazingira. NEMC tutaendelea kutoa muongozo wa sera na kuboresha mazingira ya kisheria ili kuchochea mzunguko wa uchumi na uvumbuzi wa kijani,” amesema.

Warsha hiyo imejikita kwenye mikakati ya vitendo vya kupunguza taka za viwandani, kuboresha mifumo ya urejeleaji na kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania yanakwenda sambamba na malengo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira.