Makardinali kupanga tarehe kumchagua Papa mpya leo

Muktasari:
- Hadi sasa, kuna dalili chache zinazoashiria ni nani anaweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya.
Vatican City. Baada ya mazishi ya Baba Mtakatifu, Papa Francis yaliyofanyika Jumamosi Aprili 26, 2025, shughuli ndani ya Vatican zimeendelea na sasa mchakato wa kumchagua Papa mpya umeanza.
Leo Jumatatu Aprili 28, 2025 makardinali wanatarajiwa kukutana kupanga tarehe ya kuanza kwa mkutano wa kumchagua Papa mpya atakayekuwa kiongozi wa waumini zaidi ya bilioni 1.4 wa Kanisa Katoliki duniani, kufuatia kifo cha Papa Francis.
Makardinali hao wanaojulikana kama ‘Wafalme wa Kanisa’ kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekusanyika mjini Vatican tangu Papa Francis, raia wa Argentina aliyekuwa na umri wa miaka 88, alipofariki dunia Aprili 21, 2025.

Hadi sasa, kuna dalili ndogo zinazoashiria ni nani anaweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya.
"Naamini kama Francis alikuwa Papa wa mshangao, basi hata mkutano huu wa uchaguzi hautabiriki kwa namna yoyote," amesema Kardinali wa Hispania, Jose Cobo, katika mahojiano aliyofanya jana na Shirika la Habari la Marekani, AP.
Katika mikutano iliyopita ya uchaguzi, "ungeweza kubashiri mwelekeo wa mambo," aliliambia gazeti la Hispania, 'El Pais', lakini safari hii makardinali wengi wanatoka nje ya Ulaya na hata hawajawahi kukutana ana kwa ana.
Papa Francis alizikwa Jumamosi katika ibada iliyohudhuriwa na watu wapatao 400,000 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na maeneo jirani, zikiwamo familia za kifalme, viongozi wa dunia na mahujaji wa kawaida.
Hali kadhalika, umati mkubwa wa watu ulikusanyika jana Jumapili katika Kanisa la Santa Maria Maggiore mjini Roma kutembelea kaburi lake la marumaru, baada ya ‘Papa wa wanyonge’ kuamua kuzikwa nje ya kuta za Vatican.
Katika kipindi hiki ambapo dunia inakumbwa na migogoro na misukosuko ya kidiplomasia, Kardinali wa Italia Pietro Parolin, ambaye alikuwa Katibu wa Jimbo chini ya Papa Francis, yaani msaidizi wake mkuu anatabiriwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa kurithi kiti hicho.

Kardinali wa Italia, Pietro Parolin.
Kampuni ya ubashiri ya William Hill ya Uingereza imemweka mbele kidogo Parolin, akifuatiwa na Luis Antonio Tagle kutoka Ufilipino, Askofu Mkuu mstaafu wa Manila, na kisha Kardinali Peter Turkson kutoka Ghana.
Wengine wanaofuatia kwenye orodha yao ni Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, Kardinali Robert Sarah wa Guinea na Matteo Zuppi, Askofu Mkuu wa Bologna.
‘Papa sahihi’
Ricardo Cruz, 44, mtaalamu wa data na 'akili mnemba' aliyekwenda kutembelea kaburi la Francis jana Jumapili, amesema akiwa Mfilipino, angefurahi kuona Papa mpya akitoka bara la Asia, lakini kama Mkatoliki, anatamani tu makardinali wamchague ‘Papa sahihi."’.
Ingawa juhudi za Papa Francis kulifanya Kanisa kuwa na huruma zaidi zilimletea mapenzi na heshima kubwa, baadhi ya mageuzi yake yaliwakera wahafidhina ndani ya Kanisa, hasa nchini Marekani na barani Afrika.
Profesa Roberto Regoli, mtaalamu wa historia na utamaduni wa Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian mjini Roma, aliiambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa makardinali watahitaji "kumpata mtu atakayejenga umoja mkubwa zaidi."
"Tupo katika kipindi ambacho Ukristo wa Kikatoliki unakabiliwa na migawanyiko mbalimbali, hivyo sidhani kuwa uchaguzi huu utakuwa wa haraka sana," amesema.

Mtaalamu wa historia na utamaduni wa Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian mjini Roma, Profesa Roberto Regoli
Makardinali wamekuwa wakifanya vikao vya jumla tangu kifo cha Francis kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi na masuala ya baadaye.
Leo Jumatatu makardinali walitarajiwa kufanya kikao cha tano ambapo watapanga tarehe rasmi ya kuanza kwa mkutano wa kumchagua papa (conclave).
Wataalamu wanasema huenda mkutano huo ukaanza Mei 5 au 6 baada ya kumalizika kwa siku tisa za maombolezo ya Papa hapo Mei 4, 2025.
Mpaka sasa, hali ya vikao imeelezewa kuwa ya "wazi sana," kwa mujibu wa Kardinali Giuseppe Versaldi wa Italia aliyezungumza na gazeti 'La Repubblica' la Italia.
"Ingawa kuna maoni tofautitofauti, hali iliyopo ni ya kiroho zaidi kuliko ya kisiasa au ya mivutano," alisema hayo jana.
‘Kiongozi mwenye ujasiri’
Kati ya makardinali 252 waliopo, ni 135 pekee wenye umri wa chini ya miaka 80 na hivyo kustahili kupiga kura kumchagua Papa mpya.

Takriban asilimia 80 ya wapiga kura hao waliteuliwa na Papa Francis mwenyewe lakini hilo si dhamana kuwa watamchagua mtu mwenye mtazamo sawa na wake.
Wengi wao ni vijana wa kati kwa umri na kwa wengi, huu utakuwa ni mkutano wao wa kwanza wa uchaguzi wa Papa.
Upigaji kura, unaofanyika ndani ya Kanisa la Sistine lililopambwa na michoro ya karne ya 16 ya Michelangelo, ni wa siri sana na hufuata taratibu kali na mila maalumu.

Mchakato huo unaweza kuchukua siku kadhaa, au hata zaidi, kabla ya kufikia muafaka.
Kila siku, upigaji kura hufanyika mara nne, mara mbili asubuhi na mara mbili jioni hadi mgombea mmoja apate angalau theluthi mbili ya kura. Chini ya nusu ya wapiga kura wanatoka Ulaya.
"Tunahitaji kiongozi jasiri, mwenye uthubutu, anayeweza kuliongoza Kanisa kwa msimamo thabiti hata katikati ya dhoruba, mtu atakayeleta utulivu katika enzi hii ya sintofahamu kubwa," anasema Ricardo Cruz