Makardinali 103 waidhinisha ratiba maadhimisho ya ekaristi kwa ajili ya Papa

Vatican. Makardinali 103 jana jioni, Aprili 23, 2025 walishiriki mkutano mkuu wa pili katika ukumbi wa Sinodi, mjini Vatican na kuidhinisha ratiba ya Novendiali (yaani siku tisa) za maadhimisho ya ekaristi kwa ajili ya Papa Francis.
Maadhimisho hayo yataanza na misa ya mazishi Aprili 26, 2025 na kuhitimishwa siku ya tisa ambayo ni Dominika ya Mei 4, katika Basilika ya Vatican.
Miongoni mwa makardinali waliohudhuria mkutano huo ni Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, nchini Tanzania.
Papa Francis (88), alifariki dunia Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta.
Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican News, liturujia ziko wazi kwa wote, lakini kwa ushiriki wa kila siku kwa kikundi tofauti kwa kuzingatia uhusiano wake na Papa wa Roma.
Katika taarifa iliyochapishwa na ofisi ya vyombo vya habari imebainishwa kwamba: "Aina hii ya makusanyiko inaonyesha kwa namna fulani, upeo wa huduma ya mchungaji mkuu na umoja wa Kanisa la Roma."
Taarifa hiyo imesema makardinali katika mkutano huo walianza kwa sala ya ‘Uje Roho Mtakatifu’ na kisha maombi kwa ajili ya Papa Francis. Baadaye makardinali ambao hawakuwa wamekula kiapo waliapa.