RPC Iringa: Ajali ya basi Mlima Kitonga hakuna majeruhi, kifo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi
Muktasari:
- Ajali iliyotokea Mlima Kitonga, abiria wote wako salama na hakuna majeruhi
Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema abiria wote wako salama na hakuna majeruhi yeyote katika ajali iliyotokea eneo la Mlima Kitonga kufuatia basi la Kampuni ya New Force kupinduka na kulalia upande mmoja.
Tukio hilo lilotokea saa 3:30 asubuhi leo Julai 2, 2023 ambapo basi hilo aina ya Yutong lilikuwa limebeba abiria 57 likitokea mkoani Iringa kuelekea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda Bukumbi amesema basi hilo lilipinduka na kuegama pembezoni mwa barabara wakati dereva akiyapita mabasi mengine yaliyokuwa yanateremka katika mlima huo yakiwa kwenye foleni.
“Watu wote wako salama na hakuna majeruhi yeyote na hakuna mali nyingine zilizoharibika na kinachofuata tunapima ajali na kuchukua hatua stahiki kwa dereva huyu na mmiliki kuja kuondoa gari lake eneo la tukio,”amesema
Kamanda amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kwa kung’ang’ania kupita mazingira ambayo hakutakiwa kupita huku akijua eneo hilo kuna mteremko mkali na magari yanapita kwa foleni.
“Kushindwa kulimudu basi hilo na kupanda gema na hatimaye basi hilo kulala pembezoni mwa barabara na chanzo ni uzembe wa dereva kung’ang’ania kupita mazingira ambayo hakutakiwa kufanya hivyo,”amesema
Kamanda huyo amesema kikubwa kinachofuata kwa sasa ni kuhakikisha abiria wanapata msaada wa gari nyingine waweze kuendelea na safari yao kwenda mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha Kamanda Bukumbi ametoa wito kwa kuwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani kwani kufanya hivyo ni kujihami na kujenga weledi katika kutekeleza majukumu yao.
“Siyo rahisi sisi polisi kusimama kila kona kwani kuna maeneo mengi tunafanya kazi,”amesema.