Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Udhibiti ajali Mlima Iwambi bado kitendawili

Malori yakiwa kwenye foleni yakisubiri kuruhusiwa kupita kwenye Mlima Iwambi, Mkoa wa Mbeya

Muktasari:

  • Ili kudhibiti ajali zinazotokea mara kwa mara katika Mlima Iwambi, Wilaya ya Mbeya vijijini Mkoa wa Mbeya, jeshi la polisi limeweka utaratibu wa kupishanisha magari madogo na makubwa.

Mbeya. Licha ya kuwepo kwa utaratibu wa kupita kwa awamu katika Mlima Iwambi ili kudhibiti ajali, utaratibu huo umeonekana bado una changamoto kutokana na kukosekana usimamizi wa askari sehemu ya mteremko.

Utaratibu huo umekuwepo kwa takribani miaka miwili iliyopita, lakini bado ajali zinaendelea kutokea katika eneo hilo zikisababishwa na mwendokasi na uzembe wa madereva.

Mwananchi Digital imeshuhudia magari yakikimbizana yanaporuhusiwa baada ya dakika 30 kumalizika, huku wengine wakiwapita wenzao bila kuchukua tahadhari za kuepuka ajali.

Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo pamoja na madereva waliozungumza na Mwananchi wamesema utaratibu huo bado una changamoto, kwani kumekuwa na ajali zinazotokea mara kwa mara.

Neema Mwakitalima, mkazi wa Mbalizi, amesema kuna haja ya kuwepo askari wa barabarani eneo hilo, ili kuzuia magari yanayofanya vurugu yanapofika katikati ya mlima.

“Unakuta dereva amefika katikati, haoni trafiki anawapita wenzake bila kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha ajali,” amesema Neema.

Kwa upande wake, Ayubu Mwakifuna, dereva wa daladala ya Mbalizi kwenda Nsalaga amesema magari yanaporuhusiwa hususani madogo yamekuwa na vurugu, kwani kila mmoja anakuwa na haraka.

“Hapa tunakaa muda mrefu karibu dakika 30, ili kwenda na muda tunajikuta tunakimbizana hadi kusababisha ajali na wengine wana overtake sehemu isiyo sahihi,” amesema Mwakifuna.

Lameck Zabron, dereva wa lori linalofanya safari zake nje ya nchi, amesema jambo lililofanyika ni zuri, lakini linawapa wakati mgumu wanapofika katikati kwani yapo malori ambayo hayana nguvu ya kupanda mlima.

“Kwenye kushuka magari yanafeli breki na wakati wa kupanda yanakuwa kwenye mwendo wa taratibu, hivyo zamu ya magari madogo yanakutana na lori njiani kama si kugongana, basi mojawapo litapoteza muelekeo wa njia,” amesema Zabron.

Akizungumzia jambo hilo, Kamanda wa Usalama barabarani mkoa wa Mbeya, Hussein Gawile amesema kutokana na changamoto hiyo waliamua kuweka kibanda cha polisi mita chache kabla ya kuteremka mlima kwa jili ya kuangalia wanaovunja sheria za usalama barabarani.

“Tumeweka askari na kamera kwa ajili ya kupiga picha wale wote wanaokiuka sheria, hivyo wanavyoshuka au kupandisha watakamatwa na askari atakayekuwepo,” amesema Gawile.

Pia, amekiri kuwa hakuna doria inayofanyika katika eneo ambalo hakuna askari na kamera, hivyo watafanyia kazi jambo hilo, ili kuendelea kudhibiti madereva wazembe na wasiofuata sheria.

Septemba 22, 2023, katika Mlima Iwambi ilitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu tisa na majeruhi 23, baada ya dereva wa lori kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko mkali na kwenda kuligonga kwa nyuma gari ya abiria aina ya Coaster.

Kutokana na kuwepo kwa ajali katika eneo hilo na ufinyu wa barabara, Serikali imeanza upanuzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa mkoani Mbeya hadi Tunduma mkoani Songwe yenye urefu wa kilomita 218 utakaogharimu Sh1.33 trilioni.

Akizungumzia ujenzi wa barabara katika mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema wamepokea fedha kutoka Serikali Kuu zaidi ya Sh 1.402 trilioni katika miradi ya barabara, hivyo miongoni mwa maeneo yatakayofikiwa ni barabara kuu ya Tanzam itakayogharimu zaidi ya Sh138 bilioni.

“Kutokana na changamoto iliyokuwapo Mlima Iwambi kwa ajali za mara kwa mara itabaki historia pale mradi huu utakapokamilika, kwani mkandarasi yupo kazini,” amesema Homera.