Kamati ya Jafo yafunua kichaka cha Wachina Kariakoo

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo akipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya wataalamu ya kukagua biashara zinazofanywa na raia wa kigeni katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Thabit Massa (kulia), kushoto ni Dk Suleimai Serera na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara hiyo, Sempeho Manungi. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Chabaini wanavyofanya biashara kinyume na sheria majina ya Watanzania 32 yatumika wakati si wamiliki wa biashara husika.
Dar es Salaam. Kikosi Kazi cha utekelezaji cha Kamati ya kuchunguza raia wa kigeni wanaofanya biashara kinyume na sheria Kariakoo, kimebaini uwepo wa raia wa kigeni 183 wanaofanya biashara katika maeneo hayo kinyume na sheria.
Kati ya hao, raia 135 wanatoka China, huku waliobaki wakiwa ni kutoka mataifa mengine –Kenya (5), Misri (2), India (2), Yemen (2), Nigeria (5), Uingereza (2) na Uholanzi (1).
Aidha, Watanzania 32 wamebainika wakifanya kazi kinyume na sheria kwa kusaidia wageni hao.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, Juni 6, 2025 na Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Thabiti Massa, alipokuwa akiwasilisha ripoti kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, kuhusu jukumu walilopewa ya kukagua wageni wanaofanya biashara kinyume na sheria.
Kamati hiyo iliundwa na Waziri Jafo Februari 5, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyetoa maelekezo ya kufanyika kwa uchunguzi ili kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na Watanzania.
Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe 15 ilifanya kazi kwa siku 30, pamoja na mambo mengine, ilikuwa na jukumu la kufuatilia utoaji leseni za biashara kwa wazawa na wageni sambamba na kusajili wafanyabiashara ili kuwa na kanzi data yao.
Baada ya kumaliza kazi yake na kumkabidhi ripoti, Waziri Jafo aliunda kikosi kazi cha kufuatilia na kufanya ukaguzi katika maduka yaliyopo Kariakoo kilichopewa mwezi mmoja kuifanya kazi yake (Mei 5 hadi Mei 30, 2025) na kutoka taarifa hiyo.
Ripoti hiyo imetolea ikiwa takriban mwezo mopja tangu Idara ya Uhamiaji ilipotoa taarifa kuwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama ilifanya ukaguzi maalumu eneo la Kariakoo ambako raia wa kigeni 62 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa na kuondoshwa nchini kwa kosa la kuishi na kufanya biashara bila ya kuwa na vibali na baadhi yao kukiuka masharti yaliyoanishwa katika vibali vyao vya biashara.
Ripoti ya Kikosi kazi
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mwenyekiti wa kikosi kazi, Thabiti Massa amesema miongoni mwa mambo waliyoyabaini ni pamoja na raia 183 wa kigeni kufanya biashara nchini kinyume na sheria, huku 32 kati yao wakiwa Watanzania wanaotumika kama wasimamizi wa biashara hizo.
Akifafanua zaidi, Massa amesema: “Utakuta dukani yupo raia wa kigeni anayefanya kazi, lakini ukienda kwenye usajili wa duka hilo jina lililosajiliwa ni la Mtanzania. Hata hivyo, Mtanzania huyo ukiangalia kwa mwonekano haonekani kuwa na uwezo wa kumiliki duka husika na hata kwenye akaunti yake hana hela yoyote iliyohifadhiwa.”
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa maduka 112 kati ya yale waliyoyakagua yalibainika kutolipa kodi, ambapo 55 tayari yamefikishwa TRA kwa ajili ya makadirio, na kiasi cha zaidi ya Sh milioni 300 kimepatikana.
Kwa upande wa bidhaa zisizokidhi viwango, amesema kampuni 83 zilizokaguliwa, 73 zilikiuka sheria ya viwango.
Kuhusu bidhaa bandia, amesema kati ya kampuni 23 zilizokaguliwa na Tume ya Ushindani (FCC), tisa zilikutwa na bidhaa bandia zikiwemo chupi za wanaume, vesti, mitandio 6,621 pamoja na viatu vya wazi na vya kufunika (jozi 1,692).
“Hata hivyo, kaguzi hizi zote zilizofanyika zimeiwezesha nchi kupata zaidi ya Sh milioni 400, kati ya hizo kodi zikiwa ni Sh milioni 346 na zingine zikitokana na faini mbalimbali,” amesema Massa.
Akichambua hadidu za rejea, Massa amesema kikosi hicho kiliundwa kwa malengo ya kubaini wageni wanaofanya kazi bila vibali pamoja na wafanyabiashara wanaokiuka sheria za kodi.
“Malengo mengine ni kubaini wafanyabiashara wanaouza bidhaa zisizo na viwango na wanaouza bidhaa bandia,” amesema Massa.
Kikosi kazi hicho, mbali na kuundwa na wafanyabiashara, pia kilihusisha taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Idara ya Kazi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wakala wa Usajili wa Biashara na Kampuni (BRELA), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Nje (Tantrade), pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katika mapendekezo yake, Massa amesema kutokana na changamoto walizokutana nazo, kuna haja ya kuwepo kwa sheria mahususi ya biashara, kwani baadhi ya kampuni walizozifungia zimeshaanza kufungua malalamiko zikitaja kuwa hakuna sheria inayozuia wageni kufanya biashara maeneo hayo.
Mapendekezo mengine ni kuongeza juhudi katika kuhakikisha mifumo ya taasisi za serikali inasomana ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa, pamoja na kutoa elimu ya biashara kwa wafanyabiashara wa ndani ili wasiwe rahisi kutumiwa na raia wa kigeni.
“Pia kuna haja ya wafanyabiashara kupewa elimu ya biashara ili kuwawezesha kufanya biashara kwa kufuata sheria za nchi na kuepuka kutumika kufaidisha mataifa mengine,” amesema Massa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amepongeza kazi iliyofanywa na kikosi hicho na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.
Amesema mojawapo ya mapendekezo hayo ni kuandaa sheria ya biashara, na kwamba atajaribu kupeleka muswada huo bungeni kwa hati ya dharura endapo muda utaruhusu, kutokana na Bunge lililopo sasa kuwa la bajeti.
“Nitajitahidi nipeleke sheria hii kwa hati ya dharura kama muda utaruhusu bungeni, kwa kuwa Bunge lililopo sasa si la kupitia miswada, lakini kwa hali ya tathmini mliyoitoa baada ya ukaguzi wenu, naona kuna haja ya kuiharakisha ili ifikapo Julai ianze kutumika,” amesema Jafo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Severine Mushi amepongeza hatua hiyo akisema itasaidia kuimarisha sekta ya biashara na kuhakikisha mapato ya serikali yanapatikana.
“Ilifika mahali hawa wageni wanabadilisha namba ya mfanyabiashara (TIN) kwa lengo la kukwepa kodi na wanapoondoka wanaacha mzigo wa deni kwa wazawa. Ifike mahali wanapotaka kuondoka nchini wapitiwe taarifa zao kama hawana deni, kabla ya kuwaruhusu,” amesema Mushi.
Pia ameshauri kuwa ukaguzi huo uwe endelevu na ushirikishe taasisi zote ili kuwadhibiti wageni wanaofanya biashara kinyume na sheria.
Renatus Mlelwa, mmoja wa wafanyabiashara, amesema hali ya biashara ilikuwa inasababisha wengi kufikiria kurudi vijijini kulima kama Serikali isingechukua hatua, kwa kuwa wageni walikuwa wamehodhi biashara.
“Niipongeze Serikali kwa hatua hii, kwani kwa ilichokifanya walau imeleta dira katika biashara. Msisitizo wetu ni kuwa sheria ziboreshwe ili kudhibiti vitendo hivyo,” amesema Mlelwa.
Naye Martha Mwaijande amesema wanashukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao cha muda mrefu na kwamba ripoti hiyo imeonyesha uhalisia wa malalamiko yao.
Martha amesema endapo ripoti hiyo itatekelezwa, watakuwa katika nafasi nzuri ya kufanya biashara kwa kuwa, hawawezi kushindana na Wachina na hivyo hatua hiyo itawapa mazingira salama.