Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maelfu wauaga mwili wa Papa Francis

Muktasari:

  • Mwili wa Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 utazikwa Jumamosi hii ya Aprili 26, 2025 katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu.

Vatican. Umati wa waamini umeendelea kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Papa Francis kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, shughuli inayoendelea hadi kesho Ijumaa Aprili 25, 2025 saa 2:00 usiku (saa za Afrika Mashariki na Kati).

Inaelezwa hadi kufikia saa 3:30 asubuhi ya leo Alhamisi Aprili 24, watu 48,600 wameshatoa heshima zao kwa mwili wa Papa.

Taarifa kupitia mtandao wa Vatican News inaeleza Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambaye ni ‘Camerlengo’ Mkuu wa Kanisa Katoliki, ataongoza jopo la viongozi wakuu kutoka sekretarieti kuu ya Vatican kufunga jeneza lenye mwili wa Papa.

Pia ataongoza jopo la viongozi wakuu kutoka sekretarieti kuu ya Vatican, kusindikiza mwili wa Papa hadi kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu.

Jumamosi Aprili 26, 2025 Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ataongoza ibada ya mazishi na hatimaye kuzikwa Papa kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu.

Papa Francis (88), aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta, alikabidhi maisha na huduma yake ya kipadre na kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Katika wosia wake aliomba maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, akingojea siku ya ufufuo wa wafu.

Kardinali Farrell, Jumatano Aprili 23, aliwaongoza waamini kutoa heshima zao za mwisho, shughuli inayoendelea kufanyika.

Baada ya jeneza lenye mwili wa Papa kuhamishwa kutoka Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican, Aprili 23 asubuhi, waumini waliruhusiwa kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 12:30 asubuhi ya leo Aprili 24, kutoa heshima za mwisho. Waliendelea na shughuli hiyo kuanzia saa 2:00 asubuhi (saa za Afrika Mashariki na Kati).

Taarifa ya Vatican News inasema hadi kufikia saa 3:30 asubuhi ya Aprili 24, watu 48,600 wameshatoa heshima zao kwa mwili wa Papa.


Mkutano wa makardinali

Katika hatua nyingine, makardinali 103 jana jioni, Aprili 23, 2025 walishiriki mkutano mkuu wa pili katika ukumbi wa Sinodi, mjini Vatican na kuidhinisha ratiba ya Novendiali (yaani siku tisa) za maadhimisho ya ekaristi kwa ajili ya Papa Francis.

Maadhimisho hayo yataanza misa ya mazishi Aprili 26, 2025 na kuhitimishwa siku ya tisa ambayo ni Dominika ya Mei 4, katika Basilika ya Vatican.

Miongoni mwa makardinali waliohudhuria mkutano huo ni Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican News, liturujia ziko wazi kwa wote, lakini kwa ushiriki wa kila siku kwa kikundi tofauti kwa kuzingatia uhusiano wake na Papa wa Roma.

Katika taarifa iliyochapishwa na ofisi ya vyombo vya habari imebainishwa kwamba: "Aina hii ya makusanyiko inaonyesha kwa namna fulani, upeo wa huduma ya mchungaji mkuu na umoja wa Kanisa la Roma."

Taarifa hiyo imesema makardinali katika mkutano huo walianza kwa sala ya ‘Uje Roho Mtakatifu’ na kisha maombi kwa ajili ya Papa Francis. Baadaye makardinali ambao hawakuwa wamekula kiapo waliapa.

Mkutano mwingine wa makardinali ulitarajiwa kufanyika leo Aprili 24 saa 4:00 asubuhi (saa za Afrika Mashariki na Kati).