Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usanifu mbovu wa barabara chanzo cha ajali

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa barabara salama na kuchunguza vyanzo vya ajali kutoka mikoa ya kanda ya ziwa yanayoendeshwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa siku tano jijini Mwanza.

Muktasari:

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), zinaonyesha usanifu duni wa miundombinu ya barabara ni moja ya chanzo cha ajali barabarani

Mwanza. Usanifu mbovu wa miundombinu ya barabara umetajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya ajali zinazotokea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha madhara ikiwamo vifo, ulemavu, uharibifu na upotevu wa mali.

Akizungumza jijini Mwanza leo Jumatatu Machi 25, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ukaguzi wa barabara salama na kuchunguza vyanzo vya ajali, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk Prosper Mgaya amesema utafiti umebaini pamoja na uzembe wa baadhi ya madereva na watumiaji wengine wa barabara, uduni wa miundombinu pia huchangia ajali za barabarani.

“NIT tumefanya utafiti na kubaini kuwa siyo ajali zote za barabarani hutokana na uzembe wa madereva; kuna maeneo  ajali husababishwa na  ama jinsi barabara ilivyosanifiwa au ilivyojengwa,” amesema Dk Mgaya.

Huku akionesha msisitizo, amewaambia wadau wa sekta ya usafirishaji kutokana na utafiti huo, NIT imebaini kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu usafirishaji salama ili kuongeza uelewa wa wananchi na wasimamizi wa sheria za usalama barabarani.

Amesema usalama wa barabara yoyote unaanzia kwenye usanifu na baada ya ujenzi kukamilika, watumiaji na wasimamizi wa sheria za usalama barabarani wanatakiwa kuzisimamia ili kuepusha ajali zinazorudisha nyuma si uchumi wa mtu binafsi tu, bali nchi kwa jumla.

“Mhandisi anaposanifu barabara mbali ya vitu vingine, lakini pia anatakiwa kujiridhisha kama  barabara anayoisanifu itakuwa salama,” amesema Mgaya.

Amesema mara zote watu hutegemea barabara inayojengwa iwe inakuwa salama kwa abiria wanaosafiri na wanaosafirisha mizigo.

Mkuu huyo wa chuo amesema kwa kutambua hilo, mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia yatatolewa kwa wahandisi, wasanifu, askari wa usalama barabarani, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), wasimamizi wa sheria za usalama barabarani na vyama vya usafirishaji ili  kuwajengea uwezo kuzuia ajali zinazozuilika.

Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani mkoani Mara, Mathew Ntakije amekiri baadhi ya ajali kusababishwa na ubovu wa barabara na namna zilivyojengwa akidai mafunzo hayo yatawapa fursa ya kuwasilisha maoni na mawazo yao kwa Tanroads.

Mratibu wa Taasisi ya Kutetea Haki za Abiria Kanda ya Ziwa (Takuha), Hashim Ramadhani amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakidai miundombinu kuwa chanzo cha ajali pindi ikitokea.

“Dereva ukienda kumuhoji anakwambia shida ni barabara, shida ilikuwa ni shimo sikuliona,  sikuona alama ya daraja, kwa hiyo mafunzo haya yatatusaidia kuona upungufu na kuwajulisha wahusika,”amesema Ramadhani.

Mkuu wa Kitengo cha usalama barabarani mkoani Mara, Mathew Ntakije amekiri baadhi ya ajali kusababishwa na ubovu wa barabara na namna zilivyojengwa akidai mafunzo hayo yatawapa fursa ya kuwasilisha maoni na mawazo yao kwa Tanroads.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia vizuri kwenye utendaji kazi wao ili kupunguza kama si kuondoa kabisa ajali za barabarani.