Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujasi yasheheni wajasiriamali Udom

Sehemu ya eneo la Ujasi lililopo Mtaa wa Ng'hong’hona mkoani Dodoma. Picha na Merciful Munuo.

Muktasari:

  • Wahitimu, wanafunzi Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wachangamkia fursa za ujasiriamali.

Dodoma. Eneo la Ujasi, likiwa ni kifupisho cha ujasiriamali ni maarufu katika Mtaa wa Ng’hong’hona ulio jirani na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Ni eneo lenye wafanyabiashara 60O, wengi wakiwa wajasiriamali wanawake. Baadhi yao wakiwamo wanafunzi walio masomoni na wahitimu wa Udom.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa mawasiliano na masoko wa Udom, Rose Joseph amesema hana ushahidi wa kutosha kuhusu wanafunzi chuoni hapo kujihusisha na biashara katika eneo hilo.

Amesema Udom ina zaidi ya wanafunzi 35,000 hivyo kumfuatilia kila mmoja na kujua anafanya nini ni suala gumu.

Amesema kila mwanafunzi ni lazima azingatie masomo kama sheria za chuo zinavyotaka.

“Mtu anaweza kusema kuwa ni mwanafunzi wa Udom kumbe si kweli ni lazima tumfuatilie tuone kama kweli ana kitambulisho chetu ndiyo tuamini, maana kila mtu siku hizi anajitambulisha kuwa ni mwanafunzi wetu ili aweze kufanya biashara,” amesema Rose.

Wateja katika eneo hili kwa asilimia kubwa ni wanafunzi wa Udom ambao huenda kupata mahitaji ya kila siku, hivyo kupunguza safari za kwenda mjini.

Ukifika eneo hili, utakumbana na shughuli kadhaa zikiendelea.

Kuna vibanda vya biashara, maduka ya bidhaa mbalimbali, wachuuzi wa petroli kwenye vidumu, mafundi viatu, saluni za kike na za kiume, taasisi za mikopo na shughuli zingine ambazo kwa asili hufanyika sokoni.

Mwenyekiti wa eneo hilo, Odilo Mwambigija amesema lina jumla ya watu 1,000, kati ya hao wafanyabiashara ni 600, huku wengine waliosalia ni wasaidizi wao wa kazi.

Amesema kati ya hao wapo wafanyabiashara wa maduka 420, huku wenye vibanda vya vyakula na mamalishe wakiwa 68.

Amesema baadhi ya wahitimu wa Udom waliamua kubaki Dodoma ili kutumia fursa ya ujasiriamali iliyopo eneo hilo na kujiajiri.

Mwambigija amesema asilimia kubwa ya wafanyabishara wamepanga kwenye majengo ya wenyeji katika mtaa huo, hivyo huwalipa kodi wamiliki na Serikali.

Amesema asilimia kubwa ya wateja ni wanafunzi wa Udom na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Kutokana na hilo, amesema chuo kikifungwa biashara nyingi pia hufungwa kusubiri kifunguliwe.

“Bei ya bidhaa zinazopatikana hapa ni za kawaida tofauti na maeneo ya ndani ya chuo, pia zipo ambazo hazipatikani humo hivyo wanafunzi huja kununua huku,” amesema.

“Hapa tuna kila kitu, hata kama unataka kuagiza gari tuna madalali wanafanya kazi hiyo na magari yanafika bila shida yoyote,” amesema Mwambigija.

Amebainisha biashara katika eneo hilo ni nzuri kwani wanahudumia chuo chenye idadi kubwa ya wanafunzi.

Baadhi ya wahitimu wa Udom waliozungumza na Mwananchi Digital wanasema maisha ya ujasiriamali katika eneo hilo ni bora kuliko kusubiri ajira serikalini, ambazo si za kuaminika.

Michael Njau, aliyehitimu chuoni hapo mwaka 2016 masomo ya Shahada ya kwanza ya Elimu katika Utawala amesema alianza biashara eneo hilo tangu akiwa mwaka wa pili wa masomo.

Amesema biashara anayofanya ni ya mazao anayoyatoa mikoani na kuyauza.

Kwa biashara hiyo amesema amejenga nyumba na kusomesha watoto wake watatu shule  binafsi, huku akiwalipia ada bila shida yoyote.

Njau amesema hafikirii kuajiriwa kwa sababu kama ni suala la kupata pesa anapata zaidi ya mtu aliyeajiriwa.

“Nimeanza biashara tangu nikiwa mwaka wa pili wa masomo 2013, baada ya kuona fursa hii, niliamua kumleta mke wangu na kufungua duka hili. Baada ya kumaliza masomo nilijiunga naye mpaka leo tunaendesha maisha yetu, sina ninachokosa,” amesema Njau.

Mkomolwa Oswald, anayeuza nyama ya nguruwe anasema alihitimu chuoni hapo mwaka 2015 kozi ya Shahada ya kwanza ya Elimu na Tehama.

Anasema alianza biashara mwaka 2013 kwa kutumia fedha za ‘boom’ alizokuwa anazipata kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB).

Anasema baada ya kuhitimu aliamua kujikita zaidi kwenye biashara kwa kuwa aliomba ajira serikalini mara moja akakosa. Amesema hajawahi kuomba tena.

"Nimemaliza chuo zaidi ya miaka minane hata nikiomba ajira nitakuwa sikumbuki nilichojifunza labda wanirudishe kwenye crash program (mafunzo ya kujengewa uwezo), maana nimeshasahau kila kitu," amesema Oswald.

Wafanyabiashara wengine ni wanafunzi wanaoendelea na masomo Udom ambao hutumia muda wao wa ziada kufanya biashara.

Emma Fwande, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesoma kozi ya Shahada ya kwanza ya Uongozi (BED ADEC) amefungua saluni.

Anasema hufanya kazi akiwa hana vipindi darasani.

Emma amesema fedha alizotumia kufungua biashara hiyo zilitokana na ‘boom’ ambapo anafanyia biashara ili aendelee kuishi akiwa chuoni.

Amesema biashara ni nzuri kwa kuwa kwa siku hakosi Sh30,000 ambayo akitoa mahitaji anabaki na fedha kidogo, ambapo  kwa mwezi hupata faida ya wastani wa Sh70,000.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya kwanza katika kozi ya Sayansi ya Hisabati, Nombo Aloyce amesema amefungua ofisi ya kukarabati vifaa vya umeme vilivyoharibika na kuungua kwa kuwa ana utaalamu huo tangu akisoma kidato cha tano na cha sita.

Amesema biashara hiyo humwingizia kipato kikubwa kwa kuwa vifaa vingine vikiungua huwa anavitengeneza hadi kwa Sh70,000 kiasi ambacho ni kikubwa sana kwake.


Changamoto

Wakizungumzia changamoto zilizopo kwenye eneo hilo, wafanyabiashara hao wamesema bado kuna tatizo la uondoshaji wa takataka.

Manka Kileo, ambaye ni mamalishe amesema huwa zinakaa muda mrefu bila kuondoshwa hivyo kuhatarisha afya za watu.

Mbali ya hilo, ameiomba Serikali kutengeneza miundombinu hasa barabara na huduma za kijamii kama vile maji ambayo hayatoki, wakitumia ya visima.

Manka amesema wanatumia maji mengi kufanya shughuli zao, hivyo wanahitaji huduma nzuri ya maji angalau mara mbili kwa wiki.

Amesema wateja wao wengi ni wanafunzi wa Udom, hivyo kama hakutakuwa na huduma endelevu ya maji katika eneo hilo kuna hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Isack Mpali amekiri kuwapo changamoto ya mindombinu ya barabara na maji, akisema visima vinavyotumika ni vya watu binafsi.

Ili kutatua changamoto hiyo, amewaomba watu binafsi kuchimba visima viweze kuwasaidia wafanyabiashara hao kuendesha  shughuli zao.

kuhusu barabara, amesema kuna ujenzi wa daraja linalounganisha eneo hilo na Mtaa wa Ng'hongh'ona unaendelea ambao ukikamilika itafikia mpaka Hospitali ya Benjamin Mkapa.

"Barabara ikikamilika itakuwa kiunganishi kati ya eneo la Ujasi, Mtaa wa Ng'hongh'ona na Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa sababu zinatenganishwa na korongo. Tumeshaanza kuliweka daraja la kudumu," amesema.