Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matarajio ya Watanzania bajeti ya Serikali

Muktasari:

  • Alhamisi ya Juni 12, 2025, bajeti za Serikali za nchi za Afrika Mashariki zitawasilishwa. Nchini Tanzania, wadau mbalimbali wamezungumzia kile wanachotarajia kwenye bajeti hiyo itakayosomwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba

Dar/mikoani. Wakati wiki hii Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26 itasomwa bungeni jijini Dodoma, wadau wa kada mbalimbali wameonyesha matarajio yao huku wengi wakitabiri itajikita zaidi kwenye kugharimia uchaguzi.

Sambamba na masuala ya uchaguzi, kutokana na mwaka huu kuwa wa Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, baadhi ya wadau na wananchi wamependekeza uwekezaji katika sekta muhimu ikiwemo kilimo, elimu na afya.

Kubanwa kwa matumizi ya Serikali, ni jambo lingine lililoibuliwa na wadau inapokwenda kusomwa bajeti ya Serikali katika kipindi cha mwaka huo wa fedha wa mwisho wa Serikali ya awamu ya sita.

Bajeti kuu itasomwa Alhamisi Juni 12, 2025 na kabla ilitanguliwa na bajeti za wizara mbalimbali zilizohitimishwa Juni 4, 2025.

Machi 11, 2025, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliwasilisha bungeni, Mapendekezo ya Mfumo na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/2026 kwenye Kamati ya Bunge zima jijini Dodoma.

Katika uwasilishaji huo, Dk Mwigulu alisema Serikali imependekeza kukusanya na kutumia jumla ya Sh57.04 trilioni kwa mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 13.4 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha, 2024/25 ya Sh50.29 trilioni.

Bajeti kuu itakuwa ni ya mwisho kujadiliwa na kupitishwa katika Bunge la 12, kabla ya kuvunjwa Juni 27, 2025 na kuelekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

Matarajio ya wachumi

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo amesema kwa mwaka huu Watanzania watarajie bajeti itakayojielekeza zaidi katika masuala ya uchaguzi na kukamilisha utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Kwa hiyo uchaguzi utachukua sehemu kubwa sio vitendea kazi tu bali na yanayozunguka, usalama, utulivu na ukiachilia hilo bado kuna miradi ya kimkakati inaendelea, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR),” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Kinyondo, kwa maana nyingine ni bajeti ya kumalizia ahadi za ilani ya uchaguzi ili Serikali inapokwenda katika uchaguzi isimame na kusema iliahidi na kutekeleza.

“Kimsingi mambo makubwa na yale tunayoona katika ilani ya uchaguzi ya mwaka huu inaahidi kama Katiba mpya na kadhalika hivyo ni vitu ambavyo vitakuja kwenye mwaka wa fedha utakaokuja,” amesema.

Mhadhiri na Mchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema kwenye kupanga mipango huwa Tanzania inajitahidi kufanya vizuri lakini bado kuna umuhimu wa kuangalia utekelezaji.

"Hatua ya utekelezaji inatakiwa kuangaliwa kwa maana ya umakini ili vilivyopangwa vitekelezwe na kuangalia vyanzo vya fedha vilivyopo, unaweza kupanga lakini ukakosa vyanzo vya fedha za kutekeleza,” amesema.

Dk Mwinuka amesema kuna umuhimu pia wa kuangalia vyanzo vya fedha nafuu na si mzigo kwa Taifa. Akimaanisha kama ni mikopo kwa maana kama mikopo iwe nafuu na kupunguza mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa.

Kwa upande wa sekta ya afya, amesema matarajio ni kuona jinsi Serikali ilivyojipanga kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inayolenga kuwezesha wananchi wote kupata huduma za afya.

"Vyanzo vya mapato vinatajwa kuwa ni ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, kodi za michezo ya kubahatisha, ada za bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kieletroniki," amesema.

Mtazamo wa kiafya

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha watoa huduma za afya Tanzania (Aphfta), Dk Samwel Ogillo amesema matarajio yao ni kuona Bajeti Kuu ya Serikali iweze kuleta unafuu kwa sekta binafsi ili iweze kuwekeza zaidi katika sekta ya afya, kwa lengo la kuwahudumia hawa watakaoongezeka baada ya kupata bima.

Amesema ni tabia ya binadamu akiwa na bima anatafuta huduma za afya, hivyo sekta binafsi inatakiwa kuwekeza zaidi katika kuongeza hospitali maeneo mbalimbali, iweze kuwahudumia watakaokuwa wameongezeka baada ya kupata bima.

Dk Ogillo amesema bajeti ya afya ina mwelekeo mzuri, kwani mpango wa afya kwa wote umeonyesha mwelekeo umeonekana wazi kabisa, ingawaje bado kuna wasiwasi kutokana na uchumi wa nchi kuwa chini bado rasilimali za nchi hazitoshi kuendesha kikamilifu.

“Tunaamini angalau itakapokuja Bajeti Kuu, itakuwa na maono ya kuhakikisha angalau kuwe na fedha fulani itakayoelekezwa moja kwa moja kutekeleza mpango wa afya kwa wote, lakini kilio cha wananchi maskini watanufaika vipi?,” amesema.

Dk Ogillo amesema wanatarajia bajeti ionyesha ule mpango unatekelezeka:“Wakishakuwa na bima ya afya wengi hutafuta matibabu wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji wataenda hospitali, watu wakiongezeka hospitali hazitatosha.”

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema bajeti ya wizara imepitishwa kwa Sh1.61 trilioni, hivyo matarajio itaweza kusaidia utoaji wa huduma na uendelevu wake hasa zilizotolewa chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

“Tunatarajia bajeti hii itaweza kutengeneza ustahimilivu wa kuwa na uwezo wa kuagiza vitu vyetu wenyewe na kuagiza zile dawa za ARV, kifua kikuu na malaria.

“Utasaidia jitihada za utekelezaji wa huduma zinazosaidia bima ya afya kwa wote, matarajio yetu tusikie Bajeti Kuu ikitamka hili pia pamoja na kuajiri wafanyakazi. Tunategemea vile vipaumbele vyetu 10 vitatekelezeka na bajeti hii,” amesema.

Hata hivyo, Dk Mugisha amesema wasiwasi wa wengi kila mwaka Serikali haitimizi bajeti kwenye vituo vya utoaji huduma.

Amesema utekelezaji kwa miaka ya nyuma umekua kati ya asilimia 60 mpaka 70 hakuna wakati bajeti ilifikia asilimia 100, ingawaje kuna sababu hutajwa ikiwemo matarajio kushindwa kufikiwa.

Dk Mugisha ameshauri mifumo iwekwe sawa na kisha itumike kama walivyoweka chama cha madaktari na wengine wanaohamasisha huduma za afya nchini, kwani wanatamani kuona afya za Watanzania zinaimarika huduma zinapatikana, zikiwa bora na wananchi wanashirikishwa katika kupata hizo huduma.

Matarajio ya wananchi

Kipaumbele katika elimu hasa bila malipo ndicho anachokitarajia, Mwajuma Ramadhani, anayeishi Kisosora jijini Tanga, inapokwenda kusomwa bajeti hiyo mpya.

Sambamba na elimu bila malipo, Mwajuma anaona kuna umuhimu wa uwekezaji katika ukarabati wa samani za shule ziendane na idadi ya wanafunzi, kwani zipo zilizoelemewa.

“Kama inawezekana bajeti iangalie jinsi ya kuweka fungu litakalosaidia kukarabati shule kwa kushirikiana na wananchi, lakini pia kuongeza madawati kwani watoto wanakaa chini baada ya kuwepo ongezeko la wanafunzi kutokana na sera ya elimu bure,” amesema Mwajuma.

Kwa upande wa Robert Kimaro, anayefanya biashara katika soko la Tangamano mkoani Tanga, amesema anatamani kuona bajeti inajielekeza katika kuboresha mazingira ya masoko.

“Kuna baadhi ya wafanyabiashara tumesajiliwa na kutambuliwa na Serikali kuhusu biashara zetu, ila imekuwa ni changamoto kupata mikopo, bajeti iangalie kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutuwekea dirisha maalumu la kuweza kukopa kama vile wanafunzi wa vyuo na baada tunarejesha fedha zao kwa utaratibu utakaowekwa,” amesema Robert.

Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, James Kisemo amesema Watanzania wanatarajia kwa hamu Bajeti Kuu ya Serikali, wakilenga kuona jinsi serikali itakavyoshughulikia changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Tunatarajia kuona mikakati madhubuti ya serikali katika kukabiliana na changamoto za sekta ya afya, hasa baada ya kuondoka kwa baadhi ya wafadhili kama USAID. Matarajio ni kwamba bajeti itaelekeza rasilimali zaidi katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa na dawa muhimu,” amesema Kisemo.

Mkazi wa Nyegezi, jijini Mwanza, Petro Noel amesema anatarajia Serikali itakuja na mpango wa kupanua wigo wa walipa kodi utakaosaidia kuongeza mapato.

"Kwa sasa, wanaolipa kodi kwa uhakiki ni waajiriwa kwenye sekta rasmi wakiwemo waajiriwa serikalini na sekta binafsi huku idadi kubwa ya Watanzania waliojiajiri kwenye sekta isiyo rasmi wakiachwa nje kwenye mfumo wa kodi. Hii inasababisha mzigo wa kodi kwa wachache.

"Kutokana na elimu na ufahamu mdogo wa masuala ya kodi, baadhi ya wafanyabiashara wadogo hujikuta wakitumia sehemu ya mitaji yao kulipia kodi hata kabla ya kufanya biashara na kupata faida. Ni muhimu kodi ilipwe kutoka kwenye faida na siyo mtaji," amependekeza.

Ameshauri Serikali iweke mazingira na mfumo utakaodhibiti mianya ya kukwepa kodi miongoni mwa wafanyabiashara na wawekezaji wenye mitaji mikubwa kwa kuwa baadhi yao hutumia ujanja wa ama kubadilisha majina au kuhamisha umiliki kwa kujiuzia hisa.

"Pia natarajia Serikali itapunguza au kuondoa kabisa kodi na ushuru kwa Watanzania wenye vipato vidogo wakiwemo wafanyabiashara na wachuuzi wadogo kwenye masoko, magulio na minada.

"Wafanya biashara na wachuuzi katika masoko, minada na magulio hutakiwa kulipa ushuru mara tu wanapofikisha bidhaa zao sokoni hata kabla ya kuuza. Hii siyo sawa kwa sababu kundi hili hulazimika kutoka nyumbani wakiwa na fedha ya ushuru bila kujali iwapo watauza bidhaa zao au la," ameongeza.

Mkazi wa Iseni jijini Mwanza, Jasimin Kulwa amesema anatarajia bajeti hiyo itajikita kwenye kuwapunguzia machungu wananchi hasa kuangalia namna ya kufanya bei ya mahitaji muhimu kuwa sawa na kiasi Mtanzania anachoingiza kwa mwezi.

"Sitarajii kuongezewa mzigo, sasa hivi maisha yamepanda sana, mahitaji muhimu yapo juu kulinganisha na pesa tunazoingiza katika kazi zetu...imefikia hatua ukipokea mshahara unaisha wote kwa kulipa madeni. Yaani utasema tunafanyia kazi taasisi za mikopo au wauza maduka mitaani kwetu," amesema.

Revina Costantine mkazi wa Uyole jijini Mbeya, amesema bajeti kubwa ielekezwe upande wa afya, miundombinu ya barabara na maji kwa kuwa ndio maeneo yanayolalamikiwa.

“Gharama za matibabu haswa kwa sisi wa kipato cha chini tunatamani kusikia sehemu ya afya tukipata nafuu, lakini barabara nyingi ni mbovu na huduma ya maji maeneo mengi hakuna” amesema Revina ambaye ni mjasiriamali.

Mbunge wa Viti Maalum, Conchesta Rwamlaza amesema anatarajia bajeti hiyo, itajibu matatizo ya wananchi yakiwemo masuala ya miundombinu ya barabara, elimu, afya na kutazama makundi mengine ya kijamii hasa wazee.

“Tuseme kwamba bajeti iunganishe makundi yote, isiache mtu nyuma ndio mambo mazuri yanapaswa kuwa bajeti. Bajeti imepanda sasa hivi kwa hiyo nina mategemeo kwamba itaweza kukusaidia kujibu,” amesema.

Amesema matarajio ya Watanzania kutoka kwenye bajeti yao ni kuona makundi yote ya kijamii yanashirikishwa katika bajeti na hakuna mtu anayeachwa nyuma.

“Lakini pia kuhakikisha hakuna hii kitu inaitwa mdondoko wa watoto, kuhakikisha anayetakiwa kumaliza darasa la saba, kidato cha nne wanamaliza,” amesema.

Rwamlaza amesema nchi haiwezi kuwekeza katika elimu halafu kuna watoto hawamalizi masomo yao.

Viongozi wa dini

Dk Benson Bagonza, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema hatarajii kuona mabadiliko yoyote kwenye bajeti kama suala la rushwa halitashughulikiwa ipasavyo.

“Sivutiwi na bajeti mpya, hata wangerudisha hii inayoisha nisingepata shida sana, shida yangu kubwa ni kiwango cha rushwa na ubadhirifu wa fedha kimeongezeka, hata ungekuja na bajeti nzuri ya aina gani kama hujashughulikia masuala ya rushwa haiwezi kuwa na tija.

“Watu wanakula fedha za umma kama hawana akili nzuri. Hakuna muujiza zaidi ya kushughulika na rushwa natamani kuona viongozi wote wanakemea rushwa, sasa hivi rushwa inawakemea viongozi. Chanzo cha haya ni kukosekana kwa utawala bora, utawala unapaswa uwajibike kwa wananchi tofauti na ilivyo sasa” amesema Bagonza.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema anatarajia bajeti itakayoangazia maeneo muhimu ikiwemo kukamilisha mchakato wa bima ya afya kwa wote ili kuleta nafuu kwa Watanzania wasiomudu gharama za matibabu.

Eneo lingine alilotaka liangaliwe ni bei ya mafuta ya taa kwa kile alichoeleza bidhaa hiyo bado inategemewa na familia duni.

Pia, ametaka Serikali iweke nguvu kwenye kufanya sensa ya wafanyabiashara na wamiliki wa rasilimali zinazopaswa kulipiwa kodi ili kupanua wigo wa walipa kodi nchini.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Boay mkoani Manyara, Elieth Mtaita amesema kinachopaswa kuangaziwa kwenye bajeti hiyo ni kubana matumizi hasa kwenye mambo yasiyohusisha maendeleo.

"Misururu ya magari ya viongozi ipunguzwe na fedha iongezwe kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara, miradi ya maji kwa wananchi, dawa na vifaatiba vipelekwe hospitalini.

Tumeona wabunge wakipendekeza watu wakatwe fedha kwenye simu, kwa nini tusiangalie posho za wabunge na hata mishahara yao ipunguzwe ili kuwaletea wananchi huduma kwa sababu hao wabunge wanawatumikia wananchi," amesema.

Mchungaji huyo amesema sekta za huduma za jamii ziongezewe bajeti tofauti na sasa, kwani ndio njia ya kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwalimu Samson Sombi wa mkoani Morogoro amesema mara nyingi unapokuwa mwaka wa uchaguzi fedha nyingi zinaelekezwa kwenye uchaguzi lakini ni muhimu sekta ya elimu iangaliwe kwa kina.

"Tuna mitaala mipya ambayo inahitaji utekelezaji, lazima kutenga fedha za kuajiri walimu na kuwapa semina ya namna ya kutekeleza mitaala hii, lazima kununua vifaa vitakavyoendana na mitaala mipya pamoja na kuboresha mazingira ya ujifunzaji," amesema.

Mwalimu Sombi amesema kwa kuwa nchi inategemea wakulima na wafugaji ni muhimu kukuza uchumi wao kwa kuwaboreshea mazingira ya kilimo na ufugaji.

“Hayo yakifanika wakulima watalima kilimo chenye tija  na kuondokana na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.”