Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zimamoto waiokoa familia iliyovamiwa na nyuki nyumbani


Muktasari:

  • Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limefanikiwa kuwaondoa nyuki waliokuwa wamejenga makazi kwenye mabanda ya njiwa na mti uliokuwa karibu na nyumba

Morogoro. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, limemuokoa Abina Kiasi na familia yake baada ya nyuki kuvamia nyumba yao iliyopo Mtaa wa Bomba la Zambia, Kata ya Kingolwira, Manispaa ya Morogoro.

Mbali na kuwaokoa, jeshi hilo pia limefanikiwa kuwaondoa nyuki hao waliokuwa wamejenga makazi kwenye mabanda ya njiwa na mti uliokuwa karibu na nyumba hiyo, hali iliyosababisha familia hiyo kujifungia ndani tangu Aprili 26.

Akizungumza na Mwananchi jana baada ya kuiokoa familia hiyo, Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Sajenti Alexander Makuluni amesema walipofika eneo la tukio walifanikiwa kuwaondoa nyuki kisha kuikomboa familia hiyo iliyokuwa imejifungia ndani.

"Tumeondoa makazi ya nyuki waliokuwa wamejenga ukutani na kwenye mti, kisha tukapuliza dawa ya kuwafukuza. Mpaka tunamaliza kazi na kuondoka, nyumba pamoja na maeneo ya jirani yalikuwa salama, hakuna mtu aliyepata madhara wakati wa shughuli  nzima," amesema Sajenti Makuluni.

Pia, amesema baada ya kuwahamisha nyuki hao, wamemshauri mama huyo na familia yake kutoingia mara moja nyumbani kutokana na uwepo wa nyuki wachache waliokuwa bado wanaranda hewani, hivyo walimshauri kurejea nyumbani kwake usiku kwa usalama zaidi.

Kwa upande wake, Abina amelishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa msaada waliompatia, lakini pia ameeleza mshangao wake kuhusu tabia ya nyuki hao ambao licha ya kuondolewa, walikuwa wakirudi tena na kuhatarisha usalama wa familia.

"Mimi tangu nizaliwe sijawahi kuona nyuki wa namna hii. Leo wanahamishwa, kesho wanarudi. Lakini namuamini Mwenyezi Mungu, ndiye anayejua kama hawa nyuki ni wa heri au wa shari," amesema Abina.

Amesema licha ya kuondolewa, bado wanaishi kwa tahadhari kubwa kwa kuwa hawana uhakika kama nyuki hao wameondoka kabisa au watarejea kama ilivyokuwa awali.

"Nawashukuru askari wa zimamoto wamenielekeza kuwa endapo nyuki hao watarudi tena, niwajulishe mara moja ili waweze kuja kunisaidia," amesema Abina.