Mahiga awataka wahitimu Udom kuwa wajasiriamali

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Augustine Mahiga.
Muktasari:
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Augustine Mahiga amewataka wahitimu wa chuo hicho kujiongezea elimu ya ufundi na ujuzi katika fani mbalimbali, ili kuwa na fursa za ajira na kupanua wigo wa ujasiriamali.
Dodoma. Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Augustine Mahiga amewataka wahitimu wa chuo hicho kujiongezea elimu ya ufundi na ujuzi katika fani mbalimbali, ili kuwa na fursa za ajira na kupanua wigo wa ujasiriamali.
Balozi Mahiga alitoa kauli hiyo jana, kwenye mahafali ya sita ya Udom yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga chuoni hapo.
Aliwapongeza wahitimu wote kwa kufanya vizuri zaidi na kupata shahada zenye sifa bora zaidi ya wengine, lakini akawaambia kuwa ubora wakati mwingine si kielelezo katika utendaji na wala siyo mwisho wa elimu.
Pia, aliwasihi wanafunzi waliojiunga na chuo hicho mwaka huu wa masomo kutumia fursa nyingi za kisheria kujadili masuala yanayowakwaza na kuboresha mazingira yao ya masomo na makazi.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema wahitimu 4,136 walihitimu katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwamo vyeti, stashahada, shahada, shahada za uzamili na shahada za uzamivu. Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alijivunia mafanikio yaliyofikiwa tangu chuo hicho kwa kusimamia misingi ya taaluma.