Ufahamu wosia wa Papa Francis, alichosema kuhusu kaburi lake

Muktasari:
- Papa Francis ambaye ameugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kiharusi (Stroke) amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.
Vatican. Wakati Wakristo wakiendelea kuomboleza kifo cha kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis. Wosia aliouacha umewekwa wazi ambapo alisisitiza mahali pa kuzikwa, aina ya mazishi na anayetoa gharama za mazishi hayo.
Papa Francis alifariki Jumatatu ya Aprili 21, 2025, asubuhi akiwa na umri wa miaka 88.
Katika wosia huo, Papa Francis ameeleza kwamba, lazima azikwe katika Kanisa Kuu la Bikira Maria lililoko Roma, Italia. Hivyo Papa Francis hatozikwa Vatican ambako mapapa wengi wamekuwa wakizikwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
"Miserando atque Eligendo
Kwa jina la Utatu Mtakatifu. Amina. Katika maisha yangu nimekuwa nikimtumainia Mama Bikira Maria daima, kwa sababu hii nizikwe kwenye kanisa hilo nikisubiri kufufuliwa siku ya ufufuo", imesema taarifa hiyo.
Papa Francis amekuwa akiishi maisha ya ufukara hali ambayo ameisisitiza kuhusu maziko yake kuwa yazingatie alichoandika katika wosia wake.
Wosia wake unaeleza kwamba, mazishi yake yasiwe ya kifahari na wala kaburi lake lisiwe na mapambo yoyote isipokuwa liandikwe jina lake tu la ‘Fransicus’.
Katika andiko la wosia huo, Papa Francis umeeleza kuwa gharama zote zimetolewa na mfadhili ambaye hakutajwa jina na zimekabidhiwa kwa Kardinali, Rolandas Makrickas.
Mwisho wa wosia wake Papa `Francis aliandika, "Mola awape thawabu ifaayo wale wote walionipenda na wanaoendelea kuniombea. Mateso ambayo yamenizonga katika kipindi cha mwisho cha maisha yangu, nayatoa kwa watu, kwa ajili ya amani duniani ya udugu kati ya undugu na kati ya mataifa.”
Sababu za kifo chake
Taarifa iliyotolewa na Vatican inaeleza kuwa kabla ya kufariki Papa Francis (88) aliugua ugonjwa wa kiharusi hali iliyosababisha moyo kushindwa kufanya kazi, huku ikidokeza kuwa madaktari walifanya jitihada kurudisha moyo katika hali ya kawaida lakini ilishindikana.
"Papa amefariki kutokana na kiharusi,” inaeleza sehemu ya taarifa rasmi ya sababu ya kifo cha Papa Francis iliyochapishwa katika ukurasa rasmi wa Vatican.
Hati ya kifo cha kiongozi huyo wa kiroho imetaja magonjwa mengine yaliyokuwa yanamsumbua, ni pamoja na homa ya mapafu, kushindwa kupumua, shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari.
Kwa taratibu za kimatibabu ugonjwa ambao mgonjwa huwa anakuwa nao muda mfupi au saa chache kabla ya kifo chake, ndio huwa unatajwa kwenye cheti cha kifo kama sababu ya kifo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.