Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu auawa akidhaniwa mwizi

Mwalimu Fredrick Nyambo enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 15, 2025, katika Mtaa wa Mwanyanje, Kata ya Igawilo, ambako marehemu alikuwa akiishi.

Mbeya. Fredrick Nyambo (40), Mwalimu wa Shule ya Sekondari Hayombo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana waliomdhania kuwa ni mwizi.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 15, 2025, katika Mtaa wa Mwanyanje, Kata ya Igawilo, ambako marehemu alikuwa akiishi.

Akizungumza na Mwananchi leo, Alhamisi Aprili 17, 2025, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanyanje, Joseph Ndambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kwa mujibu wa Ndambo, alipokea simu kutoka kwa wananchi Aprili 15,2025 wakimjulisha kuhusu tukio la mauaji ya mwalimu huyo, ambapo mwili wake ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igawilo.

Mke mdogo wa marehemu Grace Simlapa akieleza namna alivyopata taarifa ya kifo cha mumewe.

“Nilipata mshtuko baada ya taarifa hizo, ndipo nilipoelekea hospitalini na kuingia chumba cha kuhifadhia maiti, ambako nilithibitisha kuwa mwili ni wa mwalimu Nyambo,” amesema Ndambo.

Amesema mwalimu Nyambo hakuwa na historia ya kuhusika na uhalifu, alikuwa mtu mwema, mcheshi na mwenye ushirikiano mzuri na majirani.

“Nimeishi naye kwa miaka kadhaa, alikuwa mwalimu mwaminifu, hajawahi kutuhumiwa kwa wizi wala ugomvi. Hili tukio limeniacha na masikitiko makubwa,” amesema Ndambo.

Akizungumzia tukio hilo,   Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dk Yesaya Mwasubila amesema Nyambo alipokelewa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo Aprili 16, 2025, saa 3 asubuhi akiwa na majeraha makubwa kichwani.

“Majeraha hayo yalisababisha madhara kwenye mishipa ya fahamu na kuvuja damu nyingi. Alikuwa akilalamika kwa maumivu makali wakati akiendelea kupatiwa matibabu, lakini alifariki dunia muda mfupi baada ya kuanza kuhudumiwa,” amesema Dk Mwasubila.

Ametoa rai kwa jamii kuwa na utaratibu wa kuwapeleka majeruhi hospitalini haraka, hasa wenye majeraha ya kichwani ili kunusuru maisha yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema baadhi ya watu wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi unaendelea.

“Kuna watu tunawashikilia kwa ajili ya mahojiano. Tutarudi na taarifa kamili baada ya kukamilisha uchunguzi,” amesema Kamanda Kuzaga.


Kauli za wake wa marehemu

Anatalia Mahenge, mke mkubwa wa marehemu, amesema alipigiwa simu na askari aliyemtaka afike Kituo cha Polisi Uyole akimwambia mumewe amejeruhiwa kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana.

“Nilienda mara moja na nikamkuta mume wangu akiwa amelala chini, hali yake ilikuwa mbaya sana, alikuwa amepigwa mapanga, tukamchukua na kumpeleka hospitali, lakini akafariki wakati anaanza kutibiwa,” amesimulia Anatalia huku akilia.

Ameliomba Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla ichunguze tukio hilo na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kutekeleza mauaji hayo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwanjanje Kata ya Igawilo, Joseph Ndambo alieleza namna alivyopata taarifa.

“Naomba Serikali itupe msaada ili haki ipatikane kwa mume wangu. Ni maumivu makubwa mno,” amesema Anatalia.

Grace Simpanga, mke mdogo wa marehemu amesema kwa mara ya mwisho walizungumza na mumewe Jumanne mchana.

“Jioni nikapigiwa simu na rafiki yangu kuniuliza kama nimewasiliana na mume wangu jioni, nilimjibu hapana, akaniambia nimpigie, nikapata  mashaka na kumuomba anieleze kama kuna jambo, hakutaka akaniambia mpigie tu,” amesimulia Grace.

Amesema baada ya kujishauri, akaamua kupiga simu ya mumewe, ikapokelewa lakini hakusikia sauti yake badala yake alisikia sauti za watu wengine wakizungumza pembeni na aliyepokea hakuzungumza kitu.

Amesema mumewe amewaachia watoto sita kwa wake zako hao wawili.

Akizungumzia tukio hilo, Aloyce Jumanne, mkazi wa Uyole, ameitaka Serikali na vyombo vya dola kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

“Kumekuwa na tabia ya watu kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuua wenzao. Serikali iweke sheria kali dhidi yao huenda ikakomesha vitendo hivi vya kinyama,” amesema Jumanne.