Maeneo ya kipaumbele Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman akiwasilisha Bajeti ya wizara hiyo barazani Chukwani Unguja Zanzibar
Muktasari:
- Katika vipaumbele hivyo, watawapatia wajasiriamali elimu, uelewa na ufahamu zaidi kuhusiana na fursa za uchumi wa buluu ili kukuza ubunifu, uwezo wa kupata zana za ujasiriamali, uongezaji wa thamani wa mazao ya baharini, kuchangia katika sekta ya uvuvi, uhifadhi wa bahari, utafiti wa uvuvi na bahari, biashara za baharini.
Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imepanga kutekeleza vipaumbele 12 katika mwaka wa fedha 2025/26 ambavyo vitajikita katika mbinu, nyenzo, mitaji na utafutaji wa masoko kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.
Katika vipaumbele hivyo, watawapatia wajasiriamali elimu, uelewa na ufahamu zaidi kuhusiana na fursa za uchumi wa buluu ili kukuza ubunifu, uwezo wa kupata zana za ujasiriamali, uongezaji wa thamani wa mazao ya baharini, kuchangia katika sekta ya uvuvi, mazao ya baharini, mwani, uhifadhi wa bahari, utafiti wa uvuvi na bahari, biashara za baharini.
Pia wizara hiyo itatekeleza miradi 10 ya maendeleo ambayo ni kujenga viwanda na bandari za uchumi wa buluu.
Akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Juni 2, 2025 barazani, Waziri wa wizara huyo, Shaaban Ali Othman ameliomba baraza kuidhinisha Sh172 bilioni, kati ya fedha hizo Sh157 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo Sh131.245 bilioni zinatoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Sh25.836 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo, ambapo Sh23.138 bilioni ni mkopo na Sh2.698 bilioni ni ruzuku.
Akitaja vipaumbele hivyo Shaaban amesema ni utoaji wa elimu na uelewa katika masuala ya uchumi wa buluu ikiwemo mbinu, nyenzo, mitaji na utafutaji wa masoko kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.
Uwezeshaji na uwekezaji katika uvuvi endelevu wa mwambao na bahari kuu na uwezeshaji na uwekezaji katika kilimo cha mwani.
Waziri Shaaban amesema kuna mafanikio makubwa katika sekta hiyo, uzalishaji wa zao la mwani umeongezeka kwa asilimia 124.6 kutoka tani 8,785 zenye thamani ya Sh5.387 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia tani 19,716 zenye thamani ya Sh16.14 mwaka 2024.
“Uwezeshaji na uwekezaji katika ufugaji wa viumbe maji, majongoo bahari, kaa na samaki na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na nishati mbadala za baharini, ujenzi wa miundombinu ya uhifadhi pamoja na biashara ya mafuta na gesi,” amesema
Pia amesema watajikita ujenzi wa miundombinu ya bandari za uvuvi, madiko, masoko, viwanda, huduma na biashara za uchumi wa mazao ya baharini.
Amesema kiwango cha uzalishaji wa samaki kimeongezeka kwa asilimia 107.2 kutoka tani 38,107 zenye thamani ya Sh205.35 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia tani 78,943 zenye thamani ya Sh618.18 bilioni mwaka 2024.
Hivyo, mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 5.7 mwaka 2024 kwa mujibu Ofisi ya mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Pia sekta ya uvuvi imekua kwa asilimia 14.2 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2023. Ongezeko hili linatokana na hatua mbalimbali za serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi.
Waziri amesema katika kipindi cha mwaka 2025/26 utafiti wa uvuvi, sayansi za bahari, maliasili za bahari, mazingira na mabadiliko ya tabianchi baharini na kuhifadhi wa maeneo ya bahari (matumbawe, nyasi bahari, mikoko na bioanuwai ya baharini).
Kipaumbele kingine ni usimamizi wa bahari kwa kupambana na uvuvi haramu na kuweka misingi imara na kuimarisha utekelezaji wa bajeti inayozingatia jinsia na watu wenye mahitaji maalumu.
Pamoja na vipaumbele hivyo, amesema wizara itatekeleza miradi 10 yenye thamani ya Sh157.081 bilioni ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari ya uvuvi Shumba na ujenzi wa viwanda vya kuchakata na uongezaji wa thamani wa mazao ya baharini.
Ametaja mradi wa ujenzi wa masoko ya kisasa ya samaki na kuendeleza kilimo na uvuvi unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), ikiwemo ununuzi wa meli kubwa ya uvuvi wa Bahari Kuu.
“Tutakuwa na mradi wa kukuza usimamizi endelevu wa uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji wa bahari (Tasfam) na mradi jumuishi wa uwezeshaji wa wanawake katika ufugaji wa mazao ya baharini unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Korea (Koica),” amesema
Ametaja mradi wa ujenzi wa kituo cha Taifa cha kuhifadhia taarifa za mafuta na gesi asilia na mradi wa usambazaji wa gesi Zanzibar na utafiti wenye lengo la kudumisha uchumi, usalama wa chakula na maisha endelevu kwa jamii.
Akisoma maoni ya kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo, mjumbe wa kamati hiyo Suleiman Makame Ali ameipongeza wizara kwa kuendeleza sekta ya uvuvi kupitia ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani ya mazao baharini ambapo wanakadiria kutumia Sh51 bilioni
“Kupitia mpango huo viwanda vitakavyojengwa bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa zenye thamani na kuhitajika sokoni na kutumika ndani na nje ya nchi,” amesema