Maneno ya mwisho ya Papa Francis

Muktasari:
- Papa Francis alipumzika alasiri na kula chakula cha jioni kwa utulivu. Ilikuwa yapata saa 11:30 alfajiri dalili za kwanza za ugonjwa zilipoonekana.
Vatican. "Asante kwa kunirudisha kwenye uwanja." Ni miongoni mwa maneno ya mwisho ya Papa Francis aliyoyatoa kwa ambao katika wakati wa ugonjwa, lakini hata muda mrefu uliopita, walimwangalia bila kuchoka.
Miongoni mwa hao ni Massimiliano Strappetti, muuguzi ambaye kama alivyowahi kusema Papa aliokoa maisha yake kwa kupendekeza afanyiwe upasuaji wa tumbo.
Papa alimteua kuwa msaidizi wake wa afya tangu mwaka 2022.
Kando yake kwa siku zote 38 za kulazwa katika Hospitali ya Gemelli na saa 24 kwa siku, wakati akiendelea kupumzika katika nyumba ya Mtakatifu Marta, Strappetti alikuwa na Papa Dominika ya Pasaka Aprili 20, wakati wa Baraka.
Siku moja kabla walikwenda kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ili kukagua ‘njia’ ya kupita siku ambayo ingefuata wakati Papa Francis angetokea katikati ya Kanisa Kuu kwa ajili ya kutoa baraka.
Baada ya muda huo wa Dominika asubuhi, kwenye balkoni ambayo ni kitovu cha mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, wakati waamini 35,000 wa awali walikuwa tayari wameongezeka na kufikia 50,000, Papa alitaka kufanya ‘sapraiz’, muhimu kwenda kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro kuzunguka kwa kutumia kigari maalumu. Bila hofu ya awali: "Je, unafikiri ninaweza kufanya?" Alimuuliza Strappetti ambaye alimtuliza. Kutoka huko kukumbatia umati na hasa watoto. Huu ulikuwa mzunguko wa kwanza baada ya kutoka hospitalini Gemelli na wa mwisho wa maisha yake.
Akiwa amechoka lakini mwenye furaha, Papa Francis alimshukuru msaidizi wake binafsi akisema: “Asante kwa kunirudisha kwenye uwanja.” Maneno ambayo yanafichua hitaji la Papa wa Argentina, ambaye ameonyesha alama ya upapa wake kwa kurejea kati ya watu kabla ya kurudi kwa Baba Mungu.
Saa za mwisho
Papa Francis alipumzika alasiri na kula chakula cha jioni kwa utulivu. Ilikuwa yapata saa 11:30 alfajiri dalili za kwanza za ugonjwa zilipoonekana na uingiliaji wa haraka wa wale waliokuwa wanamtazama.
Kwa zaidi ya saa moja baadaye, baada ya kumpungia mkono Strappetti aliyekuwa amelala katika nyumba yake kwenye ghorofa ya pili ya nyumba ya Mtakatifu Marta, Papa aliingia katika hali ya kukosa fahamu.
Hakuteseka, yote yalitokea kwa haraka, alisema mtu aliyekuwa karibu naye katika dakika hizo za mwisho.
Kifo chake kilitokea siku iliyofuata ya Pasaka, siku moja baada ya kuubariki mji wa Roma na dunia (Urb et Orbi).
Imeandikwa na Angella Rwezaula wa Vatican News.