Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waombolezaji 250,000 waaga mwili wa Papa Francis

Muktasari:

  • Viongozi wakuu wa mataifa zaidi ya 150 wahudhuria ibada ya mazishi yanayofanyika leo Jumamosi Aprili 26, 2025.

Vatican. Waombelezaji takribani 250,000 wameshiriki kuaga mwili wa Papa Francis katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, shughuli iliyohitimishwa jana Ijumaa Aprili 25, 2025 kwa kufungwa jeneza lenye mwili wake.

Taarifa ya mtandao wa Vatican News inasema ibada ya kufunga jeneza ilifanyika saa 2:00 usiku (saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati) ikiwa ni maandalizi ya maziko yanayofanyika leo Aprili 26 kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.

Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa miongoni mwa marais walioshiriki kuaga mwili wa Papa Francis ni Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Pia inaelezwa wafalme, marais, mawaziri wakuu kutoka mataifa zaidi ya 150 duniani na maelfu ya waumini wanatarajiwa kushiriki misa ya mazishi ya Papa Francis (88) aliyefariki dunia Aprili 21, akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta.


Ibada ya kufunga jeneza

Ibada hiyo iliongozwa na Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma, Msimamizi wa Maadhimisho ya Liturujia, Kardinali Kevin Farrell.


Askofu Mkuu Diego Ravelli alisoma hati ambayo iliwekwa kwenye jeneza mwishoni mwa maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mujibu wa maagizo ya kanuni ya mazishi ya Papa wa Roma yalihitimishwa saa 3:00 usiku (saa 4:00 usiku zaa za Afrika Mashariki na Kati).

Papa Francis ambaye jina lake la kuzaliwa ni Jorge Mario Bergoglio aliyezaliwa Desemba 17, 1936 jijini Buenos Aires nchini Argentina ibada ya kufunga jeneza lake ilihudhuriwa pia na ndugu wa familia yake.

Miongoni mwa viongozi watakaohudhuria misa itakayofanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican ni Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye mara kadhaa aliingia katika mivutano na Papa Francis kutokana na kutofautiana mitazamo kuhusu sera ya uhamiaji.

Misa hiyo pia itahudhuriwa na marais wa Argentina, Ufaransa, Gabon, Ujerumani, Italia, Ufilipino, Poland na Ukraine. Mawaziri wakuu wa Uingereza na New Zealand, na pia familia za kifalme kutoka Ulaya.

Baada ya misa, jopo la viongozi wakuu kutoka sekretarieti kuu ya Vatican, litasindikiza mwili wa Papa hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu ambako atazikwa.

Wakati wa kuhamisha jeneza kupitia lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro maofisa wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali watakuwa upande mmoja wa nguzo za mawe wakitazamana na makardinali waliokaa upande mwingine.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ataongoza ibada ya mazishi na hatimaye kuzikwa Papa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.

Papa Francis aliyehudumu kwa miaka 12 alijikita kuwatetea maskini na waliotengwa, huku akizitaka nchi tajiri kuwasaidia wahamiaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akiwa na sifa ya unyenyekevu, anatarajiwa kuzikwa akiwa amebeba msimamo huo kukiwa na mabadiliko aliyoyafanya katika ibada za mazishi ya mapapa.

Wakati mazishi ya Papa Yohane Paulo II mwaka 2005 yalidumu kwa saa tatu, ibada ya leo Jumamosi, Aprili 26 inatarajiwa kuchukua dakika 90.

Katika wosia wa maisha ya kiroho, aliouandika Juni 29, 2022 Papa Francis aliomba kaburi lake liwekwe kwenye kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi.

Pia alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalumu bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.”

Italia imefunga anga la juu la Jiji la Vatican City na kupeleka majeshi ya ziada, yakiwamo makombora ya kujihami na ndege na boti za doria.

Baada ya maziko ya Papa Francis makardinali watakuwa na mkutano maalumu wa faragha kuchagua Papa mpya.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.