Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Francis afariki dunia

Muktasari:

  • Papa Francis, Aprili 20, 2025 alikutana katika nyumba ya Mtakatifu Marta na Makamu wa Rais wa Marekani, James Vance.

Dar es Salaam. Papa Francis amefariki dunia leo Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88.

Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Vatican News, Papa Francis amefariki dunia akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta.

Kiongozi huyu wa Kanisa Katoliki na kiongozi wa Vatican, alizaliwa Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina na kubatizwa jina la Jorge Mario Bergoglio.

Papa Francis alichaguliwa Jumatano Machi 13, 2013 siku ya pili ya makutano ya makardinali. Alipata ushindi katika duru ya tano ya upigaji kura.

Katika maisha ya uongozi kiroho, amejulikana kwa unyenyekevu na msisitizo kuhusu huruma ya Mungu. Kimataifa anatambulika kwa kuwajali maskini.

Alichagua kuishi kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta (Domus Sanctae Marthae) inayotumiwa na wageni, badala ya kuhamia katika makazi ya kipapa.

Papa Francis amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kudumu ya mapafu, jambo ambalo kwa sehemu limechangia afya yake kuzorota.

Katika miaka ya hivi karibuni alikuwa akipata matatizo ya mafua, kikohozi, maumivu ya koo na kifua wakati wa baridi.

Pia, maumivu ya magoti na mishipa ya nyonga yalisababisha mara kwa mara atumie kitimwendo au mkongojo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari Vatican, Papa Aprili 20, 2025 alikutana katika nyumba ya Mtakatifu Marta na Makamu wa Rais wa Marekani, James Vance katika mkutano wa faragha uliodumu kwa dakika kadhaa.

Kwa mujibu wa habari kutoka Vatican, wawili hao walibadilishana matashi mema katika siku ya Pasaka.

Katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mji wa Roma na dunia kwa mwaka 2025, uliosomwa na mshereheshaji wa Liturujia za Kipapa, Papa Francis alitoa wito wa kusitishwa mapigano huko Gaza.

Katika ujumbe huo, pia alizungumzia kuhusu amani ya Ukraine na maeneo ya Afrika. Alitoa mwaliko wa kusaidia wakazi wa Myanmar waliokumbwa na tetemeko la ardhi.

Papa alisema hakuna amani bila kupokonywa silaha, akitoa wito wa kuheshimiwa uhuru wa kidini na kuachiwa wafungwa wa vita na wa kisiasa.


Tangazo la kifo chake

Kwa mujibu wa Vatican, tangazo la Camerlengo Kardinali Farrell kutoka nyumba ya Mtakatifu Marta imesema:

"Saa 1:35 asubuhi ya leo Jumatatu Aprili 21, Askofu wa Roma, Francisko alirudi kwenye nyumba ya Baba. Maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na Kanisa."

Kardinali Kevin Farrell alitangaza kifo cha Papa akisema: "Kaka na dada wapendwa ni kwa huzuni kubwa kwamba sina budi kutangaza kifo cha Baba yetu Mtakatifu Francisko. Saa 1:35 asubuhi ya leo, (Jumatatu Aprili 21, 2025), Askofu wa Roma, Francisko, alirejea nyumbani kwa Baba.”

Amesema maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na kanisa lake.

“Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu wote, hasa kwa kupendelea maskini zaidi na waliotengwa zaidi. Kwa shukrani nyingi kwa ajili ya kielelezo chake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunaiweka roho ya Papa Francisko kwa upendo wa huruma usio na kikomo wa Mungu mmoja na wa Utatu,” amesema.