Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasiojulikana wavamia nyumbani kwa kigogo wa CCM, wateketeza gari


Muktasari:

  • Watu wasiojulikana wamevamia nyumbani kwa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini na kuteketeza gari huku, waliokuwa ndani wakinusurika kuungua moto unaodaiwa kuwashwa usiku wa kuamkia leo Aprili 22, 2025.

Mbeya. Taharuki imetanda katika familia ya Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbeya Mjini, Philimon Mng'ong'o baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumbani hapo na kuchoma gari.

Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia leo Aprili 22, 2025 nyumbani kwa kiongozi huyo huku watu takribani 11 waliokuwa ndani wakinusurika kuungua moto huo,  ambao ulikuwa umeanza kuunguza vitu kwenye nyumba zilizopo eneo hilo.

Akizungumza nyumbani kwake kuhusiana na tukio hilo, Mng'ong'o ameeleza kuwa ni wiki moja tangu watu wasiojulikana kufika nyumbani hapo kuiba tairi jipya la gari hilo aina ya Nisan Xtrail.

Muonekano wa gari aina ya Nisan Xtrail, mali ya Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Philimon Mng'ong'o ambayo imechomwa moto usiku wa kuamkia leo Aprili 22, 2025 na watu wasiojulikana nyumbani kwake mtaa wa Isanga Kati, Mbeya.

Amesema pamoja na tukio hilo la kushtua na kushangaza, lakini hawezi kulihusisha na masuala ya kisiasa kwa kuwa hana tofauti na mtu yeyote iwe ndani au nje ya chama.

"Zaidi labda ni mambo ya kiuchumi, bado sijatoa taarifa katika matukio hayo, nimestuka na niombe vyombo vya dola vichunguze kubaini wahusika"

"Tukio limetokea kama saa 10 alfajiri ambapo mke wangu aliamka kwa ajili ya ibada ndio akasikia sauti ya moto, tulipotoka nje tukakuta umeanza kushika hizi nyumba za pembeni tukawapigia Zimamoto hawakupatikana haraka tukatumia mchanga na kufanikiwa kuuzima" amesema Mng'ong'o.

Kwa upande wake Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Isanga Kati, Bakari Yusuph amesema tukio hilo ni la kushtua ambapo mkakati wa Serikali mtaani hapo ni kuitisha mkutano wa dharura haraka kujadili matukio ya uhalifu ili kubaini wahusika.

Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbeya Mjini, Philimon Mng'ong'o.

Amesema wakati wakijipanga na hatua hizo za haraka, wanaliomba Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufuatilia zaidi ili kusaidia kuwabaini wahusika wa tukio hilo na mengine  na kuwachukulia hatua.

"Tukio hili ni la kwanza na limetushtua, kimsingi uongozi wa mtaa na kata nzima tutaenda kufanya mkutano wa dharura kujadili matukio haya na kuchukua hatua kwa wahusika ili kukomesha uhalifu huu, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vitusaidie" amesema Yusuph.

Mmoja wa wananchi, Diana Yusuph ambaye ni mpangaji katika nyumba hiyo, amesema hawaamini kilichotokea kwani ilikuwa ni tukio ambalo lingewasababishia vifo kutokana na muda uliotokea moto huo.

"Zaidi tunashukuru Mungu kutuokoa, vinginevyo familia zetu leo ingekuwa ni vilio, imetushtua sana haya matukio lazima yakomeshwe, Serikali iingilie kati" amesema Diana.

Akizungumzia tuko hilo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama hicho mkoani Mbeya, Christopher Uhagile amesema wameshangazwa na kitendo hicho, akieleza kuwa kwa sasa hawana maelezo mengi zaidi ya kujipa muda kutafakari zaidi.

"Chama hatuna taarifa yoyote kuhusu kiongozi wetu kuwa katika mgogoro wa namna yoyote na mtu ndani au nje ya chama, kimsingi tunajipa muda kutafakari tunaamini tutakuja na picha nzima" amesema Uhagile.

Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha tukio hilo akieleza kuwa bado hajapata undani zaidi, akiahidi baadaye kuweza kulitolea maelezo.

"Ni kweli nimesikia taarifa hiyo, kwa sasa nipo Kyela nikirudi naweza kulielezea zaidi" amesema Kamanda Kuzaga.